GWIJI WA WIKI: Dkt Deborah Nanyama Amukowa

GWIJI WA WIKI: Dkt Deborah Nanyama Amukowa

Na CHRIS ADUNGO

KUNA mwimbaji aliyeimba kuwa: “Maisha ni foleni sisi sote tumejipanga mbele zake Mungu… Kila siku tunasongea polepole. Mwamini Mungu, ipo siku utafanikiwa”.

Hivyo, kufua dafu katika jambo lolote maishani hutegemea jinsi mtu binafsi anavyohusiana na Muumba wake. Mtumainie katika hali zote na mtangulize katika kila hatua. Waswahili husema, kunga za ngoma ya mahepe hufahamika na wanaohusika tu!

Changamoto nyingi za maisha zinaweza kukabiliwa na kila mtu kulingana na uwezo na tajriba aliyo nayo. Jitume katika hicho unachokifanya kwa sababu bahati ni chudi.

Huo ndio ushauri wa Dkt Deborah Nanyama Amukowa ambaye kwa sasa ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maseno.

MAISHA YA AWALI

Deborah alizaliwa katika familia ya Kikristo kijijni Misemwa, eneo la Webuye Mashariki, Kaunti ya Bungoma. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto sita wa marehemu Bi Susan Lumonya Nyukuri na marehemu Bw Wycliffe Wamalwa Cherwenyi waliokuwa walimu katika uzima na uhai wao. Ama kweli, mwana wa mhunzi asiposana huvukuta.

Deborah ilianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Misemwa kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Nakalira alikohamia mama yake mzazi kikazi.

Kati ya 1982–1985, aliendeleza masomo yake ya kiwango cha ‘O-Levels’ katika Shule ya Upili ya Mudavadi – Madzuu Girls. Alihitimu na kujiunga na Shule ya Upili ya Tumutumu Girls (1986–1987).

Deborah alisomea Shahada ya Sanaa (BA) katika tahasusi ya Kiswahili, Historia na Sosholojia katika Chuo Kikuu cha Egerton (Bewa la Njoro) kati ya 1988–1991.

Miongoni mwa wahadhiri waliomtandikia zulia la Kiswahili na kumkuza vilivyo kiakademia ni Profesa Chacha Nyaigotti-Chacha, marehemu Dkt Karisa Beja na marehemu Jay Kitsao.

Deborah alisomea kozi ya stashahada; yaani Diploma ya kuhitimu katika elimu (PGDE) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kati ya Disemba 1996 na Agosti 1997.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Maseno kusomea shahada ya uzamili mnamo 2003 na akafuzu 2005 baada ya kuwasilisha tasnifu “Taswira ya Mtoto wa Kike katika Riwaya ya Kiswahili” chini ya uelekezi wa Profesa Kenneth Inyani Simala na Profesa Wangari Mwai.

Alijisajili kwa minajili ya shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Maseno mnamo 2009 na akafuzu 2013 baada ya kuwasilisha tasnifu “Changamoto za Ujana katika Riwaya za John Habwe” chini ya usimamizi na uelekezi wa Profesa Wangari Mwai na Profesa Florence Indede.

UALIMU

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma Deborah kufundisha katika Shule ya Upili ya Chianda Boys, Bondo mnamo 1992. Alihudumu huko hadi mwaka wa 2002 alipopata likizo ya kusomea uzamili 2003–2005.

Alifundisha baadaye katika Shule ya Upili ya Lirembe Girls Ikolomani, Kakamega kati ya Januari na Desemba 2005 kabla ya kuhamia katika Shule ya Upili ya Shieywe mjini Kakamega. Alihudumu huko kati ya Januari na Novemba 2006 kabla ya kuajiriwa na Chuo Kikuu cha Maseno.

UANDISHI

Tangu utotoni, Deborah alikuwa na hamu ya kuchangia makuzi ya Kiswahili kupitia sanaa ya uandishi. Hata hivyo, tatizo kubwa lilikuwa kutojua pa kuanzia, nani wa kumshika mkono na wapi pa kuelekeza kazi zake kwa ajili ya kuchapishwa.

Kati ya watu waliomchochea kujitosa katika ulingo wa uandishi ni walimu wake wa awali waliotia azma ya kupalilia kipaji chake cha utunzi wa kazi bunilizi baada ya kutambua upekee na ukubwa wa uwezo wake katika Kiswahili.

Mwingine aliyemwamshia ari ya kuandika bila kukoma ni Bw Timothy Omusikoyo Sumba anayezidi kumhimiza kuogelea katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili.

Kufikia sasa, Dkt Deborah amechapisha makala kadhaa katika majarida ya kitaaluma ya kitaifa na kimataifa. Aidha, ametunga pia hadithi fupi kadhaa ambazo zimejumuishwa katika antholojia mbalimbali.

‘Mwanzo Mpya’ ni hadithi yake nyingine ambayo iko katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika shirika moja la uchapishaji wa vitabu nchini Kenya.

Dkt Deborah amechangia pia utunzi wa kitabu ‘Uandishi na Uhariri: Mbinu na Nadharia’ kwa kushirikiana na wataalamu wengine – Dkt Beverlyne Asiko Ambuyo, Dkt Jackline Njeri Murimi, Dkt Hamisi Babusa, Dkt David Turuthi, Dkt Wanjohi Githinji, Dkt Evans Makhulo, Bw Henry Indindi, Prof Clara Momanyi na Bw Sumba aliyekuwa msimamizi wa mradi huo.

UANACHAMA

Deborah ni mwanachama wa vyama mbalimbali vya kitaaluma, vikiwemo Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA), Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU). Yeye kwa sasa ndiye Naibu wa Katibu Mkuu wa CHAKITA.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Dkt Deborah ni kuweka hai ndoto ya kuwa profesa na mwandishi mashuhuri wa Kiswahili.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wanataaluma wengi ambao wametangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Baadhi yao ni Dkt Fridah Miruka (Chuo Kikuu cha Masinde Muliro), Alice Atemo (Shule ya Upili ya Shieywe), Samuel Sinzore, Edwin Atukunda na Martin Mulei. Miongoni mwa wanafunzi wake wa shahada ya uzamili kwa sasa ni Bi Aidah Mutenyo ambaye ni mtaalamu wa Kiswahili nchini Uganda.

Dkt Deborah anajivunia kuwa mwalimu wa lugha. Anaamini kwamba lugha hutawala maisha ya binadamu na ndicho chombo aula cha kumfinyanga, kuelezea fikra zake, kuendeleza mahusiano na kuhifadhi pamoja na kupitisha utamaduni wa jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Kwa pamoja na mumewe Michael Amukowa Ochiel, wamejaliwa watoto wanne: Marvin Justo Ochiel, Murray Oburah, Alverah Lumonya na Shiphrah Nyangasi. Pia wanawalea Melody Nanjala na Elkanah Nyongesa.

You can share this post!

Wabunge wa Wiper watishia kutema Kalonzo

Italia wakomoa Lithuania na kuweka rekodi ya kutopigwa...