Makala

GWIJI WA WIKI: Dkt James Ontieri

December 2nd, 2020 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

KUFAULU katika jambo lolote ni zao la jitihada, nidhamu, imani na stahamala.

Siri ya kuwa mwalimu bora ni kutawaliwa na upendo wa dhati kwa taaluma, kuchangamkia masuala yanayohusiana na mtaala na kuwa mwepesi wa kubuni mbinu mbalimbali za ufundishaji.

Hakuna mafanikio utakayoyapata bila ya kujituma. Shindana na wakati, jiwekee malengo mapya ya mara kwa mara na uzoee kuangusha jasho ndipo upate.

Hatua ya kwanza katika safari yoyote ya mafanikio ni kufahamu kile unachokitaka, kujielewa wewe ni nani na kutambua mahali unakokwenda. Jiamini, jikubali na ukatae maisha ya kujihukumu.

Mtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga na uwe na moyo wa kushirikiana na watu wengine katika mambo unayoyafanya.

Huu ndio ushauri wa Dkt James Ontieri – msomi wa isimu, mhariri shupavu, mtafiti stadi, mwandishi mahiri, mwanataalamu msifika na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Rongo, Kaunti ya Migori.

MAISHA YA AWALI

Ontieri alizaliwa mnamo 1970 katika kijiji cha Nyabiosi, eneo la Keumbu, Kaunti ya Kisii. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto kumi na mmoja wa Bw Benedicto Omari na Bi Hellen Nyang’ara.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Nyabiosi mnamo 1976. Alisomea huko hadi 1978 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Kamwaura, eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru mnamo 1979. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Saba (CPE) mwishoni mwa 1982.

Alifaulu vyema katika mtihani huo na akapata nafasi ya kusomea katika Shule ya Upili ya Mong’oni, Kaunti ya Nyamira kati ya 1983 na 1986. Alijiunga baadaye na Shule ya Upili ya Nyambaria, Kaunti ya Nyamira kwa minajili ya masomo ya kiwango cha ‘A-Levels’ mnamo 1987 na akafanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Sita (KACE) katika mwaka wa 1988.

Mnamo 1989, Ontieri alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Historia). Alihitimu mwishoni mwa 1992.

Miongoni mwa wahadhiri waliompokeza malezi bora ya kiakademia na kumtandikia zulia zuri la kukichangamkia Kiswahili ni Dkt Allan Lennox Opijah, Profesa Said A. Mohamed, marehemu Davies Muthondu Mukuria, marehemu Dkt Hannington Oriedo, marehemu Prof Abel Gregory Gibbe na marehemu Ibrahim Ngonzi.

Wengine waliomchochea pakubwa kwa imani kwamba Kiswahili ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi ni Prof Isaac Ipara Odeo, Prof Miriam Mwita na Mwalimu Luganda.

Ontieri anakiri kuwa ilhamu zaidi ya kukichapukia Kiswahili ilichangiwa na baadhi ya wanafunzi waliowatangulia kimasomo chuoni, akiwemo Prof Nathan Oyori Ogechi ambaye kwa sasa ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Moi.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa Ontieri msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Egerton kusomea shahada ya uzamili katika mwaka wa 2002. Hatua hiyo ilikuwa zao la kuhimizwa pakubwa na Dkt Samuel Obuchi.

Alihitimu mnamo 2005 baada ya kuwasilisha Tasnifu ‘Matumizi ya Lugha katika Magazeti ya Kiswahili mfano Gazeti la Taifa Leo’ chini ya uelekezi wa Dkt John Kimemia na Prof Aswani Buliba.

Ilikuwa hadi 2007 ambapo Ontieri alirejea katika Chuo Kikuu cha Egerton kwa minajili ya kusomea shahada ya uzamifu (PhD). Aliandaa Tasnifu ‘Uchanganuzi wa Makosa katika Insha za Wanafunzi wa Shule za Upili mfano wa Wilaya ya Nakuru’ chini ya uelekezi wa Prof James Onyango Ogola na marehemu Prof Mwenda Mukuthuria. Alifuzu katika mwaka wa 2010.

UALIMU

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma Ontieri kufundisha katika Shule ya Upili ya Kamobo, Kaunti ya Nandi mnamo 1993. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya Koitalel Samoei, Nandi (1994-1999).

Ontieri aliwahi pia kuwa mwalimu katika Shule ya Upili ya Moi Tea Girls, Kericho (1999-2002) na Kericho Boys High (2004-2008) kabla ya kufundisha katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Murang’a kati ya 2008 na 2009.

Hadi alipojiunga na Chuo Kikuu cha Rongo mnamo Februari 2020, Ontieri alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Kaunti ya Narok. Kabla ya kupanda ngazi kuwa Mhadhiri Mwandamizi mnamo 2015, alikuwa Mhadhiri (2011-2015) na Mhadhiri Msaidizi (2009-2010).

Ontieri amewahi pia kufundisha katika Chuo Kikuu cha St John’s (SJUT), Dodoma, Tanzania (Mei – Agosti 2018) chini ya mradi wa kubadilishana wahadhiri wa Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA).

UANDISHI

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Ontieri tangu alipoanza kufundisha. Idadi kubwa ya walimu wenzake walimpigia mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na wakamtia motisha ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa Fasihi ya Kiswahili.

Baada ya kuchapishiwa ‘Mwongozo wa Visiki’ (Khaemba Ongeti), Ontieri alishirikiana na Dkt Obuchi kuandika ‘Mwongozo wa Siku Njema’ (Ken Walibora).

Hadi kufikia sasa, Ontieri amechapishiwa makala tisa katika sura za vitabu mbalimbali na kuchangia makala mengine 14 ya kitaaluma katika majarida ya kimataifa.

Mbali na kuwa miongoni mwa wahariri wa ‘Jarida la Mwanga’ (Chuo Kikuu cha Moi) na ‘Jarida la Mnyampala’ (Chuo Kikuu cha St John’s); Ontieri amewahi pia kuwa mhariri wa vitabu mbalimbali vya Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA).

Alishirikiana na Dkt Mark Mosol Kandagor, Dkt Leonard Sanja na marehemu Prof Mukuthuria kuhariri kitabu ‘Kiswahili na Maendeleo’ (2015) kabla ya kushirikiana na Prof Ernest Sangai Mohochi na marehemu Prof Mukuthuria kuhariri kitabu ‘Kiswahili katika Elimu’ mnamo 2019.

UANACHAMA

Ontieri ni mwanachama wa vyama mbalimbali vya Kiswahili vikiwemo Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). Vyama hivi vimempa majukwaa mwafaka ya kusambaza maarifa, kuendeleza msingi imara wa lugha na kutoa mchango mkubwa katika uandishi, utafiti, ufundishaji na matumizi ya Kiswahili.

Ontieri ameongoza CHAKAMA katika nyadhifa mbalimbali. Amewahi kuwa Afisa wa Ushirikiano (2011-2013), Afisa Mwenezi (2013-2015), Naibu Mwenyekiti (2015-2017) na Mwenyekiti (2017-2019). Tangu 2015, amekuwa Mwenyekiti wa CHAKAMA–Kenya na anahudumu sasa katika Kamati Tendaji ya Afrika Mashariki.

Amewahi pia kuwa Mlezi wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara (2010-2015) na Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) kati ya 2017-2019.

Katika mengi ya makongamano ya vyama hivi, Ontieri amekuwa akitoa ushauri wa kitaaluma kwa wanafunzi na kuwahimiza walimu wenzake kuchochea kasi ya malengo mahususi ya kukuza Kiswahili katika nyanja zote ambamo lugha hii inatumika; pamoja na kuongeza ufanisi wa mawasiliano katika ufundishaji na utafiti wa maarifa ya aina zote mathalan uandishi na uchapishaji wa vitabu na majarida.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa, Ontieri anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wanataaluma wengi ambao amewaelekeza katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Baadhi yao ni Bw Aggrey Katima, Bi Fridah Oiko, Bi Martha Nyangweso, mwanariadha Wilfred Bungei, Dkt Mark Odawo, Dkt Stanley Kevogo, Dkt Jackline Ogolla na Seneta wa Kaunti ya Kericho, Aaron Cheruiyot.

Ontieri amewahi pia kuchangia mijadala ya kitaaluma kupitia vipindi vya ‘Bahari ya Lugha’ (Radio Citizen) na ‘Ramani ya Kiswahili’ (KBC Radio Taifa).

Kwa pamoja na mkewe Bi Joyce Kemunto, wamejaliwa watoto watatu – Sylvia Mandere, 24, Sheilah Kwamboka, 22, na Catherine Moraa, 13.