Kimataifa

Gwiji wa ngwenje Jeff Bezos na mkewe kutalikiana

January 9th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na CHARLES WASONGA

CALIFORNIA, AMERIKA

MTU tajiri zaidi ulimwenguni Jeff Bezos na mkewe MacKenzie, wametangaza kuwa wanapanga kutalikiana baada ya kuishi kama mume na mke kwa miaka 25.

Kwenye taarifa ya pamoja walioituma kwa akaunti ya Twitter ya Bezos, wawili hao walisema wanahisi kuwa na bahati ya kupata na kushukuru kwa kila mwaka ambao waliweza kuishi pamoja.

“Baada ya muda mrefu wa majaribio ya mapenzi na kutengana, tumeamua kutalikiana na kuendelea na maisha kama marafiki wa kawaida tu,” wawili hao walisema.

“Na kama tulijua tungeachana baada ya miaka 25, tungelioana tena,” wakaongeza.

Bezos, 54 na MacKenzie, 48, walikutana na wakaoana wakifanya kazi katika Shirika la D.E Shaw, lenye makao yake makuu jijini New York, mapema miaka ya 1990s.

Baadaye walifunganya virago vyao na kusafiri hadi Seatle ambako Bezos alianzisha kampuni ya Amazon.

Wakati huu Bezos, ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Amazon, anaorodheshwa kama mtu tajiri zaidi ulimwenguni, akiwa na mali inayokadiriwa kuwa ni dola 137 bilioni (sawa na Sh1.3 7 trilioni), kulingana na orodha ya mabilionea katika wavuti ya Bloomberg

Hii ina maana kuwa talaka hii inaweza kuishi kuwa ya gharama kubwa zaidi katika maisha ya wawili hao.

MacKenzie ni mwandishi wa vitabu kadha vya riwaya, kikiwemo “Traps” na “The Testing of Luther Albright”.