GWIJI WA WIKI: Ali Salim M’Manga

GWIJI WA WIKI: Ali Salim M’Manga

Na CHRIS ADUNGO

WAZEE hawa wamestaafu na kuachia vijana usukani. Walikuwa na mvuto wa haiba na weledi wa hali ya juu katika utangazaji wa soka.

Wakianza kutangaza mpira, ilikuwa lazima usikilize hadi kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kipulizwe.

Mmoja wao ni Ali Salim M’Manga.

Upekee wake ni utajiri wa msamiati, ufundi wa kucheza na maneno na wepesi wa kutumia maneno kumchorea msikilizaji picha za akilini (taswira) kuhusu matukio ya uwanjani.

“Niamshe hata usiku wa manane na unipe maikrofoni! Nitakupangia kilichokuwa kikosi kizima cha Harambee Stars katika miaka ya themanini na ‘utazame’ mpira redioni!” anasema M’Manga ambaye ni shabiki mkubwa wa Real Madrid ya Uhispania.

Wengine waliobaki – ambao nawafahamu kutoka humu nchini – ni Leonard Mambo Mbotela, Jack Oyoo Sylvester, Salim Mohamed, Nick Okanga na James Abila.

M’manga alizaliwa katika kijiji cha Zibani, eneo la Ng’ombeni, Kaunti ya Kwale.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Msingi ya Ng’ombeni (1961-1967) na akasomea katika shule mbalimbali za upili kabla ya kujiunga na Allidina Visram High Mombasa alikofanyia KCE mnamo 1971.

Aliwahi kuuza sigara kabla ya kuwa mhasibu katika kampuni ya ulinzi ya Securicor, Mombasa.

Aliajiriwa na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) mnamo 1977 na akapata mafunzo ya uanahabari katika taasisi ya mawasiliano ya KIMC.

‘Sikio la Mkulima’, ‘Jifunze Kiswahili’, ‘Lugha Yetu’, ‘Maendeleo Wilayani’, ‘Karibu KBC’, ‘Wajue Wanamuziki’, ‘Ni Yupi Uliyemchagua’ na ‘Matatizo’ ni vipindi vya awali alivyokuwa akivitayarisha katika idhaa ya KBC.

Kwa sasa anaendesha vipindi ‘Ulimwengu wa Wanamuziki’ na ‘Michirizi ya Spoti’.

M’Manga pia amewahi kutangaza mpira kwa mkataba katika runinga ya kidijitali ya SuperSport.

Aliyemwamshia hamu ya kutangaza mpira ni Ahmed Kipozi wa Radio Tanzania Dar es Salaam.

Azma hiyo ilichochewa zaidi na Abila aliyekuwa mwanafunzi mwenzake Allidina Visram.

“Mtangazaji bora hufanya utafiti wa kina na huzamia mapema historia ya kipute husika na vikosi vinavyopambana na ahudhurie mechi nyingi ndipo atambue wachezaji uwanjani kwa urahisi,” anasema.

M’Manga alitangaza fainali za AFCON nchini Senegal (1992) na Tunisia (2004) kisha Kombe la Dunia nchini Ujerumani mnamo 2006.

Alitawazwa Mtangazaji Bora wa makala ya nne ya Michezo ya Bara la Afrika iliyofanyika Kenya 1987.

Amewahi kutangaza mechi za Cecafa, Kombe la Mashirikisho na Klabu Bingwa Afrika (CAF) nchini Uganda, Tanzania, Rwanda, Ethiopia, Misri, Liberia, Benin, Nigeria, Cameroon, Ivory Coast, Bukini, Guinea na Zambia.

M’Manga amejaliwa watoto watano – Maku, Bahati, Nuru, Salim na Mwanajuma ambaye pia ni mtangazaji.

You can share this post!

VALENTINE OBARA: Tujihadhari sana Pwani isigeuke kuwa Sodoma

KAULI YA MATUNDURA: Mapema mno kusherehekea mchakato wa...

T L