GWIJI WA WIKI: Dkt Naomi Musembi

GWIJI WA WIKI: Dkt Naomi Musembi

Na CHRIS ADUNGO

HATUWEZI kupiga hatua yoyote ya kusonga mbele bila kuvumiliana.

Jifunze kutokana na yaliyopita ndipo uweze kujenga ya sasa na kukabili yajayo.

Salia imara katika safari ya kufikia malengo yako. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta. Ruhusu mawazo yako yatawaliwe na fikira za ushindi. Mtangulize Mungu, vumilia na ujitume.

Pania kutenda mema, kipende kwa dhati hicho unachokifanya, jiwekee malengo ya mara kwa mara na ujiepushe na watu wasio na maono.

Huu ndio ushauri wa Dkt Naomi Nzilani Musembi – msomi na mwandishi shupavu wa fasihi ambaye kwa sasa ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST), Kaunti ya Siaya.

MAISHA YA AWALI

Naomi alizaliwa kijijini Malikini, Kaunti ya Machakos katika familia ya Bw Henry Musembi na Bi Phelis Wanza.

Alianza masomo katika Shule ya Msingi ya Malikini kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Moi High Mbiruri, Embu. Alifaulu vyema katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne na akajiunga na Chuo Kikuu cha Moi kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini).

Anakiri kwamba mapenzi yake kwa lugha hii ni zao la kuhimizwa na Bw Matano aliyemfundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Mbiruri. Wengine waliompokeza malezi bora ya kiakademia na kumchochea zaidi kukichapukia Kiswahili ni Prof Clara Momanyi, Prof Kitula King’ei na marehemu Prof Ken Walibora.

“Ken alinichochea pakubwa hasa baada ya kuisoma riwaya yake ya kwanza, ‘Siku Njema’”.

UALIMU

Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri Naomi mnamo 1996 na ikamtuma kufundisha katika Shule ya Upili ya Thome Andu Boys, Kaunti ya Makueni.

Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuhamia Wachoro Boys (1999-2000, Embu), Gitaraka Girls (2000-2001, Embu) na Kangaru Girls (2001-2005, Embu).

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa Dkt Naomi msukumo wa kusomea shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Alifuzu mnamo 2008 baada ya kuwasilisha tasnifu “Matumizi ya Taswira na Ukinzano kama Kichocheo cha Zinduko katika Riwaya za G.K. Mkangi” chini ya usimamizi wa Dkt Richard Wafula na Dkt Peter Mugambi.

Alifundisha katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha St John’s Kilimambogo, Kaunti ya Kiambu kati ya 2009 na 2010 kabla ya kuajiriwa na Chuo Kikuu cha Kenya Methodist (KeMU) mnamo 2011. Alifundisha huko kwa miaka sita kabla ya kuhamia JOOUST mnamo 2017.

Dkt Naomi alihitimu na shahada ya uzamifu (phD) mnamo 2016 baada ya kuwasilisha tasnifu “Mabadiliko ya Maudhui katika Nyimbo Jadiiya za Wakamba” chini ya uelekezi wa Prof Tom Olali na Dkt Pamela Ngugi.

UANDISHI

Sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani yake mnamo 2009. Kufikia sasa, amechapishiwa makala ya kitaaluma katika sura za vitabu na majarida mbalimbali ya kitaifa na ya kimataifa kama vile ‘Mwanga wa Lugha’, ‘Mediterranean Journal of Social Sciences’ n.k

Ametunga pia hadithi kadhaa za watoto zikiwemo ‘Dhiki Yangu’, ‘Malimwengu’, ‘Mkono wa Sheria’, ‘Paka Mtundu’ na ‘Nipe Sababu’. Oxford Publishers ilimtolea kitabu ‘Dhibiti PTE Kiswahili’ mnamo 2010.

Dkt Naomi ameandika miswada mingi ya fasihi ya watoto na hadithi fupi ambayo kwa sasa ipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu nchini Kenya.

UANACHAMA

Dkt Naomi ni mwanachama kindakindaki wa Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA), Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). Aliwahi kuwa Afisa Mwenezi wa CHAKITA kati ya 2017 na 2019.

Vyama hivi vimempa majukwaa mwafaka ya kusambaza maarifa, kuendeleza msingi imara wa lugha na kutoa mchango mkubwa katika uandishi, utafiti, ufundishaji wa Kiswahili.

JIVUNIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Dkt Naomi ni kuweka hai ndoto ya kuwa profesa na mwandishi mashuhuri wa fasihi ya watoto.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha inayotawala wanataaluma wengi ambao wametangamana naye katika ngazi na viwango tofauti vya elimu. Dkt Naomi kwa sasa ni mwanachama wa Bodi ya Usimamizi katika Shule ya Upili Karaba Boys, Embu.

Kwa pamoja na mumewe Bw Alex Muathe, wamejaliwa watoto wawili – Carol na Steve.

You can share this post!

TAHARIRI: Mapuuza ni hatari kwa haki na sheria

NASAHA: Kujitolea kukuza vipaji vya wengine kutakupa fursa...