Michezo

Guendouzi aonywa kwa ukosefu wa nidhamu

June 25th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HUKU Arsenal ikijiandaa kuzuru Southampton kwa mechi muhimu ya Ligi Kuu ya Uingereza leo Alhamisi usiku, kiungo Matteo Guendouzi ameonywa na kocha Mikel Arteta dhidi ya kuenda kinyume na maadili ya klabu hiyo yake.

Guendouzi aligonga vichwa vya habari kwa utovu wa adabu dhidi ya Brighton & Hove Albion mnamo Juni 20, 2020, alipoonekana kukaba koo Mfaransa mwenzake Neal Maupay na kumsukuma baada ya kipenga cha mwisho kulia.

Mshambuliaji Maupay, ambaye alikuwa amechezea kipa Bernd Leno visivyo, alifunga bao la ushindi ‘wanabunduki’ wakizimwa na Brighton 2-1 ugenini.

Guendouzi, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Lorient, pia alisuta wapinzani wao.

Si mara ya kwanza Guendouzi, 21, ameudhi kocha huyo Mhispania aliyeamua kutomchezesha mnamo Februari 16 dhidi ya Newcastle kwa sababu mtazamo hasi mazoezini.

Arteta sasa amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Uingereza akisema kuwa anataka kushughulikia suala la Guendouzi kwa njia ya faragha, ingawa alikumbukusha mchezaji huyo kuwa anahitaji kudumisha viwango bora vya maadili.

“Tuna tamaduni nyingi tofauti katika timu yetu. Kila mtu ameelimishwa kwa njia tofauti na lazima nielewe na kukubali. Hata hivyo, lazima tufahamu kuwa kuna njia inayostahili kufuatwa, tuna vitu tunavyofaa kufanya, tuna maadili na haustahili kuvuka mipaka,” alisema Arteta.

Shirikisho la Soka Uingereza limethibitisha kuwa Guendouzi hatachukuliwa hatua kwa tabia yake dhidi ya Maupay.

Dhidi ya Southampton, Arsenal itakuwa mawindoni kulipiza kisasi cha kulimwa 3-2 ilipozuru uwanjani St Mary’s mara ya mwisho Desemba 16, 2018. Katika mechi hiyo, Danny Ings alifungia Southampton mabao mawili ya kwanza naye Henrikh Mkhitaryan akapachika magoli ya Arsenal kabla ya Charlie Austin kupatia wenyeji bao la ushindi dakika ya 85.

Kabla ya hapo, Arsenal ilikuwa imetoka na alama moja uwanjani humu ilipotoka 1-1. Ushindi wa mwisho wa Arsenal uwanjani St Mary’s ulipatikana Mei 2017 kupitia mabao ya Alexis Sanchez na Olivier Giroud, ambao wanachezea Inter Milan na Chelsea, mtawalia.