Lugha, Fasihi na ElimuMakala

GWIJI WA WIKI: Deon Musau Muia

June 5th, 2019 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

MOLA alikupa karama ambayo aliwanyima wanadamu wote wengine. Wewe una umuhimu mkubwa duniani.

Usijilinganishe na mtu mwingine. Yalinganishe tu maendeleo yako na ulivyokuwa jana. Ukijilinganisha na wengine, bila shaka utapooza katika maisha na hatimaye utajiponza kwa masikitiko na majuto.

Majuto ni mjukuu. Jiamini. Unaweza. Waliofanikiwa ni watu kama wewe! Jitume sana katika mambo yakayokusaidia kusonga mbele kwa sababu ufanisi hauji vivi hivi.

Doyen wa Kiswahili Guru Ustadh Wallah Bin Wallah husema, “Siri ya kusonga mbele ni kuanza kusonga mbele.”

Usiwazie tu mustakabali mwema. Usijione tu ukiwa maarufu katika maisha yako yajayo na ukazembea kwa sababu wazazi wako wana mali na hela nyingi.

Cha muhimu ni kuyatekeleza mambo yatakayokusaidia kufikia kitembo cha ufanisi unachotaka.

Jiwekee gharadhi mpya kila baada ya kupiga hatua fulani. Hiyo ndiyo siri itakayokuwezesha kukua kila uchao.

Soma sana na uwaulize wajuao ili ujijenge kitaaluma. Kuuliza si ujinga, kutouliza na kutolitafitia jambo usilolijua ndio ujinga wa kiwango cha juu.

Kila mja ana upungufu na inamjuzu kuyauliza asiyoyajua ili kuupunguza upungufu huo.

Ipande mbegu ya ufanisi kila siku ya maisha yako na mavuno yatakuwa mazuri, makubwa na mengi ajabu. Kusema kweli, huwezi ukapanda mahindi kisha utarajie kuvuna kahawa! Mtu huvuna alichopanda. Ukipandana kupalilia vyema, bila shaka utapata tabasamu ya milele.

Ukitaka kufikia kilele cha mafanikio, basi nyenyekea, heshimu wanadamu wengine na mtumainie sana Mungu wako. Unyenyekevu ni mbolea katika mafanikio ya mtu. Usiwe mwenye majitapo na majigambo. Heri watu wakuone mjinga kwa sababu ya utuvu na unyenyekevu wako.

Huu ndio ushauri wa Bw Deon Musau Muia – mwandishi chipukizi, mtaalamu wa Sarufi na Isimujamii ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi na mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Mukaa Boys’, Makueni.

Maisha ya awali

Deon alizaliwa mnamo Agosti 8, 1993 kijijini Mang’elete katika Kaunti ya Makueni. Ni mtoto wa katikati kuzaliwa katika familia ya Bw James Muia Nganda na Bi Ann Mutee. Alisomea katika shule tatu tofauti za msingi kwa sababu ya uhamisho wa kikazi wa baba yake.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Mang’elete kati ya 2000 na 2005. Mnamo 2006, alijiunga na Shule ya Msingi ya Mtito-Andei. Baadaye, alijiunga na Shule ya Msingi ya Emali mnamo 2007.

Msukumo wa kukipenda Kiswahili ulizidishwa na vitabu

‘Kiswahili Mufti’ ambavyo vimeandikwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah.

Vitabu hivyo vilimpa mwamko wa kipekee kutokana na ubora wavyo. Kwa hakika, vitabu hivyo vilichangia zaidi ya asilimia 80 katika jumla ya alama 96% alizopata katika mtihani wa KCPE Kiswahili. Ni katika Shule ya Msingi ya Emali alikofanyia mtihani wake wa KCPE mnamo 2007.

Baadaye alijiunga na Shule ya Upili ya Mukaa Boys’ katika jimbo la Makueni mnamo 2008. Ni wakati akiwa Mukaa Boys’ ndipo alipoboresha kiwango chake cha umilisi wa Kiswahili baada ya kuhimizwa pakubwa na walimu wake.

Bw Kaula alimfaa sana kwa nasaha zake aula. Aidha,

ndiye aliyeidhinisha ombi la Deon la kuanzisha Jopo la Kiswahili (kwa sasa ni Chama cha

Kiswahili shuleni Mukaa Boys’). Idhini hiyo ilimpa nafasi ya kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Jopo la Kiswahili.

“Bw Kaula alinichochea pakubwa kukichapukia Kiswahili. Alipanda ndani yangu mbegu zilizootesha utashi na kariha ya kuichangamkia lugha hii. Alijitolea kunielekeza kwa ari na idili.”

Nasaha za Mwalimu Mkuu, Bw Francis Mutua zilimpa Deon mtazamo chanya katika kuyachambua maisha na kukabiliana vilivyo na changamoto za mara kwa mara.

Kuna kauli ya Bw Mutua anayoikumbuka sana hadi leo. Kwamba, “Failure is a situation, never a person. Notice the difference between what happens when a man says to himself that he failed three times and what happens when he says he is a failure.”

Maneno hayo yalimkosha kwelikweli. Yalimfumbua macho kabisa na kumfanya kujitambua.

Deon anatambua pia ukubwa na upekee wa mchango wa Bw Kau (Naibu wa Mwalimu Mkuu shuleni Mukaa Boys’) aliyempokeza malezi bora zaidi ya kiakademia.

Msemo wake wa mara kwa mara kwamba, “ivitukaniaa kitindioni” uliamsha ari na hamu ya Deon kujizatiti vilivyo kutimiza nyingi za ndoto zake. Kauli ya Bw Kau ina maana kwamba wanafunzi wanapoenda shuleni huwa ni wengi na wanafungiwa katika zizi moja (shule).

Wanapoendesha shughuli zao shuleni, kuna wale wanaofanikiwa na kunao pia wanaokosa kufanikiwa kulingana na namna wanavyoutumia muda wao.

Uongozi katika Jopo la Kiswahili ulimpa Deon jukwaa mwafaka la kuitafitia lugha ashirafu ya Kiswahili. Usikivu, umakini na heshima ya wanafunzi wenzake vilimshajiisha sana na kumpa mihemko chanya ya ufanisi.

Usomi na utaalamu

Deon alijiunga na Chuo Kikuu cha Egerton (Bewa Kuu) mnamo Septemba 2012. Alipania kufanya Shahada ya Isimu katika Kiswahili na Kiingereza lakini akaarifiwa kwamba haiwezekani humu nchini.

Alishauriwa aende Ujerumani kunakofundishwa kozi hiyo. Alipewa michepuo kadhaa ya masomo achague anaotaka. Kwa sababu ya utashi wake wa kusomea Kiswahili aliishia kufanya Shahada ya Ualimu, mchepuo wa Kiswahili na Dini.

Akiwa chuoni, alijiunga na Chama cha Kiswahili cha Egerton (CHAKIE). Mnamo 2013, aliingia katika uongozi wa CHAKIE akiwa Katibu. Baada ya kuwa katika uongozi

kwa mwaka mmoja, alipendekeza kuundwa kwa vitengo mbalimbali vya CHAKIE: Kitengo cha Sarufi, Kitengo cha Fasihi, Kitengo cha Tafsiri na Ukalimani na Kitengo cha Sanaa na Uigizaji. Pendekezo hilo liliungwa mkono na takribani viongozi wote wa chama.

Kuanzia 2014, aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitengo cha Sarufi pamoja na kile cha Tafsiri na Ukalimani. Mwanzoni mwa 2015, aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA – Ukanda wa Kenya). Wadhifa huu wa kitaifa ulimpa hamasa ya kuyazamia zaidi masuala ya Kiswahili.

Deon amehudhuria makongamano mengi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi hii. Mnamo 2013, alihudhuria na kushiriki kikamilifu Kongamano la Kimataifa la CHAWAKAMA katika Taasisi ya Elimu jijini Kigali, Rwanda.

Mnamo 2016, alihudhuria Kongamano la Kimataifa la CHAWAKAMA katika Chuo cha Kitaifa cha Zanzibar (SUZA).

Mnamo Mei 6, 2017, alimwalika Profesa Ken Walibora katika Shule ya Upili ya Mukaa Boys.’ Wanafunzi walinufaishwa sana na hotuba yake. Isitoshe, amewatangamanisha wanafunzi wake na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah mara nyingi. Nasaha za Guru Ustadh ambaye ni mwalimu wa walimu na mwandishi maarufu barani Afrika, zinawahimiza wanafunzi wengi kwa sasa kujikaza kisabuni katika masomo yao.

Baada ya kufuzu na kuhitimu kuwa mwalimu mnamo 2016, Deon alianza kufundisha Kiswahili na somo la Dini katika Shule ya Upili ya Mukaa Boys’ alikosomea.

Kwa sasa ndiye Mlezi wa chama cha Kiswahili cha Mukaa Boys’ (CHAKIMU). Isitoshe, ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Uandishi

Deon ni mwandishi chipukizi wa kazi za Kiswahili. Ndoto yake ya uandishi ilichipuza alipokuwa mwanafunzi wa shule ya upili.

Mara si chache, aliwahi kushiriki mashindano mbalimbali ya uandishi akiwa katika shuleni na kuwapiku wenzake. Jambo hili likawa kiini cha msukumo wake wa kujitosa katika ulingo wa uandishi wa vitabu.

Kwa sasa anaandika vitabu vya Kiswahili kwa minajili ya mtaala mpya wa 2-6-6-3. Vitabu hivyo vitachapishwa na kampuni ya Spearsharp Educational Publishers hivi karibuni.

Pia ana miswada ya kazi mbili: (a) Usaili Sahili wa Ushairi na (b) Isimujamii ambazo anaamini zitachapishwa kufikia mwisho wa mwaka huu. Ana imani kwamba nakala hizi zikichapishwa, zitawafaidi wasomi wa Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki.