HabariSiasa

Gumzo kuhusu Mau lachacha, viongozi wataka kikao na Rais

September 2nd, 2019 2 min read

NA ERICK MATARA

MJADALA kuhusu mpango wa serikali wa kuwafurushwa watu kwenye msitu wa Maasai Mau Jumatatu uliendelea kuchacha, viongozi na wazee kutoka Bonde la Ufa sasa wakiomba kuandaa mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu operesheni inayonukia baada ya makataa ya Oktoba 31.

Mbunge wa Kuresoi Joseph Tonui, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee kutoka Bonde la Ufa Gilbert Kabage na Kinara wa wazee wa Ogiek Joseph Towett walisema ni Rais Kenyatta pekee ambaye anaweza kuyaokoa maisha ya maelfu ya raia ambao wanakodolewa macho na mahangaiko makubwa serikali ikiwaondoa msituni humo.

“Tutafanya kila tuwezalo kukutana na Rais Uhuru Kenyatta na kusuluhisha utata huu ambao umeibua taharuki kati ya jamii mbalimbali. Iwapo suala hili halitatuliwa basi kutatokea janga kubwa la kibinadamu litakalowaathiri watahiniwa wa mitihani ya kitaifa mwaka huu,” akasema Bw Tonui.

Mbunge huyo wa chama cha Jubilee aliongeza kuwa hatima ya wanafunzi 8,000 na watahiniwa 1,000 sasa ipo mikononi mwa Rais na kumwomba aunde jopo la wataalamu ili kupendekeza suluhu kwa masuala tata yanayozingira msitu huo kila mara.

Kwa upande wake, Mzee Towett alisema wanaunga kikamilifu juhudi za kuhifadhi msitu huo unaotegemewa na mamilioni ya watu ila akaomba serikali kushughulikia suala hilo kwa makini bila kudhuru raia.

“Ili kuzima taharuki ya kijamii inayoendelea kupanda kati ya jamii zinazoishi kwenye msitu, serikali lazima iunde jopo la wataalamu kusuluhisha utata wa ardhina dhuluma za kihistoria ndani ya Mau,” akasema Mzee Towett.

Wito wa kumtaka Rais Kenyatta kuingilia suala hilo linajiri baada ya viongozi wa jamii ya Kalenjin wiki jana kumwomba Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko kuwa na kikao nao huku serikali ikiwapa zaidi ya familia 60,000 muda wa siku 60 kuondoka msituni au zifurushwe kwa nguvu.

Bw Kabage naye alilaumu utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi kwa hali ya sasa akisema kuruhusiwa kwa jamii moja kujitwalia vipande vikubwa vya ardhi ndiyo kiini cha uhasama wa kikabila msituni humo.

“Umefika wakati ambao suala hili la Mau linafaa kutatuliwa mara moja badala ya kuwaacha wanasiasa kulitumia kila mwaka wa uchaguzi kutafuta kura,” akasema Bw Kabage.