Michezo

Guardiola sasa ahisi ushindani wa EPL

October 21st, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amekiri kwamba ukubwa wa viwango vya ushindani katika kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ni wa kutisha.

Man-City ambao ni mabingwa watetezi wa EPL kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini kwa alama 19 baada ya kuwatandika Crystla Palace 2-0 mnamo Jumamosi katika uwanja wa Selhurst Park.

Ingawa hivyo, Guardiola anahisi kwamba kusuasua kwa kikosi chake katika mechi nane za kwanza za kampeni ya msimu huu ni jeraha ambalo linatarajiwa kumweka nje beki Aymeric Laporte hadi Februari 2020.

“Msimu jana, mshindi wa taji la EPL alikuwa tayari ameanza kujulikana baada ya kupigwa kwa jumla ya mechi nane za ufunguzi. Hali ni tofauti kabisa muhula huu. Majeraha pia yametulemaza. Ushindani ni mkubwa na hakuna kikosi kinachotabirika,” akasema Mhispania huyo ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich.

Kutokuwepo kwa Laporte kunamsaza Guardiola katika ulazima wa kuendelea kutegemea huduma za mabeki wawili pekee wazoefu; John Stones na Nicolas Otamendi.

Amesisitiza kwamba hili ni jambo ambalo litamchochea kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho wa wachezaji mwanzoni mwa mwaka 2020.

Wakicheza dhidi ya Palace, Man-City walifunguliwa ukurasa wa mabao na Gabriel Jesus katika dakika ya 39 kabla ya Bernardo Silva kupachika goli la pili wavuni dakika mbili baadaye.

Kufunga mabao zaidi

Man-City wangalifunga mabao zaidi iwapo kipa Wayne Hennessey wa Palace angalizembea langoni na kutoyadhibiti vilivyo makombora ya Silva, Jesus, Sergio Aguero na Kevin De Bruyne.

Man-City walikuwa katika ulazima wa kusajili ushindi katika mchuano huo hasa baada ya chombo chao kuzamishwa kwa 2-0 na Wolves katika mechi ya awali. Ushindi kwa Man-City dhidi ya Palace una maana kwamba kwa sasa wamesajili ushindi mara 12 kutokana na mechi 14 za EPL ambazo wamezipiga ugenini hadi kufikia sasa mwaka huu.

Katika mapambano yote ya awali, Man-City wamevuna ushindi katika mechi 16 kutokana na michuano 19 iliyopita dhidi ya Palace huku wakipachika wavuni jumla ya mabao 47.