Gunners wakamatia chini Newcastle FC!

Gunners wakamatia chini Newcastle FC!

Na MASHIRIKA

RISASI mbili za Arsenal zilitosha kuyumbisha Newcastle kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Emirates, jana.

Baada ya kushuhudia rekodi ya kutoshindwa katika mechi 10 mfululizo kwenye mashindano yote, ikipigwa breki kali kwa kichapo cha 4-0 kutoka kwa Liverpool wikendi iliyopita, Arsenal walijinyanyua jana kwa kuwatandika wageni wao hao kwa mabao ya kipindi cha pili.

Newcastle ya kocha Eddie Howe ilishuka dimbani ikiwinda ushindi wa kwanza msimu huu, baada ya kuambulia sare ya 3-3 dhidi ya Brentford katika mchuano uliopita ligini.Ushindi wa Arsenal, ambao sasa wanajivunia alama 23 baada ya mechi 13, uliweka hai matumaini yao ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora, na hivyo kushiriki Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal sasa wamejizolea alama 16 kutokana na mechi sita zilizopita za EPL.

Rekodi sawa na hiyo inajivuniwa na mabingwa watetezi Manchester City na Chelsea – ambayo ndiyo klabu ya pekee kuangusha Arsenal nyumbani Emirates msimu huu.Arsenal hawajawahi kushindwa na kikosi kinachoshuka dimbani kupepetana nao kikivuta mkia EPL.

Hata hivyo, wanajivunia idadi sawa ya mabao (15) ambayo pia yamefungwa na Newcastle katika mechi 13 zilizopita ligini.Mechi ya jana ilikuwa ya saba mfululizo kwa Newcastle kupoteza dhidi ya Arsenal bila kufunga bao. Mara ya mwisho kwa Newcastle kufunga bao ugani Emirates ligini ni 2014.

Kikosi hicho kwa sasa kinakokota nanga kwenye jedwali la EPL kwa pointi sita, baada ya kupiga sare sita na kupoteza mechi saba.Hii leo, Manchester United watakuwa wageni wa Chelsea katika gozi litakalowakutanisha uwanjani Stamford Bridge, wanapodizi kutarajia kocha Ralf Rangnick kupewa fursa ya kushikilia mikoba yao.

Nao Everton wataendea limbukeni Brentford, Leicester waalike Watford, Tottenham Hotspur wakwaruzane na Burnley ugenini, nao West Ham wapimane ubabe na mabingwa watetezi Manchester City uwanjani Etihad.Man-City watakuwa na motisha tele baada ya kucharaza Paris Saint-Germain (PSG) 2-1 katika pambano lililopita la UEFA.

West Ham ya kocha David Moyes itakuwa pia na ari ya kuendelea kuwika baada ya kuzamisha Rapid Vienna ya Austria 2-0 katika mechi ya Europa League mnamo Alhamisi.Ushindi kwa Man-City utaendeleza presha kwa Chelsea ambao wameshinda mechi tisa, kusajili sare mara mbili na kupoteza mechi moja kati ya 12 za hadi kufikia sasa.

Ushindi dhidi ya PSG ulikuwa wa nne mfululizo kwa Man-City kusajili katika mashindano yote na wa nane kutokana na michuano 10 iliyopita ya nyumbani. West Ham watakuwa wakipania kuwa kikosi cha kwanza kufunga Man-City katika EPL nyumbani msimu huu.

Blues watajibwaga ugani wakidhibiti kilele cha jedwali kwa alama 29 kutokana na mechi 12. Ni pengo la pointi 12 linalotenganisha Chelsea na Man-United wanaonolewa na kiungo wao wa zamani, Michael Carrick, tangu Ole Gunnar Solskjaer apigwe kalamu wikendi iliyopita sababu ya matokeo duni.

Sawa na Man-United waliopepeta Villarreal 2-0 katika mchuano wao wa UEFA, Chelsea pia watajitosa ulingoni wakipania kuendeleza ubabe uliowazolea ushindi mnono wa 4-0 dhidi ya Juventus katika mechi iliyopita ya kivumbi hicho.Mechi dhidi ya Juventus ilikuwa ya tisa kwa Chelsea kushinda kati ya 10 zilizopita katika mashindano yote.

Kufikia sasa, Chelsea wanajivunia alama tatu zaidi kuliko Man-City na wamefungwa idadi ndogo zaidi ya mabao (manne) kutokana na michuano 12 ya EPL. Hata hivyo, matatu kati ya magoli hayo yametokana na mechi ambazo masogora hao wa kocha Thomas Tuchel wametandaza nyumbani.

Bao la Matej Vydra katika sare ya 1-1 iliyosajiliwa na Chelsea dhidi ya Burnley mnamo Novemba 6 ugani Stamford Bridge ndilo bao la pekee ambalo miamba hao wamefungwa kutokana na dakika 450 zilizopita ligini.Japo uvumi kuhusu uwezekano wa Mauricio Pochettino kutua ugani Old Trafford kudhibiti mikoba ya Man-United unazidi kushika kasi, mabingwa hao mara 20 wa EPL wamepania kuaminia Rangnick fursa ya kuwaongoza hadi mwisho wa msimu huu wa 2021-22.

Man-United watategemea maarifa ya Carrick kwa mara nyingine baada ya kiungo huyo wa zamani kusuka njama iliyowezesha The Red Devils kukomoa Villarreal ugenini na kutinga hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo Jumanne.Mechi tano kati ya saba zilizopita ambazo Man-United walitandaza chini ya Solskjaer ligini zilikamilika kwa vichapo huku miamba hao wakikosa kushinda mechi mbili mfululizo katika mapambano yote muhula huu tangu wapigwe 2-1 na Young Boys kwenye UEFA mnamo Septemba 14.

Ingawa Chelsea wanapigiwa upatu wa kushinda, Man-United wanajivunia rekodi nzuri ya kutopigwa na Chelsea katika mechi saba zilizopita ligini. Aidha, Chelsea hawajawahi kufunga Man-United katika michuano minne iliyopita.Pigo la pekee kwa Chelsea ni majeraha yatakayowaweka nje wanasoka Ben Chilwell, N’Golo Kante, Mateo Kovacic na Kai Havertz.

Man-United watakuwa bila maarifa ya Raphael Varane, Paul Pogba, Edinson Cavani, Luke Shaw na Harry Maguire anayetumikia marufuku baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi iliyopita dhidi ya Watford uwanjani Vicarage Road.RATIBA YA EPL (Leo):Brentford vs Everton (5:00pm)

Man-City vs West Ham (5:00pm)Leicester vs Watford (5:00pm)Burnley vs Tottenham (5:00pm)Chelsea vs Man-United (7:30pm)

You can share this post!

Shujaa yajizolea alama 10 Dubai 7s ikimaliza ya nane

Marufuku ndege za Afrika Ulaya

T L