Michezo

GUU MAN-U: Lewandowski atarajiwa kutua Old Trafford nayo Arsenal ikitarajiwa pia kusajili vifaa kwa fujo

May 17th, 2019 3 min read

Na MASHIRIKA

BERLIN, Uingereza

HUKU kipindi kirefu cha uhamisho nchini Uingereza kikifunguliwa usiku wa kuamkia jana, wafuasi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) huenda wakaanza kushabikia mchana-nyavu matata wa Bayern Munich, Robert Lewandowski hivi karibuni ikiwa Manchester United itashinda Paris Saint-Germain katika vita vya ubabe vya kumsaini kigogo huyo.

Mbali na Manchester United, pia Chelsea, Tottenham, Arsenal zilizomaliza ligi katika nafasi za tatu, nne na tano katika usanjari huo, zinatarajiwa kuwa na shughuli nyingi sokoni katika kipindi hiki.

Zitalenga kuziba mwanya kati yazo na Manchester City na Liverpool zilizokamilisha katika nafasi mbili za kwanza kwa alama 98 na 97 mtawalia.

Man City wanatarajiwa kuachilia Vincent Kompany, Fernandinho na David Silva na kumnunua Joao Felix kutoka Benfica na Rodri kutoka Atletico Madrid.

Hii ni iwapo hawatachukuliwa hatua za kinidhamu na shirikisho la soka la Ulaya (UEFA) kwa kutumia pesa zilizozidi kiwango kusajili hapo awali.

Arsenal, ambayo mkurugenzi mpya wa kiufundi Edu ni shabiki mkubwa wa Wilfried Zaha wa Crystal Palace, inatarajiwa kutengana na Danny Welbeck na Aaron Ramsey.

Naye Mkenya Victor Wanyama anayechezea Tottenham, Victor Wanyama ni mmoja wa wachezaji wanaohusishwa na uhamisho.

City pia inaaminika kutenga Sh19.4 bilioni kwa shughuli ya kujisuka iwapo itaponea kuadhibiwa na UEFA.

Kuhusu Lewandowski, ripoti katika jarida la Kicker nchini Ujerumani zilisema jana kwamba raia huyu wa nchi ya Poland anatupiwa macho na PSG na United.

Inasemekana kwamba Lewandowski, ambaye kandarasi yake na Bayern itatamatika Juni 30 mwaka 2021, hakufurahia mipango ya waajiri wake kutaka kumuongeza mwaka mmoja pekee katika kandarasi yake, ishara kwamba mchezaji huyo alitaka kandarasi ya muda mrefu.

“Kwa wakati huu, amepokea ofa kutoka kwa Manchester United na Paris Saint-Germain,” jarida hilo lilichapisha.

Mshambuliaji huyu atakayesherehekea kufikisha umri wa miaka 31 mnamo Agosti 21 mwaka huu, amefungia Bayern mabao 189 katika mechi 240 tangu ajiunge nayo kutoka Borussia Dortmund mwaka 2014.

Amekuwa akihusishwa sana na kuyoyomea katika klabu zingine kubwa barani Ulaya.

Katika kipindi kirefu cha mwaka 2018, Lewandowski alihusishwa na Real Madrid kabla ya hatimaye kuamua kusalia mjini Munich.

Katika mahojiano na jarida hilo mwezi Machi, Lewandowski alisema yuko tayari kuongeza kandarasi yake na Bayern.

“Tumeshafanya mazungumzo ya mwanzo, lakini itachukua muda kwa sababu wakati huu, akili yangu yote iko katika kumaliza msimu msimu,” alisema.

“Hata hivyo, ni kweli ninaweza kufikiria kuwa hapa kwa muda mrefu.”

Januari 2018, ripoti nchini Ujerumani zilisema kwamba Manchester United na Real Madrid zinamezea mate Lewandowski zikidai kwamba Bayern iko tayari kusikiza ofa za zaidi ya Sh9 bilioni. Lewandowski aliondoka Borussia Dortmund bila ada ya uhamisho baada ya kandarasi yake kumalizika na kujiunga na Bayern mwaka 2014.

Anaaminika kuwa mchezaji anayekula mshahara mkubwa Bayern wa Sh38.9 milioni kila wiki nchini Ujerumani.

United wakati huu inalipa raia wa Chile, Alexis Sanchez Sh65.5 milioni kila wiki na kambi ya Lewandowski iliweka wazi kwamba haitakubali aondoke uwanjani Allianz Arena asipopata nyongeza nzuri ya mshahara, ambayo ni ya kiwango sawa na cha Sanchez.

United huenda isipate nyota huyu, hasa kutokana na kuwa ilimaliza Ligi Kuu ya msimu 2018-2019 nje ya mduara wa nne-bora na kukosa tiketi ya kushiriki Klabu Bingwa Ulaya.

Kocha wa PSG, Thomas Tuchel anasemakana angependa kuwa na Lewandowski katika kikosi chake ambacho kina mastaa Neymar, Kylian Mbappe, Edinson Cavani na Julian Draxler na wengineo.

Shughuli

Huku hayo yakijiri, mahasimu Manchester United na Arsenal pamoja na Tottenham Hotspur wanaongoza orodha ya klabu zinazodhaniwa kuwa zitakuwa na shughuli nyingi kabla ya soko kufungwa Agosti 8.

Manchester City, ambayo inakabiliwa na kesi ya kuvunja sheria ya kutotumia fedha kuliko kiasi unachopata kusajili wachezaji, pamoja na Chelsea inayopigania kuondolewa marufuku ya kutosajili wachezaji katika vipindi viwili vya uhamisho, zinaaminika zitakuwa na shughuli nzito sokoni zikikwepa marufuku.

Liverpool, ambayo ilitumia fedha nyingi kuliko klabu nyingine za EPL katika kipindi kirefu kilichopita (Sh22.9 bilioni), inatarajiwa kuwa na shughuli chache wakati huu.

Wengine walio katika mpango wa kuhama ni Philippe Coutinho (Barcelona), Nicolas Pepe (Lille), Jadon Sancho (Borussia Dortmund), Julian Brandt (Bayer Leverkusen) na Gareth Bale (Real Madrid) ni baadhi ya silaha zinazohusishwa na Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) litafungua soko la kimataifa hapo Juni 11.

Tetesi zinasema Eden Hazard (Chelsea), Leroy Sane (Manchester City) na Alexis Sanchez (Manchester United) ni baadhi ya wachezaji walio mbioni kuuzwa.

Klabu nchini Uingereza zinaweza kuanza kuviziana, lakini zitalazimika kusubiri hadi Juni 11 kutafuta vifaa nje ya nchi hiyo.

Zilitumia Sh160.9 bilioni katika kipindi kirefu kilichopita. Kipindi kirefu cha uhamisho nchini Uhispania kitafunguka Julai 1 na kufungwa Septemba 2, huku mahasimu wa tangu jadi Real Madrid na Barcelona wakitarajiwa kutetemesha sokoni.

Inasemakana Real inajiandaa kuuza wachezaji 14 akiwemo Bale ili kununua.

Ligi ya Ujerumani pia itaruhusu klabu kujitosa sokoni Julai 1 hadi Septemba 2, huku mahasimu Bayern Munich na Dortmund wakiaminika hawakosa shughuli hiyo muhimu ya kujiandaa kwa msimu 2019-2020.

Nchini Italia, kipindi cha uhamisho cha Serie A kitafunguka Julai 1, lakini kitafungwa mapema mnamo Agosti 23. Juventus imehusishwa na majina kadhaa makubwa. AC Milan na Inter wanaaminika pia wanajiandaa kujiimarisha.

Shughuli ya kununua na kuuza wachezaji katika Ligi Kuu ya Ufaransa itafanyika kati ya Juni 16 na Septemba 2.