GWIJI WA WIKI: ALVINS KASUKU

GWIJI WA WIKI: ALVINS KASUKU

Na CHRIS ADUNGO?

MTIHANI mgumu ambao Alvins Fred Owiti Kasuku alilazimika kufanya baada ya Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) ni kuteua kozi ya kusomea katika chuo kikuu.

Ingawa alitamani sana kuwa wakili, alihiari kukumbatia ualimu licha ya kwamba kipaji cha uigizaji – kilichoanza kujikuza ndani yake tangu utotoni – kilikuwa tayari kimemteka.

Vita hivyo vya ndani ya nafsi vilifichua ukubwa wa mapenzi yake kwa Kiswahili na Kiingereza japo akiwa shuleni, uwezo wake ulidhihirika zaidi katika Hisabati na masomo ya Sayansi. Alishiriki pia michezo ya soka na riadha na akawakilisha shule yake katika tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Kasuku amejaliwa kipawa cha ulimi. Wepesi wa kutema maneno anayoyasuka kwa ufundi ndio upekee unaozidi kumpigisha hatua kubwa katika ulingo wa sanaa ya uigizaji.

Kipaji cha ulumbi na umilisi wa lugha ni siri inayomfanya kuwa mwigizaji wa kustahiwa huku kiwango cha juu cha ubunifu kikimpa fursa adhimu za kufyatulia kampuni na mashirika mbalimbali matangazo ya kibiashara.

“Wakati mwingine inamjuzu mtu kuchukua hatua zitakazochochea maono yake kuwa ndoto zenye thamani na mshabaha. Kufaulisha azma hiyo kunahitaji subira na ukakamavu,” anasema.

Kasuku alizaliwa mjini Kisumu. Alikulia na kulelewa katika kijiji cha Olando, Suba, Kaunti ya Homa Bay.

Alianza safari ya elimu katika shule za msingi za Nyamasaria na Central (Kisumu) kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Mbita, Homa Bay (2005-2008).

Baada ya KCSE, alifundisha katika Shule ya Upili ya Wiga, Homa Bay, kabla ya kujitosa kikamilifu katika ulingo wa uigizaji. Alijiunga na kikundi cha Rabala Theatre kilichomkuza kisanaa kabla ya kusomea ualimu (Hisabati na Kemia) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Kasuku anajivunia kuigiza vitabu vya fasihi vilivyowahi kutahiniwa katika shule za sekondari za humu nchini akiwa na makundi ya Kenyatta University Travelling Theatre (KUTT), Theatrix Arts na Jicho Four Productions.

Amewahi pia kufanya kazi na makundi ya Culture Spills, Heartstrings Entertainment na Festival of Creative Arts (FCA) yaliyompa majukwaa ya kushiriki zaidi ya michezo 120 katika kumbi mbalimbali.

Kabla ya kuigiza mhusika Nebuchadnezzar katika mchezo wa runingani ‘The Real Househelps of Kawangware’ (TRHK) mnamo 2019, Kasuku alikuwa chale (comedian) katika vipindi ‘Kenya Kona Comedy’ (KTN, 2012), ‘Comedy Arena’ (KBC, 2013) na ‘Churchill Show’ (NTV, 2014).

Amechangia pia kazi nyingi katika programu ya Viusasa na kipindi ‘Wicked Edition’ (NTV).

Kwa sasa anaigiza mhusika Ogola katika mchezo ‘Zora’ ambao hufyatuliwa na runinga moja ya humu nchini kila Jumatatu hadi Ijumaa. Aliyemhimiza kuichangamkia fursa hiyo ni rafiki na chale mwenzake, Byron Otieno almaarufu Owago Onyiro.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iunde sera wakongwe wafunze vijana...

Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Miathene...

T L