Kimataifa

Guterres ataka nchi kuendelea kutoa misaada kwa raia Gaza

January 28th, 2024 1 min read

NA AFP

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres ameyasihi mataifa fadhili kuendelea kufanya hisani kwa shirika lake la misaada kwa wakimbizi Palestina (UNRWA).

Hii ni baada ya mataifa kadhaa kusitisha ufadhili wao kwa shirika hilo kuhusiana na tuhuma kwamba wafanyakazi wake walihusika katika shambulio lililotekelezwa na Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023.

“Ingawa naelewa malalamishi yao, binafsi nilishangazwa na tuhuma hizi. Kwa hivyo, natoa wito kwa serikali zilizositisha misaada yao kuirejesha ili shughuli za UNRWA ziendelee,” Guterres akasema kwenye taarifa aliyotoa mnamo wikendi.

Israel imedai kuwa wafanyakazi wengi wa shirika la UNRWA walihusika katika shambulio lililotekelezwa na Hamas, hali iliyochangia nchi kadha fadhili kusitisha misaada yao kwake.

Shirika hilo limewafuta kazi wafanyakazi kadha kufuatia madai hayo ya Israel huku likiahadi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo.

Wakati huo huo, Israel imeapa kusitisha shughuli za shirika hilo katika Gaza baada ya mapigano yanayoendelea sasa.

Mvutano kati ya Israel na UNRWA unajiri kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa kuhusu Haki (ICJ) uliotolewa Ijumaa kwa sharti Israel ikomesha mauaji ya halaiki Gaza na iruhusu misaada zaidi kufika eneo hilo.

“Vitendo vya wafanyakazi hao wa UNRWA sharti vikomeshwe na waadhibiwe vikali,” Guterres akasema.

“Lakini makumi ya maelfu ya wanaume na wanawake wanaohudumia UNRWA, katika mazingira hatari, hawafai kuadhibiwa,” akaongeza.

“Mahitaji ya watu wanaowahudumia sharti yatimizwe,” Guterres akasema.

Katibu huyo Mkuu wa UN alithibitisha wafanyakazi 12 wa UNRWA waliotajwa katika tuhuma hizo, ambazo umoja wa mataifa unachunguza.

“Tisa wamefutwa kazi, mmoja amekufa na wengine wawili wanaendelea kutambuliwa,” Guterres akaongeza.