GWIJI WA WIKI: Dennis Mwima

GWIJI WA WIKI: Dennis Mwima

Na CHRIS ADUNGO

MAISHA huisha. Kabla yaishe, yaishi yaishe. Usiishi kuisha.

Maisha ni safari ambayo mwisho wake ni siri kubwa isiyojulikana kwa binadamu!

Japo utajikwaa, kuteleza na mara nyingine kuanguka katika safari ya maisha, usiogope kitu! Jinyanyue upesi, futa vumbi, pangusa tope na utimke tena. Kuanguka ndiko kuinuka!

Nidhamu, bidii na uvumilivu huchangia pakubwa mafanikio ya mtu. Huwezi kabisa kujiendeleza maishani au kitaaluma iwapo hujiamini. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta!

Usitamauke unapokosa kufaulu. Mtangulize Mungu, endelea kukazana na hatimaye milango ya heri itajifungua yenyewe!

Huu ndio ushauri wa Bw Dennis Mwima almaarufu ‘Mwalimu wa Ulimwengu’ – mwandishi mzoefu wa vitabu ambaye kwa sasa anafundisha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Providence Academy, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Dennis alizaliwa na kulelewa katika eneo la Butere, Mumias, Kaunti ya Kakamega. Ndiye mwanambee katika familia ya Bw Washingtone Mwima na Bi Sarah Faluma.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Shinamwenyuli, Butere mnamo 1996. Ni katika shule hiyo ambapo hamu ya kutaka kuwa mwanahabari ilianza kujikuza ndani yake.

Mara si haba, alijipata akiiga sauti za wanahabari maarufu na akapendwa na watu kutokana na ‘sauti yake ya utangazaji’.

Baadhi ya wanahabari aliowaiga ni Jilani Wambura, Leonard Mambo Mbotela na marehemu Billy Omalla.

Kati ya walimu waliotambua utajiri wa kipaji cha Dennis katika utangazaji wa habari na kumpa majukwaa maridhawa ya kukuza na kupalilia talanta yake ni Bw Atita, Bi Susan Kageha na Bw Andrew Were Nyangweso waliomfundisha katika shule ya msingi.

Wengine waliopanda na kuotesha mbegu za utashi wa Kiswahili ndani yake ni Bi Stella Angufu na Bi Agnes Sungu waliotangamana naye kwa karibu sana katika Shule ya Upili ya Musanda, Butere.

Baada ya kufanya mtihani wa KCPE mnamo 2005 kisha KCSE mnamo 2009, Dennis alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Meru (2011-2012).

Alihiari kusomea ualimu baada ya ndoto yake ya kujiunga na chuo cha uanahabari kuyeyushwa na mawimbi ya ufukara yaliyotishia kumzimia mshumaa wa elimu. Hata hivyo, anaishi kwa imani kwamba mvuto wa kipekee uliomo ndani ya mrindimo wa sauti yake utakuja kuwa kitambulisho chake atakapokuwa mwanahabari katika siku za usoni.

UALIMU

Dennis alianza kufundisha mnamo 2013 baada ya kuajiriwa na Kakamega Hill School Junior. Akiwa huko, alikutana na walimu wazoefu wa Kiswahili – Zadock Amakoye na Bw Masika – waliomkuza pakubwa kitaaluma. Alihudumu huko hadi 2015 kabla ya kuhamia Ruai Junior Schools, Nairobi.

Kutua kwake jijini Nairobi kulikuwa mwanzo wa mkoko kualika maua. Alipata fursa za kuhudhuria makongamano mbalimbali ya Kiswahili, akapevuka zaidi kitaaluma na akawa mwalimu bora.

Kabla ya kuajiriwa na Shule ya Msingi ya Providence Academy Ruaraka mnamo Januari 2021, Dennis aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Msingi ya Anas Academy (Eastleigh), Clara Academy (Ruaraka) na Total Care Academy (Pangani).

UANDISHI

Dennis alikuwa mwepesi wa kuandika hadithi bunilizi za watoto alipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili. Insha nyingi alizozitunga chini ya uelekezi wa walimu wake zilimzolea sifa sufufu na kumfanya maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Kufikia sasa, ameandika kitabu cha kiada ‘Kichocheo cha Kiswahili KCPE’ kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Jalada la ‘Kichocheo cha Kiswahili’. Picha/ Chris Adungo

Ametunga pia hadithi fupi kadhaa ambazo zimejumuishwa katika diwani mbalimbali. Baadhi ya hadithi hizo ni ‘Kuku Mfanyabiashara’ katika mkusanyiko wa ‘Kasuku wa Salome na Hadithi Nyingine’, ‘Udongo wa Hekima’ katika ‘Mtoto wa Dhahabu na Hadithi Nyingine’ pamoja na ‘Ibilisi Mweupe’ katika ‘Kilele cha Mambo na Hadithi Nyingine’.

Dennis ameandika miswada mingi ya hadithi fupi na vitabu vya kiada kwa minajili ya Mtaala wa Umilisi (CBC). Nyingi za kazi hizo zipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu nchini Kenya.

‘Shauku ya Kuishi’ ni novela ambayo Dennis anaiandaa sasa kwa matarajio ya kuchapishwa hivi karibuni.

Miongoni mwa waandishi waliomshika mkono, kumpa motisha ya kujitosa ulingoni kikamilifu na kupiga mbizi katika bahari pana ya uandishi wa vitabu vya Kiswahili ni Ali Hassan Kauleni, Benard Simiyu Mkuyuni, Mathias Momanyi, Tom Nyambeka na Timothy Omusikoyo Sumba.

Wengine waliomshajiisha kukichangamkia Kiswahili kama kiwanda kikubwa cha ajira na maarifa ni Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, marehemu Profesa Ken Walibora, marehemu Sinjiri Mukuba na marehemu Eliud Shihanda Murono.

JIVUNIO

Dennis anaazimia kuvikwea vidato vya taaluma na kuwa miongoni mwa walimu na waandishi maarufu wa Kiswahili. Sawa na alivyoshikwa mkono hadi akafika alipo, naye anajitahidi kuwainua chipukizi katika sanaa ya uandishi.

Mbali na kufanya tafsiri na ukalimani, Dennis huendesha masimulizi na mijadala mingi ya kitaaluma kupitia kumbi mbalimbali za Kiswahili mitandaoni na YouTube (MwalimuTv).

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo sasa inatawala wanafunzi, wanahabari na walimu wengi ambao wametangamana naye katika makongamano anuwai ya kupigia chapuo Kiswahili.

Kwa pamoja na mkewe, Bi Violet Alividza, wamejaliwa watoto wawili – Mishie Nadia Neema na Zarina Zawadi Pendo.

CAPTION 2: Baadhi ya kazi za Mwalimu Dennis Mwima

You can share this post!

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika Shule ya...

NDIVYO SIVYO: Ukanushi wa kitenzi kishirikishi kipungufu...