GWIJI WA WIKI: Annette Odusi

GWIJI WA WIKI: Annette Odusi

NA CHRIS ADUNGO

MATAMANIO ya Annette Odusi tangu utotoni yalikuwa kuwa mwimbaji maarufu wa nyimbo za mtindo wa kufokafoka.

Kipaji cha muziki kilianza kujikuza ndani yake katika umri mdogo na alikuwa na mazoea ya kuiga wasanii wazoefu huku akijirekodi kwenye kanda.

Hata hivyo, marafiki walimshawishi ajitose katika fani ya uigizaji mnamo 2009, miaka mitatu baada ya kukamilisha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) katika shule ya upili ya Coast Girls, Kaunti ya Mombasa.

Alijiunga na Shirika lisilo la Kiserikali la Solidarity with Women in Distress (SOLWODI) lililotumia kabumbu na michezo ya kuigiza kuhamasisha wanawake kuhusu masuala ya afya na kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia, dhuluma za kimapenzi na ukiukaji wa haki za binadamu.

Annette aliridhisha kwenye jaribio lake la kwanza katika ulingo wa filamu na hakupoteza dira wala kurudi nyuma kisanaa tangu wakati huo.

Aliongoza wenzake kufyatua filamu kadhaa zilizochezwa katika sehemu mbalimbali za Mombasa.

Zaidi ya ujasiri, kilichomtambisha kwa urahisi ni wepesi wa ulimi na utajiri wa ubunifu.

Alijiunga na Chuo cha Fairin jijini Mombasa kusomea masuala ya usimamizi wa sekta ya hoteli na utalii kwa udhamini wa SOLWODI kati ya 2009 na 2010.

Alidhihirisha pia sifa za uongozi bora na akateuliwa kuwa Miss SOLWODI – cheo kilichomfanya kuwa mwakilishi msimamizi mkuu wa kundi la wanasoka na waigizaji wa shirika hilo.

Annette alijikuza zaidi kisanaa kupitia Little Theatre Club Mombasa (2010-2011) kabla ya kuelekea Nairobi kujiunga na kundi la Jicho Four Productions lililompa fursa ya kuigiza vitabu vya fasihi vilivyokuwa vikitahiniwa katika shule za sekondari humu nchini.

Baada ya kushiriki mchezo mingi katika kumbi za Nairobi Theatre na Sarakasi Dome iliyoko Ngara, alinogesha filamu ya kwanza runingani mnamo 2013 akiigiza mhusika Fatuma katika ‘Saida’ (Citizen TV).

Milango yake ya heri ilijifungua tena mnamo 2018 na akashiriki ‘Maza’ (Maisha Magic East – DStv) akiigiza mhusika Matatizo. Kwa sasa anaigiza mhusika Zuu katika mchezo ‘Sultana’ (Citizen TV).

Mnamo 2018, alipokea mafunzo ya kuendesha vipindi na kuratibu matangazo ya biashara redioni kupitia idhaa ya Baraka 95.5 FM.

Kubwa zaidi katika malengo yake ni kupanua wigo wa ujasiriamali na kuwa miongoni mwa maprodyusa watakaofyatua filamu zitakazokubalika kimataifa.

Annette alizaliwa katika eneo la Budalangi, Kaunti ya Busia na akalelewa katika mtaa wa Mshomoroni, Kaunti ya Mombasa. Ndiye mwanambee katika familia ya Bw Fredrick Odusi na Bi Catherine Odusi. Amejaliwa mtoto Dwayne Gitonga.

Alisomea katika shule za msingi za Beans na Central Girls jijini Mombasa kabla ya kujiunga na Coast Girls (2003-2006).Kwa mtazamo wake, kufaulu katika uigizaji kunahitaji jitihada, subira na nidhamu ya hali ya juu.

“Hatua ya kwanza katika safari ya mafanikio ni kufahamu unachokitaka, kujielewa wewe ni nani, kutambua unakokwenda na kupiga hatua kusonga mbele kuelekea huko unakolenga kufika,” anatanguliza.

“Kipende unachokifanya na namna unavyokifanya. Yafanye mambo kadri ya uwezo wako. Yafanye kwa utaratibu unaofaa na kwa wakati unaostahili. Fanya hivyo ili ufike mbali,” anashauri.

  • Tags

You can share this post!

Mradi wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta wakwama Mukuru

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Ukikataa kubadilika ujue kuwa...

T L