Michezo

GUU ANFIELD: Liverpool yawinda Mbappe

January 10th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

BAADA ya Liverpool kusaini dili nzito na kampuni ya Nike kwa mkataba unaoweza kuiletea klabu hiyo Sh10 bilioni kila mwaka The Reds imepata nguvu za kumtwaa kinda mahiri wa PSG, Kylian Mbappe.

“Iwapo watakuwa na nia ya kumsajili (Mbappe), nguvu zao za kifedha katika siku zijazo zitakuwa nyingi, kwa hivyo wako katika nafasi nzuri ya kumsajili. Ila sidhani kama wana lengo la kumsajili upesi,” akasema mtaalamu wa kuvumisha bidhaa na huduma za michezo Alan Seymour kuhusu mwansoka huyo wa PSG ambaye hufunga mabao kila anapotaka na kwa njia aipendayo.

Kwingineko, Arsenal na Manchester United zimeingia vitani kuwania saini ya kiungo mshambuliaji mahiri, Edison Cavani wa Paris Saint-Germain (PSG).

Straika huyo mwenye umri wa miaka 32 amecheza mechi nne pekee za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu huu baada ya kusumbuliwa na jeraha mbali na kukosa namba kutokana na upinzani mkali kutoka kwa Mauro Icardi.

Mkataba wake na PSG unamalizika mwishoni mwa msimu huu na sasa anatarajiwa kuwa huru iwapo atakataa mkataba mpya.

Kulingana na habari katika vyombo vya habari barani Ulaya, staa huyo raia wa Uruguay, kadhalika anawindwa na Atletico Madrid huku kuwapo na tetesi kwamba tayari klabu hiyo ya Uhispania imeanzisha mazungumzo na maajenti wake, na huenda akaanza kucheza chini ya Diego Simeone.

Pia kuna uvumi kwamba Chelsea inmfuatilia nyota huyo ambaye ameifungia PSG mabao 196 katika mechi 290.

Lakini kocha wake Thomas Tuchel anataka staa huyo aendelee kuichezea PSG.

“Imekuwa vigumu kwake kurejea katika kiwango chake bora tangu aumie.”

“Amepoteza makali yake, wakati wenzake wanazidi kuimarika. Lakini itabidi aendelee kujitahidi wakati akiwa hapa. Nina hakika ataendelea kuichezea PSG, kwa sasa siamini vingine.”

Wakati huo huo, Mauro Icardi aliifungia PSG mabao matatu na kuisaidia kutinga nusu-fainali ya French League Cup baada ya ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Saint-Etienne.

Mshambuliaji huyo wa Inter Milan anayechezea vigogo hao kwa mkopo alipata bao la kwanza dakika ya pili, kabla ya Neymnar kuongeza la pili.

Jessy Moulin alijifunga katika juhudi za kuokoa hatari na kufanya mambo kuwa 3-0 kufikia wakati wa mapumziko.

Icardi aliongeza mengine mawili kabla ya Kylian Mbappe kumimina wavuni bao la sita.

Yohan Cabaye- zamani mchezaji wa Newcastle United aliwafungia Saint-Etienne bao la kufutia machozi, muda mfupi baada ya penalti yake kuokolewa na kipa Sergio Rico.

Saint-Etienne chini ya Claude Puel – zamani kocha wa Southampton na Leicester City- walionyesha soka safi lakini wakachanganyikiwa baada ya Fofana kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea ngware Angel di Maria.

PSG walichukua usukani na kutawala mchezo huo katika kipindi cha pili, huku Mbappe na Icardi wakivuruga ngome ya wapinzani wao.

Bao la Mbappe lilikuwa la 19 msimu huu. Etienne walipewa penalti baada ya Di Maria kumchezea ngware Charlles Abi.

Timu nyingine zilizofuzu kwa nusu-fainali ni Stade Reims, Lyon na Lille.

Wakati huo huo, mpachikaji mabao stadi Emmanuel Adebayor wa Togo anatarajiwa kujiunga na moja ya klabu za EPL.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 35, huenda akasajiliwa na Aston Villa wakati wowote kuanzia sasa.

Adebayor ambaye aliwahi kuchezea Arsenal, Manchester City na Tottenham Hotspur aliwahi kufunga mabao 97 katika mnechi 243 akichezea timu hizo.