Dondoo

Gunia la miraa latolewa kanisani kama sadaka

May 10th, 2018 1 min read

Na LEAH MAKENA

MUTUATI, MERU

Polo wa eneo hili alishangaza waumini wa kanisa moja kwa kupeleka gunia la miraa kanisani kama sadaka ya kutoa shukrani kwa mavuno mema.

Yasemekana pasta wa kanisa hilo alikuwa amekubali washiriki kutoa mavuno kama sadaka.

Kwa kawaida, mavuno hayo huuzwa na pesa zinazopatikana hutumiwa kwa miradi ya kanisa.

Inasemekana kuwa waumini wengi walipeleka aina mbali mbali ya vyakula.

Hata hivyo, polo mmoja aliamua kupeleka gunia la veve kanisani akisema alikuwa amefanikiwa kupata mavuno mazuri na hangekosa kutoa shukrani kwa Maulana.

Pasta alishangaa alipofungua gunia na kupata miraa. Alimlaumu jamaa kwa kudharau kanisa lakini alijitetea akisema hakuona makosa yoyote kushukuru Mungu kwa baraka alizomjalia.

“Kama huwa mnakubali pesa ninazotoa sadaka nikiuza miraa mbona msikubali zao lenyewe? Isitoshe, mko na faida kwa sababu huwa ninauza kwa bei ya juu sana na hivyo kanisa litafaidi mkifanyia kazi zaka hiyo,” polo aliongeza.

Waumini walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa pasta alimkemea polo kwa kitendo chake na kumtaka kuondoka na gunia lake la miraa. Alisema hangekubali biashara ya vileo kanisani.

Jamaa alilazimika kurejea nyumbani na gunia lake akimlaumu pasta kwa kumbagua na kukataa kukubali zaka yake ilhali kwa miaka mingi amekuwa akikubali pesa zinazotokana na zao hilo.

Alidai pasta alijifanya kwa sababu anajua waumini wengi ni wakulima wa miraa na hiyo ndiyo njia yao ya kujitafutia riziki.

Alisema pasta alifaa kuombea zao hilo ili lizidi kunawiri wakazi wapate pesa zaidi na kutoa sadaka nono apate kufaidika.

…WAZO BONZO…