Habari

Gusa Matiang'i uone – Raila

May 25th, 2019 2 min read

Na RUTH MBULA na JOSIAH ODANGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amewakashifu vikali wale wanaomlaumu Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuhusiana na sakata ya dhahabu ghushi, akisema kuwa ni mweupe kama pamba.

Alisema wanaomtaja Dkt Matiang’i ni wasiofurahishwa na bidii yake ya kuchapa kazi, na hawatafaulu.

Bw Odinga alikubali kwamba alisafiri nchini Dubai majuzi, ambapo alikutana na kiongozi wa Milki ya Kiarabu (UAE) Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum kuhusiana na sakata hiyo.

Akihutubu Ijumaa katika Kaunti ya Kisii, Bw Odinga alisema kwamba wahusika wa biashara hiyo ni matapeli.

“Matiang’i hahusiki kwa vyovyote vile katika sakata hii. Mwacheni,” alisema.

Alisema kuwa watu wanaomshambulia Matiang’i wanafanya hivyo kwa sababu amekuwa akifanya kazi yake kwa njia ifaayo, kama waziri anayesimamia vitengo vyote vya usalama nchini.

“Wanajaribu kumpaka tope. Tunawajua. Hawatafaulu,” akasema.

Bw Odinga alikuwa akihutubu katika eneobunge la Kitutu Chache Kaskazini, kwenye mazishi ya Dkt David Ombati, aliyekuwa daktari wa kibinafsi wa babake, marehemu Jaramogi Oginga Odinga.

Waliohudhuria hafla hiyo akiwemo ndugu yake Oburu Odinga, Gavana wa Kisii James Ongwae, Mwakilishi wa Wanawake Janet Ong’era, Seneta Sam Ongeri na mbunge wa Kitutu Chache Kusini Richard Onyonka walimtetea vikali Dkt Matiang’i.

Alisema kuwa Dkt Matiang’i hapaswi kupakwa tope, na kuwa wahusika wakuu wanapaswa kukabiliwa kwani wanajulikana.

Mfichuzi

Alisisitiza kwamba ndiye aliyefichua sakata hiyo na nyingine za ufisadi nchini, na kuwa maafisa wa upelelezi wanaendelea kuichunguza.

“Nilimwambia kiongozi huyo kwamba sauti iliyonaswa kwa simu si ya Dkt Matiang’i. Nilimwambia kwamba ninajua sauti ya Matiang’i na kuwa wahusika walikuwa wakitumia jina lake kuendeleza maslahi yao,” alisema.

Inadaiwa kuwa kiongozi huyo alikuwa ameeleza tashwishi kuhusu dhababu ambayo ilidaiwa ingesafirishwa Dubai kupitia Kenya.

Katika mazungumzo ya simu yaliyowekwa mtandaoni wiki iliyopita, sauti ya mtu anayesemekana kuwa Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula inasikika ikitaja jina la Dkt Matiang’i, Bw Odinga na Rais Kenyatta.

Hilo lilimfanya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji kuagiza uchunguzi wa kina kuhusu mazungumzo hayo.

Lakini Ijumaa, Bw Odinga alisema kuwa kiongozi huyo alilaghaiwa.

Alisema alimwambia kuwa watu aliokuwa akishirikiana nao kwenye biashara hiyo ni walaghai.

Baadhi ya washirika wa karibu wa Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakimshinikiza waziri Matiang’i kujiuzulu kwa madai kwamba anapaswa kuwaeleza Wakenya anayojua kuhusu sakata hiyo.

Miongoni mwa viongozi hao ni mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa, ambaye amekuwa akimtetea vikali Dkt Ruto.

“Ni vipi unaweza kuwatumia polisi wa GSU kuwalinda wale wanaohusika katika sakata hiyo?” akasema mnamo Jumamosi iliyopita, kwenye kauli iliyoonekana kumlenga Dkt Matiang’i.

Bi Jumwa alisema kuwa Kamati ya Bunge Kuhusu Usalama itamwagiza Matiang’i kufika mbele yake kuelezea nchi alivyohusika katika sakata hiyo.

Dkt Ruto pia alikuwa katika hafla hiyo katika eneo la Endebess, Kaunti ya Trans Nzoia.