Michezo

GUMZO LA SPOTI: Barcelona waizima Arsenal kwenye kipute cha Gamper

August 6th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

BARCELONA, UHISPANIA

BAO la dakika ya mwisho ya mchezo kutoka kwa mvamizi Luis Suarez liliwavunia Barcelona ushindi wa 2-1 dhidi ya Arsenal mnamo Jumapili usiku na hivyo kutia kapuni ubingwa wa Joan Gamper Trophy uwanjani Nou Camp.

Katika mchuano huo ambao ulikuwa wa mwisho kwa Arsenal kujifua kwa msimu mpya, kocha Unai Emery aliwajibisha wengi wa wachezaji wake wa kikosi cha kwanza.

Arsenal walijipa uongozi katika dakika ya 36 kupitia kwa fowadi Pierre-Emerick Aubameyang aliyeshirikiana vilivyo na chipukizi Joe Willock, 19.

Hata hivyo, Arsenal walirejea kwa kipindi cha pili kwa matao ya juu na wakafaulu kusawazisha kupitia kwa beki Ainsley Maitland-Niles aliyejifunga katika dakika ya 69.

Suarez ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, alitokea benchi na kuzamisha kabisa chombo cha matumaini ya Arsenal walioongoza kwa kipindi kirefu.

Nahodha Lionel Messi alisalia benchi katika vipindi vyote viwili vya mchuano huo uliomshuhudia sajili mpya wa Barcelona Antoine Griezmann akiwajibishwa kwa muda mrefu zaidi mbele ya mashabiki 98,812 waliofika ugani Nou Camp.

Bao la Griezmann aliyesajiliwa kutoka Atletico Madrid kwa kima cha Sh14 bilioni mwezi jana, lilikataliwa na refa kwa madai kuwa alikuwa ameotea. Bao hilo lilikuwa zao la ushirikiano kati ya Griezmann na kiungo Ivan Rakitic.

Tegemeo Aubameyang 

Bila ya sajili wao mpya Nicolas Pepe aliyewagharimu Sh9.3 bilioni kutoka Lille ya Ufaransa, Arsenal walisalia kumtegemea pakubwa Aubameyang aliyemzidi maarifa beki Jordi Alba kabla ya kucheka na nyavu.

Bao hilo liliwaamsha Barcelona ambao katika kipindi cha kwanza, walimtegemea mvamizi Ousmane Dembele aliyenyimwa nafasi nyingi za wazi na kipa Bernd Leno.

Mbali na Willock na Eddie Nketiah, chipukizi mwingine aliyetamba zaidi kambini mwa Arsenal katika mchuano huo ni Bukayo Saka, 17.

Arsenal kwa sasa wanajiandaa kufungua kampeni za EPL dhidi ya Newcastle United wikendi hii.