Michezo

Guardiola hataki Messi atoke Barcelona

May 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Pep Guardiola amefutilia mbali tetesi zinazomhusisha nyota Lionel Messi na uwezekano wa kubanduka Barcelona na kujiunga na kikosi chake cha Manchester City msimu ujao.

Kwa mujibu wa mkufunzi huyo mzawa wa Uhispania, kubwa zaidi katika matamanio ya Messi ni kustaafu katika ulingo wa soka akivalia jezi za Barcelona ambao wamekuwa wakijivunia huduma zake kwa kipindi cha miaka 16 iliyopita.

Japo Messi, 32, amekuwa mchezaji wa Barcelona tangu utotoni, mkataba wake una kipengee kinachomruhusu kuagana na waajiri wake wa sasa mwishoni mwa msimu wowote na kujiunga na kikosi chochote kingine akipendacho bila ya ada yoyote.

Guardiola ni miongoni mwa wakufunzi waliochangia zaidi kuimarika kwa makali ya Messi wakati akidhibiti chombo cha miamba hao wa Uhispania uwanjani Camp Nou kati ya 2008 na 2012.

Katika kipindi hicho, Guardiola aliwaongoza Barcelona kunyanyua mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na mawili ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Atasalia Barcelona. Hilo ndilo tamanio lake na langu pia,” akasema Guardiola ambaye amewahi pia kuwatia makali masogora wa Bayern Munich nchini Ujerumani.

Guardiola aliyoyomea Ujerumani kuwanoa Bayern baada ya kujivunia ufanisi mkubwa wa kunyanyua jumla ya mataji 14 chini ya kipindi cha misimu minne pekee kambini mwa Barcelona.

Akiwa Ujerumani, aliwaongoza Bayern kutawazwa mabingwa wa Bundesliga kwa misimu mitatu mfululizo. Aliwaongoza Man-City kutia kapuni mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika kipindi cha mihula miwili iliyopita.

Messi ambaye mkataba wake na Barcelona unatamatika mwishoni mwa 2021, anajivunia kutawazwa mshindi wa Ballon d’Or mara sita. Isitoshe, amewaongoza Barcelona kutwaa jumla ya mataji 10 ya La Liga na manne ya UEFA.

Zaidi ya kukorofishana na wenzake wakiwa mazoezini hivi majuzi, kinachotarajiwa kumchochea Messi kubanduka Barcelona ni tukio la wiki hii lililomshuhudia akitofautiana vikali na mkurugenzi wa soka wa kikosi hicho, Eric Abidal aliyedai kwamba wachezaji hawakujituma zaidi wakati wote walipokuwa chini ya aliyekuwa kocha wao, Ernesto Valverde.

Ingawa Man-City wanapigiwa upatu wa kumsajili Messi iwapo nyota huyo mzawa wa Argentina atahiari kuagana na Barcelona, Guardiola ameshikilia kwamba hataki kabisa kuingizwa katika mgogoro wa Messi na Abidal ambao ni wachezaji wake wa zamani ugani Camp Nou.

Uwepo wa Ferran Soriano na Txiki Begiristain kambini mwa Man-City ni suala jingine ambalo huenda likamsukuma Messi kuwa mwepesi wa kutua uwanjani Etihad. Wawili hao, ambao kwa sasa ni wasaidizi wa Guardiola katika kikosi cha Man-City, pia ni wachezaji wa zamani wa Barcelona.

Mbali na Man-City, vikosi vingine vinavyohemea pakubwa fursa adhimu ya kumsajili Messi ni Manchester United, Paris Saint-Germain (PSG), Bayern Munich, Inter Milan na Juventus ambao tayari wanajivunia maarifa ya Cristiano Ronaldo ambaye alikuwa mshindani mkuu wa Messi katika soka ya Uhispania. Ronaldo aliyeagana na Real Madrid ya Uhispania misimu miwili iliyopita, amewahi pia kuchezea Man-United.

Kwa mujibu wa magazeti mengi ya Uingereza na Gazzetta dello Sport nchini Italia, Man-City na Juventus ndivyo vikosi vilivyopo pazuri zaidi kujivunia huduma za Messi ambaye kwa sasa hupokezwa mshahara wa hadi Sh160 milioni kwa wiki.

Licha ya vikosi hivi kujivunia uwezo wa kumdumisha Messi kimshahara, huenda nyota huyo akahiari pia kutua PSG katika hatua itakayomshuhudia akiungana na fowadi wa zamani wa Barcelona, Neymar Jr.

Barcelona walimtimua kocha Valverde mwanzoni mwa mwaka huu licha ya kikosi chake kuselelea kileleni mwa jedwali la La Liga na kumwajiri Quique Setien kutoka Real Betis.