Michezo

Guikan agura Gor, ayoyomea Zambia

January 29th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MSHAMBULIZI wa Gor Mahia raia wa Ivory Coast Ephrem Guikan hatimaye ameondoka klabuni humo huku ripoti zikiashiria kwamba anaelekea kusakatia klabu moja kubwa nchini Zambia.

Haya yanajiri baada ya Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia kueleza Taifa Leo kwamba Guikan alikataa jina lake lisijumuishwe katika orodha ya wanasoka watakaoshiriki mechi za kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika(CAF).

Majina ya wanasoka wenzake, Dennis Oliech, Nicholas Kipkurui na Geoffrey Ochieng hata hivyo yaliongezwa kwenye orodha ya awali kisha yakakabidhiwa CAF.

“Tumeamua kumwaachilia Guikan baada yake kutuambia tumpe barua ya kuagana nasi. Hata hivyo sijui anakoelekea japo alinidokezea kwamba anaenda Zambia. Sisi kama Gor Mahia hatuna jingine ila kumtakia kila la kheri,” Bw Aduda akaeleza TaifaLeo.

Hata hivyo, Guikan mwenyewe alikataa kueleza ni klabu gani atasakatia nchini Zambia ingawa alifichua kwamba ni mojawapo ya klabu kubwa zaidi nchini humo.

Mchezaji huyo amekuwa na wakati mgumu kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Gor Mahia chini ya aliyekuwa mkufunzi Dylan Kerr na mrithi wake Hassan Oktay.

Awali ilibidi uongozi wa Gor Mahia kujitokeza mara kadhaa na kukanusha kwamba walikuwa wamemwaachilia Guikan huku mchezaji mwenyewe akizidisha sarakasi ndani na nje ya uwanja akilalamikia kulishwa benchi.

Gor watacheza dhidi ya SoNy Sugar katika mechi ya Ligi Kuu nchini(KPL) Jumatano Januari 30 kisha ifunge kamepeni ya mechi zake za makundi za CAF dhidi ya Zamalek ya Misri siku ya Jumapili Februari 3 2019.