Habari

Gwiji Kadenge kuzikwa nyumbani Vihiga

July 18th, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

GWIJI wa soka, Joe Kadenge, atazikwa Jumamosi mtaani Gesambai eneo la Tiriki katika Kaunti ya Vihiga.

Mwanasoka huyo mstaafu aliyekuwa na umri wa miaka 84 aliaga dunia Julai 7, 2019, akitibiwa katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuzidiwa na maumivu ya kiharusi.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga aliwaongoza marafiki na jamaa wa marehemu katika ibada ya misa Jumatano jijini Nairobi katika kanisa la Friends International, Nairobi ambako wengi walimsifu Kadenge kama mwanasoka matata aliyetumia kipaji chake kusaidia wengi.

Wakati wa ibada hiyo, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula aliwahimiza wabunge kubuni mbinu za kuhakikisha maslahi ya magwiji mastaafu yanaafikiwa ili kuimarisha mchezo huo nchini kwa jumla.

Ni kauli ambayo ambayo pia ilitiliwa mkazo na umuhimu mkubwa na kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi ambaye alilitaka bunge libuni sharia itakayoboresha maisha ya wanamichezo walioiletea nchi sifa kupitia kwa michezo mbali mbali.

John Nyawanga ambaye walicheza naye alisema Kadenge alijumuishwa katika kiwango kimoja na magwiji waliovuma enzi hizo akiwemo Pierre Ndaye Mulamba ambaye alifunga jumla ya mabao tisa katika michuano ya AFCON iliyofanyika nchini Misri mnamo 1974. Mulamba aliaga dunia mapema mwaka huu nchini Afrika Kusini akiwa na umri wa miaka 70.

“Marehemu alitambuliwa kutokana na ujaziri wake uwanjani, kiasi cha kubandikwa ‘Kadenge na Mpira’ na watangazaji wa mpira siku hizo, jina ambalo limebaki kwenye vichwa za watu wengi hata wale wasiofahamu chochote kuhusu kandanda,” alisema Nyawanga.

Jamii ya marehemi ilimshukuru Rais Uhuru Kenyatta ambaye licha ya kumtembelea alipokuwa akiugua, alimpa Sh2 milioni na bima ya matibabu pamoja na kadi ya NHIF.

Kadhalika, Raila alimiminiwa sifa kutokana na msaada wake wa kukipigia kitabu cha ‘Life of a Legend’ ambacho kiliandikwa na Mtangazaji wa BBC, John Nene.

Mwaka huu pekee, Kenya imepoteza wanamichezo maarufu wastaafu watatu Naftali Bon na Nyandika Maiyoro baada ya wito wao wa mara kwa mara wa kusaidiwa kuambulia patupu.

Kwa sasa, aliyekuwa mwanariadha hodari wa kimataifa, Robert Ouko aliyekuwa kwenye timu ya Kenya iliyotwaa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 4×400 katika Olimpiki za 1972 mjini Munich ni mgonjwa zaidi bila msaada wowote.

Mbali na Julius Sang’a aliyeaga dunia mnamo 2004, Charles Asati na Hezekiah Nyamao ndio pekee waliobakia kutoka kwa kikosi hicho cha 1972, lakini wanahangaika kutokana upweke, licha ya yote walioifanyia nchi hii.

Wakenya wengi wamebaki wakijiuliza inafanya nini sharia ya Majina wa Kenya ya 2014 ambayo ilibuniwa kwa ajili ya kushughulikia wanamichezo maarufu waliosaafu na waliopo sasa?

 

Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, atoa salamu za pole wakati wa ibada kanisani Friends Church (Quakers), Nairobi baada ya kifo cha mwanasoka Joe Kadenge. Picha/ Sila Kiplagat

Katika salamu zake za pole, Raila alimsifu marehemu Kadenge kama mtu aliyejitolea kuboresha vipaji vya vijana wengi nchini akiwa kocha na pia kama meneja wa klabu mbalimbali, na vilevile timu ya taifa.

Wetang’ula naye alisema viongozi wamekuwa wakiwamiminia sifa magwiji nchini pindi tu wanafariki, badala ya kufanya hivyo wakati wangali hai.

Mazishi ya nguli Kadenge yatagharimu Sh5 milioni ambazo wakati alikuwa akiugua hakupata zimfae.

Kadenge alianza kuugua kwa miaka kadhaa iliyopita, lakini ni wachache mno waliofanya juhudi za kumtembelea.

Kadenge amekuwa akipambana na ugonjwa tangu mwaka 2006, kabla ya kupata kiharusi na kuzidiwa mnamo 2016.

Ujasiri wa kufunga mabao

Kadenge alisifika kutokana na mbinu zake za kupepeta mpira na kufunga mabao kwa ujasiri mkubwa baada ya kuwala vyenga mabeki watajika nchini na mataifa ya kigani.

Kadenge alifahamika eneo la Afrika Mashariki kama mchezaji kandanda maarufu aliyewacha historia kubwa kutokana na mchango wake.

Alikuwa na talanta ambaye hakuchukua muda mrefu kujiunga na timu ya taifa miaka ya sabini.

Akiwa na umri wa miaka 20 tayari alikuwa amewavutia makocha mbalimbali.