Michezo

Guendouzi afichua alivutiwa na mastaa wa zamani ugani Emirates

September 25th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

MWANADIMBA chipukizi Matteo Guendouzi amekiri kwamba mapenzi yake kwa mastaa wa zamani Therry Henry na Patrick Vieira ndiyo yalimchochea kujiunga na mibabe wa soka ya ligi ya Uingereza, EPL, Arsenal.

Kinda huyo mwenye  umri wa miaka 19 aliyesajiliwa na The Gunners kutoka Lorient ameibukia kama mwanasoka hodari kambini mwa mabingwa hao wa zamani wa FA kutokana na kiwango cha juu cha uchezaji kati safu ya kati.

“Nilipokuwa nakua nilitazama timu nyingi lakini nikajipata napenda Arsenali zaidi. Wachezaji Thierry Henry na Patrick Viera walinifanya nipende klabu na niwe na ndoto ya kuisakatia,” akasema Guendouzi wakati wa mahojiano na shirika la habari za spoti la L’Equipe.

Mfaransa huyo msimu huu wa 2018/19 ameanza mechi  tano kati ya sita  za ligi Arsenal imewajibikia na vile vile alicheza kwa dakika 33 kwenye ushindi wa 4-2 dhidi ya Vorskla katika ligi ya Uropa.