Makala

GWIJI WA WIKI: Elizabeth Wangari

July 24th, 2019 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

FIKRA ambazo mtu huwa nazo kuhusiana na jambo fulani ndizo humpa msimamo na mtazamo wa maisha.

Ukiona mtu amekata tamaa, chanzo huwa ni mawazo yake!

Pania sana kuelewa wewe ni nani kwa kufahamu ukubwa wa uwezo ulionao. Kuwa na msimamo na usijilinganishe na mtu mwingine.

Ili ufanikiwe, ni vyema uwe na nidhamu katika hisia zako kwa kuwa ndiyo njia ya pekee ya kujifunza mambo mengi. Haitawezekana kabisa kwa mengi ya matarajio yako kutimia iwapo hutakuwa na malengo. Badili mtazamo wako kuanzia sasa na amini kwamba jitihada zako zitazaa matunda.

Utakapopania kutia bidii katika kazi yako, Mungu atafanikisha chochote utakachokitia mikononi. Mtumainie sana Mungu wako kwa kuwa ndiye wa pekee mwenye uwezo wa kukufungulia milango ya heri.

Huu ndio ushauri wa Bi Elizabeth Wangari Nyaga ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili na Jiografia katika Shule ya Upili ya St Bakhita Gataragwa Girls, Kaunti ya Nyeri.

Maisha ya awali

Elizabeth alizaliwa mnamo Desemba 3, 1977, katika eneo la Athi River, Kaunti ya Machakos akiwa kitinda mimba katika familia ya watoto watano wa marehemu Bw Stephen Muriuki na Bi Mary Wandia.

Elizabeth alianza elimu ya msingi katika Shule ya Mukangu, eneo la Karatina, Kaunti ya Nyeri mnamo 1985.

Mwaka mmoja baadaye, familia yake ilihamia katika eneo la Embu na hivyo kujipata akisomea katika Shule ya Msingi ya Kimangaru, Kaunti ya Embu kati ya 1986 na 1992.

Alama nzuri alizozipata katika mtihani wa KCPE mwishoni mwa 1992 zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya Masinga, Kaunti ya Machakos.

Hata hivyo, uchechefu wa fedha uliyazima kabisa matumaini yake ya kusomea katika shule hiyo na badala yake akalazimika kujiunga na Shule ya Upili ya Kutwa na Mseto ya Itabua, Embu mnamo 1993.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 1996. Ilikuwa hadi 1999 ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea Shahada ya Kwanza katika Ualimu (Kiswahili na Jiografia).

Elizabeth anatambua ukubwa wa mchango wa wazazi wake katika kumwelekeza, kumshauri na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Waliomshajiisha kujitahidi zaidi masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni Bw Kipotho, Bw Kangaru na Bw Ngarari waliomfundisha Kiswahili shuleni Kimangaru.

Mbali na Bw Munyiri aliyepanda na kuotesha ndani yake mbegu za kusoma kazi nyingi za Kiswahili, Elizabeth anatambua pia upekee wa mchango wa Bw Ndwiga aliyemfanya kuanza kuvutiwa sana na taaluma ya ualimu tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya upili.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa na Elizabeth kwa sasa katika ulingo wa Kiswahili ulichangiwa zaidi na tukio la yeye kufundishwa na watu ambao mbali na kubobea ajabu katika taaluma, pia waliipenda na kutawaliwa na ghera ya kuipigia chapuo lugha hii.

Anaungama kuwa mtagusano wa karibu aliokuwa nao na wahadhiri wake katika Chuo Kikuu cha Kenyatta; hasa Dkt Jacktone Onyango, Dkt Mathooko na Dkt Kamunde ulimpa ilhamu ya kukichangamkia Kiswahili alaa kulihali.

Kariha na motisha zaidi ilitoka kwa wanafunzi wenzake waliokuwa wakimpongeza kwa matamshi fasaha ya Kiswahili na upekee wa kiwango chake cha ubunifu katika utunzi wa nyimbo na mashairi.

Mwingine aliyemchochea pakubwa Elizabeth kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hii ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi ni Dkt Leonard Chacha aliyemtanguliza vyema zaidi katika kozi ya Isimu chuoni Kenyatta.

Ingawa kwa wakati fulani changamoto za kila sampuli zilitishia kuuzima kabisa mshumaa wa tumaini lake la kukamilisha masomo ya sekondari na chuo, Elizabeth anatambua ukubwa wa mafao aliyoyapokea kutoka kwa wazazi wake waliojinyima sana kwa minajili yake.

Msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ni miongoni mwa masuala yaliyomchochea zaidi kurejea katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Watoto.

Anatazamia kuhitimu na kufuzu mwishoni mwa mwaka ujao chini ya usimamizi na uelekezi wa Profesa Catherine Ndungo na Dkt Pamela Ngugi.

Ualimu

Baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu mnamo 2003, Elizabeth alipata kibarua cha kufundisha Kiswahili na masomo ya Jiografia, Biashara na Dini katika Shule ya Upili ya Kevote, Embu. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Kiriaini Girls, Embu alikoamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

Ni wakati akiwa Kevote ambapo alitambua utajiri wa kipaji alichonacho katika uigizaji, ulumbi na utunzi wa mashairi.

Mnamo 2008, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimwajiri Elizabeth na kumtuma kufundisha Kiswahili na Jiografia katika Shule ya Upili ya Garatagwa Girls anakofundisha hadi sasa.

Mbali na majukumu ya kufundisha, pia ni msimamizi wa mabweni, mlezi wa Chama cha Msalaba Mwekundu na mlezi wa Chama cha Kiswahili shuleni Gataragwa Girls (CHAKIGA).

Zaidi ya kuwa mwanajopo wa kutunga mitihani ya viwango mbalimbali katika Kaunti ya Nyeri, yeye pia ni mwamuzi wa kupigiwa mfano katika tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Elizabeth amekuwa mtahini wa kitaifa na mhakiki wa Karatasi ya Pili ya KCSE Kiswahili (Sarufi na Matumizi ya Lugha). Uzoefu huu umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuinua kiwango cha Kiswahili kwa kuwashauri na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu ibuka na mwafaka zaidi katika kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote ni zao la imani, bidii, nidhamu na mtazamo wake kuhusu somo lenyewe na mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni Gataragwa Girls ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaoujivunia kila mwaka matokeo ya KCPE yanapotangazwa.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto zake za kuwa profesa na mhadhiri wa Kiswahili, Elizabeth anaungama kuwa kikubwa zaidi kinachomridhisha nafsi ni tija ya kuwaona wengi wa wanafunzi wake wakitaka sana kuiga mfano wake na kujitosa katika ulingo wa Kiswahili kwa lengo la kuwa ama walimu maarufu, waandishi shupavu au wanahabari mashuhuri.

Katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja na nusu, Elizabeth amefundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Kwa pamoja na mumewe Bw Thomas Nyaga ambaye kwa sasa ni mhadhiri katika Chuo cha Kiufundi cha Nairutia, eneo la Kieni, Kaunti ya Nyeri, wamejaliwa watoto wanne: John Fortunatus Mutugi, Stephen Mutero, Caleb Wachira na Sage Mary Makena.