Makala

GWIJI WA WIKI: Erick Muteti

March 11th, 2020 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

DUNIANI tunamoishi mna mengi ya kuiga na mengi ya kuyafumbuia macho.

Dunia ina marafiki na pia maadui wengi.

Dunia ina watu watakaokutia moyo na wale wenye wivu na inda kama joka la mdimu. Duniani kuna wema watakaokuhongera kwa ubora wa vitendo vyako na wabaya watakaokukashifu kwa kila jambo bila. Nia yao huwa ni kukuangusha, kukuumbua na kukukwaza ili usipige hatua zozote kwenda mbele. Achana nao!

Ili ufanikiwe, unahitaji marafiki. Lakini ukitaka kufanikiwa zaidi, waweke mahasidi wako karibu nawe. Wewe ni wewe; cheza ki-wewe! Katika dunia hii, usiwahi kung’ang’ania nafasi ya mtu mwingine, ukajilinganisha naye na ukatamani kuwa kama yeye. Hiyo ni bahati yake na bahati ya mwenzio hata ukiifungulia mlango mkubwa kiasi gani, haitaingia! Wanaokupenda wapende; wasiokupenda achana nao!

Jiamini katika kila jambo unalolifanya na kithamini sana hicho unachokitenda. Ukipenda kazi yako, hutahitaji kusukumwa na mtu.

Licha ya kuwa vimbaumbau mwiko wa pilau, Wamaasai humuua simba! Si kwa jingine lolote, ila kwa kujiamini tu. Jiaminishe kwamba unaweza na unatosha!

Huu ndio ushauri wa mwandishi na mwalimu Erick Muteti ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika California Group of Schools katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi.

MAISHA YA AWALI

Mwalimu Muteti alizaliwa madongoporomoka miaka 30 iliyopita katika kijiji cha Kiambani, kata ya Ngwata, eneobunge la Kibwezi, Kaunti ya Makueni akiwa mwanambee katika familia ya watoto sita wa marehemu Bi Josephine na marehemu Bw Sammy Muteti.

Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Msingi Iongoni, Makueni. Alikuwa akitembea peku kama ilivyokuwa ada na desturi nyakati hizo ambapo watoto walinunuliwa viatu kwa minajili ya safari za kuenda kanisani au kuwatembelea mashangazi.

Licha ya changamoto nyingi za kila sampuli, Muteti anaungama kuwa maisha yalikuwa ya kutamanisha sana. Shule ya Msingi ya Iongoni alikosomea haikuwa mbali na nyumbani kwao. Mwalimu Mkuu wa shule hiyo wakati huo alikuwa Bw Mutinda aliyemtangulia Bw Elijah Munyw’oki. Mbali na kumwelekeza Muteti katika mkondo wa nidhamu kali, walimu hao walimhimiza ajitahidi masomoni na wakampokeza malezi bora ya kiakademia.

Kitumbua cha Muteti kilikaribia kuingia mchanga baada ya mauko ya babaye mzazi. Bw Sammy aliaga dunia mwanawe Muteti akiwa mwanafunzi wa darasa la nane. Ama kweli, mti mkuu ukigwa wana wa ndege huyumba!

Kwa bahati ya mtende, ami yake Bw Kituu na mwanawe Douglas Kituu waliyafadhili masomo yake ya sekondari katika Shule ya Upili ya Dr Ugo Mazzones Kavingoni – skuli ya mbali sana na kwao iliyoko katika sehemu za Wote, eneo la Kathonzweni, Makueni. Ilimlazimu Muteti agurie kwa ami yake!

Ufadhili alioupata haukuwa wa kuutemea mate. Ilimjuzu kuuma uzi wa masomo kwelikweli. Alijitafutia pesa za masurufu kwa kuwachotea wanakijiji maji na kuwachungia mifugo wao kila wikendi. Muteti aliamini kuwa ukibebwa, usilevyelevye miguu! Anatambua pia ukubwa wa mchango wa familia ya Kamayas iliyomwashia mshumaa wa matumaini yaliyoning’inizwa kwenye uzi mwembamba wa imani.

Licha ya panda-shuka tele, Muteti hakufa moyo. Changamoto alizokabiliana nazo zilimshajiisha hata zaidi. Tangu kidato cha kwanza hadi cha nne, ilijulikana wazi kama kisima na lazima kama ibada kuwa nambari ya kwanza darasani ilikuwa yake. Hadi sasa, ‘kushindwa’ ni neno ambalo Muteti anahisi kwamba liliingizwa katika kamusi za Kiswahili kimakosa.

Baada ya kukamilisha masomo ya sekondari, alirejea kwao Kibwezi. Kwa sababu ya matokeo bora aliyoyasajili katika mtihani wa KCSE, walimu wake wa awali katika Shule ya Msingi ya Iongoni walimpa kibarua cha kufundisha. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka miwili akipokezwa mshahara wa Sh1,800 kwa mwezi.

Kwa imani kwamba akiba haiozi, alikuwa akihifadhi hela kichele kila mwezi. Nia na madhumuni yalikuwa ni adudulize fedha kiasi cha haja ili angalau ajiendeleze kimasomo. Mipango yake ilikamilishwa kwa Harambee aliyoiandaa kijijini mwao. Mbali na cheti cha ualimu, Muteti ana astashahada katika masuala ya uanahabari kutoka chuo kimoja tajika jijini Nairobi.

Mbegu zilizoamsha hamu na mshawasha wa kukichapukia Kiswahili zilipandwa na kuoteshwa ndani yake na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Nuhu Zubeir Bakari na Munene Nyaga wakati wa kipindi cha ‘Kamusi Ya Changamka’ kilichokuwa kipeperushwa na idhaa ya Q-FM na Q-TV.

Michango ya mikota hawa wa lugha ilimfanya Muteti kuzamia kamusi anuwai na kuufanya utafiti wa kina. Utafiti huo ulimwezesha kushindana vilivyo na akina Mzee Mzima na Malongo Mulatya ambaye pia alikuwa mshindani wake mkuu katika kuyajibu maswali katika kipindi cha ‘Ukarabati wa Lugha’ kilichokuwa kikiendeshwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah katika idhaa ya KBC. Ushindani huu ulijenga urafiki wa dhati kati ya Muteti na mabwana hawa wafia-lugha.

MCHANGO WA KITAALUMA

Muteti ameacha alama nzuri za kudumu katika shule zote ambazo amewahi kufundisha: Lizar Schools (Naivasha), Vickmery (Ruai) na Silvergate (Saika). Umilisi wake wa Kiswahili umemvunia mengi.

Baada ya kampuni ya Frajopa Printers Nairobi kumchapishia kitabu ‘Malezi ya Lugha’ mnamo 2007, Muteti alijitosa kabisa katika ulingo wa uandishi – sanaa ambayo anaamini ilianza kujikuza ndani yake tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Ameandika novela ‘Mjukuu Wangu’ na kushirikiana na Mwalimu Wafula wa Wafula na Bw Paul Eseme kuuandaa mkusanyiko wa hadithi fupi katika diwani ‘Mama Amerudi na Hadithi Nyingine’. Kitabu hiki kilichapishwa na kampuni ya Bustani Language Solutions Nairobi mnamo 2019.

Muteti pia ni mtunzi mahiri wa mitihani ya Kiswahili kwa wanafunzi wa shule za msingi. Kwa sasa anaandaa vitabu vya Insha kwa madarasa 4-5 (mtaala mpya) na hadithi za watoto anazotarajia kuchapishwa hivi karibuni.

Isitoshe, yeye ni mshauri wa masuala ya Kiswahili na mkalimani katika kampuni ya Pinnacle Interpretation, Nairobi. Majuzi, alichaguliwa kuwa Katibu wa Chama cha Wasomaji wa Kitaifa wa gazeti la ‘Taifa Leo’ (WAKITA) katika eneo la Nairobi.

MAAZIMIO

Mola akiridhia kwa kuwa mja hupata ajaliwalo na si alitakalo, Muteti anaazimia kuwa mhariri na mwandishi shupavu wa Kiswahili hapa nchini na duniani kote. Kielelezo chake daima ni Baba wa Takrima na Doyen wa Kiswahili, Guru Ustadh Wallah Bin Wallah wa WASTA Kituo cha Kiswahili Mufti, Matasia, Ngong.

JIVUNIO

Muteti anajivunia tuzo chekwachekwa kutokana na mapenzi yake kwa Kiswahili. Amechangia kishujaa katika uendeshaji wa vipindi vya Kiswahili katika redio za humo nchini: Nuru ya Lugha (Redio Maisha), Ramani ya Lugha, (KBC), Ukarabati Wa Lugha (enzi zile KBC), Bahari ya Lugha (enzi zile Redio Citizen) na Kamusi Ya Changamka (enzi zile Q-FM). Kituo cha WASTA kimemtambua mara kwa mara na kumtuza pakubwa!

Heshima na utulivu wa Muteti umemvunia marafiki wengi ambao kwa sasa hutangamana naye kwa karibu sana.

Anajivunia mlahaka mzuri kati yake na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Hassan mwana wa Ali, Mathias Momanyi, Abubakar Tsalwa, Amina Vuzo, Titus Sakwa, Okello Mjomba, Mathias Momanyi, Tom Nyambeka, Mwalimu Kombo, Rebecca Nandwa, Fred Obondo, Geoffrey Mung’ou, Zack Yaona na Profesa Said A. Mohamed. Anashikilia kwamba hakuna mti uendao bila nyenzo na ukiujua huu na huu huujui!

Muteti ameoa totoshoo Aziza Katherine (Mama Clian). Kwa pamoja, wamebarikiwa watoto wawili wa kiume: Mark Ian na John Clinton ambao kwa sasa ni wanafunzi katika Shule ya Msingi Komarock, Nairobi.