GWIJI WA WIKI: Dkt Alexander Rotich

GWIJI WA WIKI: Dkt Alexander Rotich

Na CHRIS ADUNGO

USHIKWAPO shikamana na ukiitwa itika.

Usiposhikamana unaposhikwa, anayekushika mkono atachoka na atakuachilia.

Mwishowe utapotea njia, utaanguka na kujuta!

Usipoitika unapoitwa, anayekuita atatamauka na atakupuuza kabisa utakapomhitaji asikie kilio chako ili akuauni!

Kuwa na malengo maishani na uziwanie fursa adimu utakazozipata za kukupigisha hatua kitaaluma. Wapuuze wasiokutakia mazuri, kuwa mtu mwenye msimamo na ushindane na wakati badala ya binadamu wenzako!

Amini kwamba hakuna kisichowezekana, jitume katika safari ya kufanikisha maazimio yako na umtangulize Mungu katika kila jambo!

Huu ndio ushauri wa Dkt Alexander Kipkemoi Rotich – mwalimu mzoefu, mlezi wa vipaji na Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kabianga.

Maisha ya Awali

Rotich alizaliwa mnamo Septemba 9, 1965 katika kata ya Kimuchul, eneo la Chemaner, Kaunti ya Bomet. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto 18 wa Mzee Jonhstone Kiprotich Tuwei na wake zake wawili – Bi Rebecca Chebet na Bi Zipporah Tuwei.

Rotich alianza safari ya masomo katika Shule ya Msingi ya Kimuchul mnamo 1972. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) mwishoni mwa 1979.

Alifaulu vyema na kupata nafasi katika Shule ya Upili ya Christ The King, Kaunti ya Nakuru alikosomea kati ya 1980 na 1981 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Tengecha, eneo la Kapkatet, Kaunti ya Kericho mnamo 1982.

Kati ya masomo yote aliyoyafanya Rotich katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCE) mnamo 1983, Kiswahili ndicho kiliongoza. Ingawa alipata nafasi katika Shule ya Upili ya Kabianga kwa minajili ya kiwango cha A-Levels, alihiari kusomea katika Shule ya Upili ya Tengecha kati ya 1984 na 1985.

Anakiri kuwa ilhamu yake ya kukichapukia Kiswahili ilichangiwa na baadhi ya wanafunzi waliomtangulia kimasomo katika Shule ya Upili ya Tengecha, akiwemo Prof John Habwe – mwandishi maarufu wa Isimu na Fasihi ya Kiswahili ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Ualimu

Rotich alijitosa katika ulingo wa ualimu baada ya kukamilisha Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Sita (KACE). Alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Upili ya Chemaner mnamo 1986 kabla ya kuhamia katika Shule ya Upili ya Merigi, Bomet alikohudumu kati ya 1987 na 1988.

Ilikuwa hadi Mei 1989 ambapo alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Kisii. Alifuzu katika mwaka wa 1991 na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ikamtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya St Michael’s Bomet.

Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kabla ya kupata uhamisho hadi Shule ya Upili ya Mulot, Bomet (1993-1996) kisha Shule ya Upili ya Chemaner (1996-1997).

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa Rotich msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kusomea shahada ya kwanza katika ualimu (Kiswahili na Dini) kati ya 1998 na 2001.

Baada ya kuhitimu, TSC ilimtuma katika Shule ya Upili ya Kapsimbiri, Bomet. Alifundisha huko hadi 2005 kabla ya kurejea katika Chuo Kikuu cha Moi kusomea shahada ya uzamili huku akifundisha katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Mosoriot, Kaunti ya Nandi.

Alifuzu katika mwaka wa 2009 baada ya kuwasilisha Tasnifu ‘Nyimbo za Watoto wa Shule za Chekechea na za Msingi katika Manispaa ya Bomet: Uchunguzi wa Kiuamilifu’ chini ya uelekezi wa Prof Issa Yusuf Mwamzandi na marehemu Dkt Hannington Oriedo.

Rotich amewahi pia kufundisha katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Kericho (2008-2013). Akiwa huko, alikuwa pia mhadhiri wa muda katika Chuo Kikuu cha Moi, Bewa la Kericho.

Alianza kusomea shahada ya uzamifu (phD) katika Chuo Kikuu cha Moi mnamo 2010 na akaajiriwa na Chuo Kikuu cha Kabianga miaka mitatu baadaye.

Alifuzu mnamo 2018 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Simulizi za Unyanyapaa Unaohusiana na Virusi vya Ukimwi katika Nyimbo za Kenya baada ya Usasa”. Wasimamizi wake walikuwa Prof Mwamzandi na Dkt Mark Mosol Kandagor aliyechukuwa nafasi ya marehemu Prof Naomi Luchera Shitemi aliyeaga dunia mnamo 2013.

Rotich alipanda daraja kuwa Mhadhiri mnamo 2019 na kwa sasa analenga kukwea ngazi za elimu na kuwa Mhadhiri Mwandamizi na kuweka hai matumaini ya kuwa Profesa wa Kiswahili.

Uandishi

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Rotich akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Insha nyingi alizoziandika wakati huo zilimvunia tuzo za haiba kutoka kwa walimu wake.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi ya kizalendo yaliyofana katika mashindano ya viwango na ngazi mbalimbali na kumpa fursa ya kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Kufikia sasa, Dkt Rotich anajivunia kuandika na kuchapishiwa makala kadhaa ya kitaaluma katika sura za vitabu na majarida mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Ameshiriki pia uandishi wa kitabu cha Gredi ya Tano katika lugha za Kikalenjin kwa minajili ya Mtaala Mpya wa Umilisi (CBC).

Uanachama

Dkt Rotich ni mwanachama kindakindaki wa Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU). Vyama hivi vimempa majukwaa mwafaka ya kusambaza maarifa, kuendeleza msingi imara wa lugha na kutoa mchango mkubwa katika uandishi, utafiti, ufundishaji na matumizi ya Kiswahili.

Tangu 2017, Dkt Rotich amekuwa Afisa wa Mahusiano Bora wa CHAKAMA–Kenya na yuko mstari wa mbele kuwalea wanachama wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kabianga (CHAKIKA) kwa ushirikiano na Dkt Mohamed Ramadhan Karama, Dkt Emmanuel Simiyu Kisurulia na Prof Mwamzandi.

Katika mengi ya makongamano ya CHAKIKA na Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA), Dkt Rotich amekuwa akitoa ushauri wa kitaaluma kwa wanafunzi na kuwahimiza walimu wenzake kuchochea kasi ya malengo mahususi ya kukuza Kiswahili katika nyanja za ufundishaji, utafiti na uandishi.

Huduma kwa jamii

Dkt Rotich ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Usimamizi wa mojawapo ya shule katika Kaunti ya Bomet na ni mwanachama wa Bodi ya Usimamizi katika shule moja katika kaunti hiyo.

Uzoefu ambao Dkt Rotich anajivunia katika ufundishaji umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kupigia chapuo Kiswahili, kuhamasisha walimu na kuwaelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka za kujikuza kitaaluma.

Jivunio

Dkt Rotich anaistahi familia yake inayozidi kuiwekea kazi yake mshabaha. Kwa pamoja na mkewe Bi Rachael Rotich, wamejaliwa watoto watatu – Winnie Chepkorir, 30, Harriet Chepng’eno, 24 na Collins Kiplang’at, 17.

Dkt Rotich anajivunia wazazi wake waliojihini mengi na wakajitolea kumsomesha licha ya panda-shuka za kila sampuli. Anatambua pia upekee wa mchango wa walimu wake wa awali ambao walimpokeza malezi bora ya kiakademia, kumzibia pengo la shaka na kumchochea pakubwa kitaaluma baada ya kutambua uwezo wake katika Kiswahili.

Hawa ni pamoja na Bw William Sanga, Bw Samuel Kirui, Bw Japhet Chirchir, Bw Gwachi Mayaka, Prof Clara Momanyi na marehemu Clement Busolo. Wengine ni Dkt Allan Lennox Opijah, Prof Nathan Oyori Ogechi na marehemu Davies Muthondu Mukuria.

Dkt Rotich anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wanataaluma wengi ambao amewafundisha katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

You can share this post!

TAHARIRI: Tuhimize maadili kwa watoto wetu

WASONGA: Ruto, Raila wasaidie kutatua shida za Kenya si...