Makala

GWIJI WA WIKI: Edwin Omoding Emoit

September 18th, 2019 5 min read

NA CHRIS ADUNGO

JIFUNZE kushinda hofu na amini katika ushindi.

Kujiamini ni mwanzo bora katika kulijaribu jambo lolote duniani.

Ukiamini kuwa huwezi kufanya kitu, ni kweli hutaweza! Ipo miujiza na nguvu kubwa ajabu katika kuamini! Bidii, nidhamu, imani na kutokata tamaa ndio msingi wa maisha!

Furaha na ustawi wa mwanadamu siku zote umejengeka katika msingi wa kutegemeana, kuhitajiana na kuchangiana mawazo. Ukamilifu katika maisha huchochewa na mchango wa marafiki wanaokuzunguka, si wanafiki ambao kubwa zaidi katika mipango yao huwa kuzima maono na ndoto zinazotawala fikra zako!

Huu ndio ushauri wa Bw Edwin Omoding Emoit; mwalimu mbobevu, mwandishi chipukizi wa fasihi, mshairi shupavu, mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za Injili ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Butula Boys, Kaunti ya Busia.

MAISHA YA AWALI

Omoding alizaliwa mnamo Novemba 1983 katika kijiji cha Apokor, eneo la Amukura, Teso Kusini, Kaunti ya Busia akiwa mtoto wa tatu kati ya wanane katika familia ya Bw Fabian Omoding na Bi Wilimina Opusi.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Apokor, Amukura alikosomea kati ya 1993 na 1996. Baadaye alijiunga na Shule ya Msingi ya Katelenyang, Teso Kusini. Huko ndiko alikofanyia mtihani wa KCPE mwishoni mwa 2000.

Alama nzuri alizozipata katika mtihani huo wa kitaifa zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya St Mark Moding, eneo la Ang’urai, Teso Kaskazini mnamo 2001.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 2004.

Miaka miwili baadaye, alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kusomea Shahada ya Elimu (B.Ed Arts). Alihitimu na kufuzu kuwa mwalimu wa Kiswahili na somo la Historia mnamo 2010.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimpa msukumo wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU), Bewa la Eldoret mnamo 2014 kusomea Shahada ya Uzamili katika Elimu ya Saikolojia.

Alihitimu mwishoni mwa 2016 chini ya usimamizi na uelekezi wa Dkt Baraza. Ili kupanua kabisa mawanda yake ya kielimu na kuendelea kuwa wa msaada zaidi kwa wanafunzi wake, Omoding anatazamia sasa kurejea chuoni kukisomea Kiswahili katika kiwango cha Shahada ya Uzamili.

Anatambua ukubwa wa mchango wa wazazi wake katika kumwelekeza vilivyo, kumshauri ipasavyo, kumhangaikia kwa kila hali na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Mbali na mama mzazi, mwingine aliyemshajiisha zaidi kujitahidi masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya upili ni Mwalimu Odisa ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Daystar.

Omoding anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa na kuhamasishwa pakubwa na aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili katika shule ya upili, Bi Beatrice Otogo ambaye kwa sasa ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya Bokoli Girls, Kaunti ya Bungoma.

Kariha na ilhamu zaidi ilichangiwa na wanafunzi wenzake waliompagaza jina ‘Kongowea’ baada ya kuvutiwa mno na ufasaha wake kila alipoyatema maneno ya lahaja mbalimbali za Kiswahili. Ari yake ya kutaka Kiswahili kipate makao salama na ya kudumu moyoni mwake iliamshwa na wahadhiri waliotangamana naye kwa karibu sana, kumpokeza malezi bora ya kiakademia na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichangamkia Kiswahili alaa kulihali akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Moi (Bewa Kuu), Eldoret.

Omoding alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliochangia kishujaa ufufuzi na uendeshaji wa Chama cha Kiswahili cha Moi (CHAKIMO) mnamo 2006 chini ya uongozi wa Bw Chris Adungo, Stephen Musamali, Simon Kigamba, Amidah Khalekha, Dickson Mwaniki na Peninah Wanjiku.

Zaidi ya Bw Davies Mukuria, mwingine aliyemchochea pakubwa kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hii ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi; ni Dkt Saidi Vifu Makoti ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Machakos.

UALIMU

Omoding alianza kufundisha katika Shule ya Upili ya St Paul’s Amukura, Teso Kusini mnamo Mei 2010. Akiwa huko, aliamsha ari ya kuthaminiwa zaidi kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na kuwachochea kuandikisha alama wastani ya 6.2 katika mtihani wa KCSE Kiswahili 2010. Awali katika mwaka wa 2009, shule hiyo ilikuwa imepata alama wastani ya 5.7 katika mtihani wa kitaifa wa Kiswahili.

“Wanafunzi walianza kushiriki zaidi mashindano ya uigizaji na kughani mashairi katika tamasha za kitaifa za muziki na drama. Jambo hili lilibadilisha pakubwa sura ya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili, nao walimu wakapata msukumo na hamasa zaidi.”

Omoding alivumisha Kiswahili Shuleni St Paul’s kiasi kwamba wanafunzi wake walisajili alama wastani ya 8.4 katika KCSE Kiswahili 2011. Mafanikio haya yalichangia kuteuliwa kwake kuwa mlezi wa Chama cha Kiswahili na Mkuu wa Idara ya masuala ya uteuzi wa taaluma miongoni mwa wanafunzi.

Aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) mnamo Mei 2012 na akawaongoza wanafunzi wake kujizolea alama wastani ya 9.4 katika KCSE Kiswahili mnamo 2014.

Ilikuwa hadi Mei 2018 ambapo alihamia katika Shule ya Upili ya St Louis Butula Boys, Kaunti ya Busia. Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili mwezi mmoja baadaye chini ya usimamizi wa Bw Daniel Ouma Onyango (Mwalimu Mkuu).

Omoding anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote ni zao la imani, bidii, nidhamu na mtazamo wake kuhusu somo lenyewe na mwalimu anayempokeza elimu na maarifa.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili Shuleni Butula Boys kwa sasa ni nguzo kubwa katika maandalizi yao kwa minajili ya KCSE 2019.

Baadhi ya walimu hao ni Makarios Makwata, Isaac Were, Caren Achieng, Celestine Obam, Derrick Efumbi na Chadwick Obwini.

Omoding amekuwa mtahini wa KCSE katika Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC) tangu 2011 na anajivunia tajriba pevu katika utahini wa Insha ambayo ni Karatasi ya Kwanza ya KCSE Kiswahili (KAR 102/1).

Uzoefu huu umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Zaidi ya kuhudhuria makongamano mbalimbali katika jitihada za kuchangia makuzi ya Kiswahili, amewahi pia kualikwa kufundisha, kuwashauri na kuwaelekeza walimu na wanafunzi katika shule mbalimbali za msingi na za upili ndani na nje ya Kaunti ya Busia.

UANDISHI

Omoding anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Nyingi za insha alizotunga zilimzolea sifa na kumvunia umaarufu miongoni mwa wenzake.

Isitoshe, ufundi mkubwa katika mashairi aliyoyasuka ni upekee uliompandisha kwenye majukwaa ya kila sampuli ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa na za kutamanika mno katika ulingo wa Kiswahili.

Mnamo 2016, kampuni ya Megawork Publishers, Nairobi ilimchapishia Omoding diwani Kurunzi ya Mashairi. Hiki ni kitabu alichoanza kukiandika akiwa katika Chuo Kikuu cha Moi baada ya aliyekuwa mwanafunzi mwenzake, Bw Barasa kumchochea zaidi kupenda Ushairi wa Kiswahili. Mengi ya mashairi yake yamekuwa yakighaniwa na wanafunzi katika tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Kwa sasa anaandaa upya mswada wa riwaya Dunia Haina Utu baada ya kazi ya awali aliyoanza kuiandika akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili kupotezwa na aliyekuwa mwalimu wake wa sekondari.

JIVUNIO

Omoding ni mtunzi na mwimbaji wa nyinmbo za Injili. Pia ni mchungaji katika kanisa la Christian Pentecostal Revival Centre, eneo la Akobwait, Teso Kusini. Kwa sasa ana albamu tano.

Kwa imani kwamba waimbaji wanaotumia Kiswahili wana nafasi kubwa katika kuchangia makuzi ya lugha, utamaduni na mawasiliano, nafasi ya Kiswahili, umuhimu wa uzalendo, maadili, elimu na uongozi bora ni miongoni mwa dhamira zinazoakisika katika baadhi ya vibao vya Omoding.

Anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Kwa pamoja na mkewe Bi Lilian Makokha Iluku, wamejaliwa watoto watatu: Alicia Willy, Damaris Akwii na Belvis Imelda.