Makala

GUGUMAJI ZIWANI: Jukumu la kwanza la Raila AU

January 23rd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI upinzani Raila Odinga Ijumaa alitekeleza wajibu wake wa kwanza kama Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Ustawi wa Miundo Msingi alipozindua mradi ya kuzoa gugumaji kutoka Ziwa Victoria ili kukwamua uchukuzi katika ziwa hilo.

Bw Odinga alieeleza imani kuwa juhudi sasa zitafanikiwa kutokana na moyo wa muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta uliotiwa saini mnamo Machi 9,2018.

Mipango kadhaa ya awali ya kuondoa mimea hiyo hatari, ambayo imetatiza uchukuzi na uvuvi katika ziwa hilo, haijakuwa ikifua dafu katika kile kilichotajwa kama ukosefu wa nia ya kisiasa katika kuifanikisha.

Bw Odinga ambaye pia ni kiongozi wa ODM alisema ushirikiano kati yake na Rais umeleta mwamko mpya katika siasa ya kanda ya Afrika Mashariki na kuipa Uganda shime ya kushirikiana na Kenya kuimarisha uchumi ya eneo la Ziwa.

“Hii ndio maana Uganda ni mshirika mkuu katika mchakato huu mpya wa kuondoa gugumaji na uimarishaji wa fuo za Kenya ambao utapiga jeki shughuli za uchukuzi wa abira, mizigo pamoja na uvuvi katika Ziwa Victoria,” akasema katika bandari ya Kisumu.

Bw Odinga alisema hayo alipoongoza halfla ya uzinduzi wa mradi mpya wa kuzoa gugumaji kutoka Ziwa Victoria na kupanua fuo kadhaa kama njia ya kuimarisha uchukuzi na uvuvi.

Kiongozi huyo wa Odinga pia alizindua merikebu maalum yenye uwezo wa kuondoa gugumaji na kuondoa kuchimbua mchanga na kuimarisha fuo za ziwa hilo, shughuli ambayo pia ilihudhuriwa na Naibu Mwenyekiti wa chama tawala nchini Uganda, NRM, George Michael Mukula.

“Mradi huo ni muhimu kwani utaimarisha biashara katika ya Kenya na mataifa jirani ya Uganda na Tanzania, hatua ambayo itayageuza kuwa kitovu cha ustawi wa kiuchumi barani Afrika,” akasema huku akiahidi kutumia wadhifa wake katika AU kuisaka ufadhili zaidi kwa mradi huo.

Bw Odinga alisema kazi hiyo ambayo inalenga kuendelea hadii mwezi wa Juni mwaka huu itaimarisha shughuli katika bandari ya Kisumu ambayo imetelekezwa kwa miaka mingi.

“Shughuli hii ambayo inasimamiwa na Muungano wa Kiuchumi wa Eneo la Ziwa na kampuni ua Mangoe Tree Ltd kutoka Uganda itapelekea kujenga mwa mtaro wenye upana wa mita 80 na urefu wa kilomita 63 kutoka Kisumu hadi Mbita,” akaongeza, akisema hatua hiyo itawezesha meli za kusafirisha mizigo na mafuta hadi mataifa jirani kutia nanga kwa urahisi.

Shughuli ya upanuzi zitaendeshwa katika fuo za Muhuru, Kendu Bay, Sori bay, Port Victoria, Asembo Bay na Karungu Bay nchini Kenya.

Eneo ambalo limewavimiwa zaidi na gugumajio hilo ni Ghuba la Winam lenye shughuli nyingi na ambalo limesambaa hadi kaunti ya Homa Bay.

Shughuli hiyo itaendeshwa kwa kutumia merikebu maalum ambayo iliwasili Kisumu mnamo Alhamisi wiki hii.

Akiongea katika bandari ya Kisumu baada ya kuwasili kwa merikebu hiyo Meneja wa Halmshauri ya Bandari Nchini (KPA) anayesimamia Uchukuzi wa Maziwa Javan Wanga alisema shughuli hiyo itadumu kwa miezi 30 na katika eneo la umbali wa kilomita 62.

Alisema ukingo wa ziwa utachimbwa hadi kufikia kina cha mita sita ili kuruhusu meli yenye mizigo mizito kutia nanga.

“Mchanga na aina nyingi za taka zimekusanyika katika gati kwa kipindi kirefu hali ambayo hutatiza meli zinapotia nanga,” akasema Bw Wanga.

Afisa huyo aliongeza kuwa chini ya mpango huo, ufuo wa ziwa utapanuliwa hadi kiwango cha mita 80 ili kuziwezesha meli mbili kutia nanga kwa wakati mmoja.

Merikebu hiyo, kwa jina Mv Mangoe Treee, chenye urefu wa mita 70, ina uwezo wa kuzoa na kubeba tani 4,000 ya gugumaji kwa wakati mmoja.

Naibu Gavana wa Kisumu Dkt Mathews Owili ambaye alikuwepo wakati wa uzinduzi wa mradi huo na merikebu alisema kuondolewa kwa gugumaji ziwani huo ni sehemu ya mpango wa serikali kwa kuimarisha uchukuzi na uvuvi katika ziwa hilo kubwa barani Afrika.