Makala

Gugu lisilopendwa na mifugo sasa latangazwa janga Kajiado

June 3rd, 2024 2 min read

STANLEY NGOTHO NA LABAAN SHABAAN

SERIKALI ya Kaunti ya Kajiado imetangaza gugu sugu la Ipomea kuwa janga la kaunti sababu ya athari yake kwa malisho ya mifugo. 

Sifa ya mmea huu ya kuenea na kuathiri mazao mengine imeibua hatari kwa utoshelevu wa chakula cha mifugo na binadamu. 

Ukijulikana na jamii ya Wamaasai kwa jina ‘oltiameleteti,’ gugu hili limezagaa hadi asilimia 40 ya kaunti baada ya kugunduliwa mwaka wa 1997 katika kipindi cha mvua za El Nino.

Hatari hii imemsukuma Gavana wa Kajiado Joseph Lenku kuzindua zoezi la kung’oa mizizi ya Ipomea katika gatuzi hilo.

Wafugaji pia wametakiwa kuhusika katika harakati hiyo.

Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku akiongoza shughuli ya kung’oa gugu kwa jina Ipomea ambalo haliliwi na mifugo na asali itokayo kwa maua yake hufanya walaji kusinzia. Picha|Stanley Ngotho

“Magugu haya yamekuwa hatari kwa utoshelevu wa chakula. Yamestawi sababu ya matumizi mabaya ya ardhi pamoja na kulisha mifugo katika sehemu ndogo ya malisho. Njia ya pekee inayoweza kutokomeza magugu haya ni kuyang’oa,” alisema Gavana Lenku katika sherehe ya Madaraka mnamo Jumamosi.

Vile vile, anaomba washikadau kushirikiana nao ili kumaliza magugu hayo pamoja na kukuza malisho ya mifugo.

“Hata kama serikali ya kaunti inaendesha programu kadhaa kutokomeza magugu na kuimarisha ufugaji, juhudi za ziada za kifedha zinahitajika,” aliongeza, akisema kuwa watafiti wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) wameanzisha utafiti wa hali ya juu kuondoa magugu kisayansi.

Seneta wa Kajiado Samuel Seki anaomba Wizara ya Kilimo kupiga jeki maeneo kame iepuke hatari hii kupitia Bunge La Seneti.

“Serikali kuu na ya kaunti zinafaa kutenga fedha kumaliza magugu haya kupitia mpango kama ule wa ‘Kazi Mitaani’ katika kaunti zilizoathiriwa,” aliomba Seneta Seki.

Kulingana na Mkurugenzi wa Kaunti wa masuala ya Mifugo Eric Aheda, mmea huu una uwezo wa kuzaa sana na kusambaa kiasi cha kuharibu mazao ambayo ni malisho ya mifugo.

Kuharibu malisho ya mifugo

“Licha ya mvua nyingi, hivi karibuni, wafugaji watakosa malisho sababu ya athari ya magugu haya,” aliteta Bw Aheda.

Katika Kaunti Ndogo za Kajiado Magharibi, Kusini, Kati, Mashariki na Kaskazini, athari ya Ipomea ni bayana.

“Mmea usiopendwa na mifugo umeenea haraka sana. Ufugaji wa ng’ombe utakuwa na shida siku za usoni,”  alilalama Bw Moses Lenkaso ambaye ni mfugaji.

Mfugaji mwingine, Bw Sankare Japan, ameambia Taifa Leo kwamba gugu hilo limeathiri pia biashara za asali katika kaunti hiyo.

“Magugu haya yenye maua mengi huvutia nyuki lakini asali inayozalishwa hufanya walaji kusinzia baada ya kula. Asali ya mmea huu ina thamani ya chini kwa hivyo wateja hawana haja nayo,” alisema.

Magugu hayo yalifanya ukame mkali wa 2020-2022 ulioshuhudiwa Kajiado kuwa mbaya zaidi.

Wakati huo, mamia ya mifugo iliathiriwa na kiangazi, hali iliyotikisa utoshelevu wa chakula asilia kwa jamii.

Kulingana na takwimu ya Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (NDMA), angalau familia 350 zilikumbwa na baa la njaa.

Nayo mauzo ya kila mwaka ya sekta ya mifugo ya Sh 3.2 bilioni yamepungua hadi Sh1 bilioni katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.