GWIJI WA WIKI: Beatrice Gatonye

GWIJI WA WIKI: Beatrice Gatonye

Na CHRIS ADUNGO

KILA binadamu ana kipaji ambacho ni wajibu wake kukitambua na kutia azma ya kukipalilia. Nidhamu, bidii, uvumilivu na imani ni kati ya mambo muhimu yanayochangia mafanikio ya binadamu.

Jitume katika hicho unachokitenda na umtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga maishani. Fanya hiyo ili ufaulu!

Huwezi kabisa kujiendeleza kitaaluma iwapo utakosa maono. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta. Usilie wala kukata tamaa usipofaulu. Endelea kukazana na milango ya heri itajifungua yenyewe.

Huu ndio ushauri wa Bi Beatrice Gatonye – mpenzi kindakindaki wa Kiswahili, mlezi wa vipaji, mwanahabari shupavu na mwanamuziki chipukizi ambaye kwa sasa ni mtangazaji wa KBC Channel 1.

MAISHA YA AWALI

Beatrice alizaliwa katika eneo la Kaptagat, Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu. Ndiye mtoto wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto wanne wa Bi Jane Wanjiku – mke wa pili wa Bw Joseph Gatonye ambaye mkewe wa kwanza ni Bi Joyce Muthoni.

Beatrice alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Kipsinende, Kaptagat mnamo 1987. Huko ndiko alikosomea hadi mwishoni mwa 1998. Alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) na akajiunga na Shule ya Upili ya Naivasha Girls, Kaunti ya Nakuru mnamo 1999.

Baada ya kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2002, alijiunga na Chuo cha Eldoret Aviation alikosomea taaluma ya Habari na Mawasiliano hadi 2004.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo cha Habari Maalum mjini Arusha, Tanzania mnamo 2009. Alifuzu katika mwaka wa 2011 na akarejea Kenya kusomea shahada ya uanahabari katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kati ya 2013 na 2015.

MCHANGO KITAALUMA

Beatrice alipata nafasi ya kuwa mwanahabari wa kujitolea katika kituo cha Sauti Ya Rehema (SAYARE) mnamo 2003. Alihudumu huko kwa muda mfupi akiwa ripota wa runinga ya Sayare TV na mwendeshaji wa kipindi cha jioni cha ‘Evening Drive’ katika Idhaa ya Sayare FM.

Ilikuwa hadi 2008 aliporejea katika kituo hicho kilichomwajiri kuwa mtangazaji wa habari runingani na mwendeshaji wa vipindi vya asubuhi redioni. Kituo hicho ndicho kilidhamini masomo ya Beatrice nchini Tanzania.

Beatrice aliajiriwa na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) mnamo Januari 2012 kuwa ripota wa KBC Channel 1. Aliaminiwa fursa ya kusoma habari za ‘Darubini ya Channel 1’ baada ya miezi miwili pekee na akatawazwa Mtangazaji Bora wa Mwaka katika tuzo zilizotolewa na Baraza la Vyombo vya Habari Nchini Kenya (MCK) mnamo 2014.

Miongoni mwa wanahabari anaowapigia mhuri kutokana na ustadi wao wa kuipa taaluma hii uhai ni Salim Kikeke wa BBC na Jamila Mohamed wa Citizen TV.

KICHOCHEO

Beatrice alianza kuvutiwa na taaluma ya uanahabari katika umri mdogo. Anatambua ukubwa na upekee wa mchango wa baba yake mzazi katika ufanisi anaojivunia kwa sasa katika ulingo wa Kiswahili.

Baada ya kubaini utajiri wa kipaji cha mwana wao huyu katika utangazaji na uandishi wa kazi za kibunifu, wazazi wa Beatrice walimpa majukwaa mbalimbali ya kuikuza talanta yake.

Beatrice alikuwa mwepesi wa kujirekodi katika kanda za sauti na kujisikiliza redioni. Babake mzazi alipalilia kipawa kilichoanza kujikuza ndani ya mwanawe kwa kumnunulia nakala ya gazeti la ‘Taifa Leo’ kila siku.

Kati ya walimu waliomchochea Beatrice kukipenda Kiswahili akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni Bw Kariuki aliyemhimiza sana kusoma vitabu vya hadithi.

“Bw Kariuki alipanda ndani yangu mbegu zilizootesha utashi na kariha ya kukichapukia Kiswahili. Alinielekeza kwa idili na akaniamshia ari ya kuthamini masomo.”

Kariha na ilhamu zaidi ya Beatrice katika makuzi ya Kiswahili ilichangiwa na Bw Mbote – mwalimu aliyemtanguliza vyema katika somo la Fasihi na kumpokeza malezi bora ya kiakademia katika shule ya upili.

Chini ya ulezi wa Bw Mbote, Chama cha Kiswahili cha Naivasha Girls kilimpa Beatrice jukwaa maridhawa la kuinua kiwango chake cha umilisi wa lugha. Kilinoa makali yake ya ulumbi na kikachangia ujasiri wake wa kuzungumza mbele ya umma.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa sasa na Beatrice katika Kiswahili ni zao la yeye kufundishwa na wataalamu wabobevu na wapenzi kindakindaki wa lugha hii.

MAAZIMIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Beatrice ni kujikuza kitaaluma, kujifunza Lugha Ishara (KSL) na kuweka hai ndoto ya kuwa miongoni mwa wadau wakuu wa kutoa maamuzi muhimu katika tasnia ya uanahabari.

Anaazimia pia kuwa mmliki wa kituo cha habari kitakachokuwa na malengo mahsusi ya kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanahabari chipukizi watakaoangazia masuala mbalimbali yaliyo na umuhimu katika jamii.

Beatrice anapania kuwa kiini cha motisha itakayotawala wanataaluma wengi wa kike wanaoinukia na watakaoinukia katika ngazi na viwango tofauti vya uanahabari.

HUDUMA KWA JAMII

Beatrice anaendesha kampeni maalum ya kusambaza sodo kwa wanafunzi wa kike kutoka jamii zisizojiweza. Kampeni hiyo inalenga wasichana wa shule za msingi na upili pamoja na wanawake kutoka familia maskini nchini Kenya.

“Inasikitisha kwamba wapo wasichana wanaolazimika kutumia vipande vya magodoro, mablanketi, majani pamoja na karatasi ili kujistiri msimu wao wa hedhi unapowadia.”

Kupitia kampeni hiyo, Beatrice anakusudia kuhakikisha kuwa mahudhurio ya wanafunzi wa kike shuleni yanaongezeka hata zaidi.

MUZIKI

Beatrice ni mtunzi wa nyimbo za sifa kwa Mwenyezi Mungu. Kufikia sasa, amecharaza kibao ‘Huniongoza’ alichokirekodi mwaka huu wa 2021. Mbali na kipaji cha uimbaji, pia ana uwezo wa kucheza vyombo na ala mbalimbali za muziki.

JIVUNIO

Beatrice anajivunia wazazi wake waliojihini mengi, wakajitolea kumsomesha na kumzibia pengo la shaka maishani.

Anaistahi sana familia yake inayozidi kuiwekea kazi yake mshabaha na thamani licha ya panda-shuka za kila sampuli.

Beatrice ni mwanandoa na mama wa watoto watatu – Gideon Parselelo, Joshua Lesalon na Tiffany Chemutai. Yeye ni mama wa kambo wa watoto wawili – Ronald Kiprono na Patricia Cheptoo. Mumewe mpendwa ni Bw Zakayo Ng’etich.

You can share this post!

NGILA: Wanawake barani Afrika wachangamkie teknolojia

KINA CHA FIKRA: Kujiamini kama kiambata cha ufanisi maishani