GWIJI WA WIKI: Dkt Beverlyne Asiko Ambuyo

GWIJI WA WIKI: Dkt Beverlyne Asiko Ambuyo

Na CHRIS ADUNGO

MAISHA ni safari. Kila hatua ya maisha ya mtu ni muhimu katika kuchangia kuwepo kwake.

Unapozaliwa, unaanza kuandaa makala kukuhusu. Kila unalolitenda – jema au baya – hujenga au kubomoa utu wako.

Lazima tutie bidii na kumakinikia yale tunayokusudia kufanya. Mengine ni ya matokeo ya haraka na mengine yanahitaji utulivu na uvumilivu ili kuyapata.

Ni muhimu kujitia moyo na kujishabikia katika shughuli zako ili uwe na hamu kubwa si tu ya kutaka kuendelea, bali pia ya kukamilisha mradi wowote unaouanza kwa njia bora na yenye ufanisi mkubwa.

Msingi muhimu zaidi katika kila hali ni kumtanguliza Mungu. Yeye ndiye hutukirimia neema na nguvu ya kutuwezesha kufikiria na hata kutekeleza shughuli zetu zote; ziwe kubwa au ndogo. Tuwe wema kwa watu wote tunaotangamana nao nyakati zote.

Huu ndio ushauri wa Dkt Beverlyne Asiko Ambuyo – mwandishi na msomi wa Isimu na Fasihi ya Kiswahili ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maseno.

MAISHA YA AWALI

Asiko alizaliwa mnamo Februari 23, 1979 katika kijiji cha Ikumba, Maragoli ya Kati, Kaunti ya Vihiga. Alilelewa katika familia ya Bi Phanice Nyamanga Liko na marehemu Mzee Sospeter Liko Agufana.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Ikumba kati ya 1983 na 1991 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Butere Girls, Kaunti ya Kakamega. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwishoni mwa 1995.

Alifaulu vyema na kupata fursa ya kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Jiografia) katika Chuo Kikuu cha Maseno kati ya 1997 na 2001.

UALIMU

Baada ya kuhitimu ualimu, Asiko alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Upili ya Kegoye, Kaunti ya Vihiga. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya Gahumbwa, Vihiga alikoamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi.

Aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Upili ya Manor House (2003, Trans Nzoia), Shule ya Upili ya Usenge (2004-2005, Siaya) na Shule ya Upili ya Thurdibuoro (2005, Kisumu).

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri Asiko mnamo 2006 na kumtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya Mahaya, Kaunti ya Siaya. Alihudumu huko hadi mwaka wa 2009.

Asiko alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa minajili ya kusomea shahada ya uzamili mnamo 2005. Alifuzu mnamo 2007 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Uamilishi Dhima wa Nomino katika Sentensi ya Luloogoli” chini ya usimamizi wa Dkt Alice Mwihaki na Dkt Mathooko Mbatha.

Alirejea kufundisha katika Shule ya Upili ya Mahaya kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Maseno kwa shahada ya uzamifu (PhD) mnamo 2008. Alifuzu mnamo 2013 baada ya kuwasilisha Tasnifu “Uchanganuzi wa Upole katika Majadiliano ya Bunge la Kenya” chini ya uelekezi wa Prof Florence Indede na Dkt Peter Karanja.

Asiko alifundisha katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino Cha Tanzania, Bewa la Mwanza, kati ya 2009 na 2010 kabla ya kuajiriwa na Chuo Kikuu cha Maseno kuwa Mhadhiri Msaidizi. Alipanda ngazi kuwa mhadhiri mnamo 2013.

Mnamo 2016, Dkt Asiko alihudhuria Kongamano la Kimataifa la Utafiti wa kithamano katika Chuo Kikuu cha Illinois, Chicago, Amerika.

Akiwa huko, Dkt Asiko alikutana na wasomi wenzake waliokuwa wakitafitia jinsi ambavyo vyombo vya mawasiliano kama vile simu, redio na runinga vinaathiri tabia ya walemavu wa akili na watoto wanaougua usonji (autism).

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Asiko tangu utotoni. Idadi kubwa ya wahadhiri waliomfundisha walimpigia mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na wakamtia motisha ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili.

Miongoni mwa mikota hao wa lugha waliompokeza malezi bora ya kiakademia ni Prof Kenneth Inyani Simala na Dkt Mwihaki.

Kufikia sasa, Dkt Asiko amechapishiwa makala ya kitaaluma katika sura za vitabu majarida mbalimbali ya kitaifa na ya kimataifa yakiwemo ‘East African Journal of Kiswahili Studies’, ‘Journal of Maseno University’ na ‘Kioo cha Lugha’.

Ametunga hadithi fupi kadhaa ambazo zimejumuishwa katika mikusanyiko mbalimbali na amechangia pia mashairi katika diwani za ‘Wosia na Mashairi Mengine’ na ‘Wasifu wa Timothy Omusikoyo Sumba’ zilizotolewa na African Ink Publishers mnamo 2021.

Mbali na tamthilia ya ‘Mwenye Macho’ ambayo kwa sasa iko katika hatua za mwisho mwisho za uhariri katika kampuni moja ya uchapishaji wa vitabu humu nchini, Dkt Asiko ana mswada wa kitabu cha ‘Mazoezi na Marudio ya Gredi ya Sita’ na hadithi za watoto anazotazamia kufyatua hivi karibuni.

UANACHAMA

Dkt Asiko ni mwanachama kindakindaki anayeshiriki kikamilifu katika shughuli za Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA).

Aliwahi kuwa mlezi wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maseno (CHAKIMA) chini ya mwavuli wa Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) kati ya 2013 na 2016.

Mbali na kuwa mwenyekiti wa masomo ya uzamili na uzamifu katika Chuo Kikuu cha Maseno, Dkt Asiko pia ni mmojawapo wa wadhamini katika Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Malipo ya Uzeeni katika Chuo Kikuu cha Maseno.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Dkt Asiko ni kuweka hai ndoto ya kuwa profesa na mwandishi mashuhuri wa Isimu na Fasihi ya Kiswahili.

Kwa imani kuwa mfuko mmoja haujazi meza, Dkt Asiko anashughulikia mradi mbadala wa ufugaji wa kuku nyakati za mapumziko.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wanataaluma wengi ambao wametangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Dkt Asiko anaistahi sana familia yake inayozidi kumzibia pengo la shaka na kuiwekea taaluma yake mshabaha na thamani. Yeye ni mwanandoa na mama wa watoto watano – Ibrahim, Timothy, Christine, Phanice na Philip. Pia ni mama wa kambo wa watoto wanne – Rose, Valentine, Stephanie na Cornel. Mumewe mpendwa ni Bw Cornel Adede.

You can share this post!

NGILA: Teknolojia itumike kukabili uchafuzi wa mazingira

NASAHA: Matokeo ya KCPE yanampa mzazi na mwana fursa...