GWIJI WA WIKI: Fatma Ali Mwinyi

GWIJI WA WIKI: Fatma Ali Mwinyi

Na CHRIS ADUNGO

JIFUNZE kuwa na msimamo katika maisha.

Usiwe bendera ifuatayo upepo.

Usiruhusu kamba yako ya matumaini kukatwa na yeyote. Tafuta marafiki watakaokujenga badala ya kukubomoa.

Kubali kurekebishwa ili uboreke zaidi. Jifunze kujifunza na uwe mwadilifu. Usiwe na mtazamo hasi kuhusu maisha. Shukuru ukifanikiwa kupata na ujitume zaidi ukikosa kufaulu. Mtegemee Mungu katika mambo yote!

Huu ndio ushauri wa Bi Fatma Ali Mwinyi – mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret, anayeinukia vyema katika uandishi wa Fasihi ya Kiswahili.

MAISHA YA AWALI

Fatma alizaliwa mnamo Machi 9, 1998 katika mtaa wa Barisheba, Kaunti ya Mombasa. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watano wa Bw Ali Mwinyi na Bi Najma Omar. Nduguze ni Binti Ali, Khamis Ali, Khadija Ali na Swabra Ali.

Alilelewa na nyanya yake, marehemu Bi Queen Kadiri, katika eneo la Rabai, Kaunti ya Kilifi kabla ya kurejea Mombasa alikoishi na mama yake mkubwa, Bi Rahma Omar.

Hali hiyo ilichangiwa na wingi wa shughuli za kikazi zilizomzonga mamaye mzazi ambaye ni nesi; naye baba alikuwa wakati huo akisomea shahada katika Chuo cha Utalii. Familia ya Bw Mwinyi ilihamia baadaye katika mtaa wa Mtopanga, Mombasa.

Nyanya wa upande wa mama, Bi Khadija Mohammed, amekuwa mstari wa mbele katika kumwelekeza Fatma kimaadili, kumtia katika mkondo wa nidhamu kali na kumshajiisha maishani.

Bi Khadija ambaye ana usuli Pemba, ndiye alimwamshia mjukuu wake huyu ari ya kukichapukia Kiswahili baada ya kumwathiri pakubwa kutokana na upekee wa lafudhi yake.

Ama kweli, jungu kuu halikosi ukoko na kinolewacho hupata!

ELIMU

Fatma alianza safari yake ya elimu mnamo 2000 katika Shule ya Msingi ya Bashiri, Mombasa. Alisomea huko hadi darasa la tatu kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Bahwan, Mombasa mnamo 2004. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwishoni mwa 2011.

Mbali na wazazi, walimu walikuwa wepesi katika kumhimiza Fatma kujitahidi masomoni baada ya kutambua utajiri wa kipaji na uwezo wake katika Kiswahili.

“Fatma jifunge kibwebwe katika somo langu la Kiswahili. Uwezo unao na alama hafifu kwako ni mwiko.” Maneno hayo ya mara kwa mara kutoka kwa Bw Issa Juma yalimpa Fatma msukumo wa kuanza kuthamini na kukichangamkia Kiswahili tangu utotoni.

Wengine waliopanda mbegu zilizootesha ari yake ya kukipigia Kiswahili chapuo ni Bw Luguah, Bw Leakeh na Bw Onyango aliyejitolea kupiga msasa matumizi yake ya lugha kwa kunyosha sarufi, tahajia na hati ya mwanafunzi wake huyu.

Fatma aliishia kuwa miongoni mwa waandishi bora wa Insha za Kiswahili na Kiingereza shuleni na akawa maarufu sana miongoni mwa walimu na wanafunzi wenzake.

Baada ya kuhitimu masomo ya shule ya msingi, alijiunga na Shule ya Upili ya Kwale Girls alikosomea kati ya 2012 na 2015.

Umahiri wa Fatma katika somo la Kiswahili ulidhihirika zaidi katika kiwango hiki cha elimu na akawa mwanafunzi wa kwanza katika mitihani yote ya Kiswahili hadi Kidato cha Nne.

Akiwa huko, alishiriki kikamilifu shughuli za Chama cha Kiswahili cha Kwale Girls na kupata jukwaa maridhawa la kuchangia makuzi ya Kiswahili shuleni. Alikuwa akiandika taarifa za matukio mbalimbali na kuwapa wenzake wasome gwarideni.

Walimu waliazimia haja ya kukuza na kupalilia talanta yake. Bw Jumaine Makoti na Bw Alphonce Kaka walijitolea kumpa Fatma vitabu mbalimbali vya hadithi na kumteua mara kwa mara kusoma vifungu vya Ufahamu darasani.

Chini ya uelekezi wa walimu hawa, Fatma alishiriki mashindano mengi ya kutoa hotuba na kujizolea tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha mno.

Alivutiwa pia na michezo ya kuigiza na akawa mshiriki wa mara kwa mara wa tamasha za muziki na drama. Fursa hizo zilimwezesha kunoa kipaji chake cha ulumbi na kuinua kiwango chake cha umilisi wa lugha.

Isitoshe, Fatma alitamba sana katika mashindano ya Fasihi ya Kiswahili yaliyohusisha shule mbalimbali kutoka ndani na nje ya Kaunti ya Kwale. Ubora wake katika mashindano hayo uliwahi kumzolea ‘Kamusi ya Karne ya 21’ na kitabu cha ‘Marudio na Mazoezi ya Kiswahili’. Tuzo hizo zilimwamshia ilhamu ya kuzamia kabisa somo la Kiswahili na akazidi kuwa wembe darasani.

UANDISHI

Fatma ni mwandishi anayeinukia vyema katika sanaa ya uandishi wa kazi bunilizi. Aliwahi kushiriki mashindano mbalimbali ya uandishi akiwa mwanafunzi wa shule ya upili na akawapiku wenzake wa vidato vya juu.

Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango mbalimbali na kumpa fursa ya kupanda majukwaa tofauti ya makuzi ya Kiswahili.

Kufikia sasa, anajivunia kuandika na kuchapishiwa kazi kadhaa za kibunifu. Baadhi ya hadithi zake ni ‘Ibra’ katika mkusanyiko wa ‘Shaka ya Maisha na Hadithi Nyingine’ (The Writers’ Pen Publishers, 2020) na ‘Mshahara wa Dhambi’ katika diwani ya ‘Maskini Maarufu na Hadithi Nyingine’ (African Ink Publishers, 2020).

Fatma ameandika pia miswada ya riwaya na tamthilia ambayo sasa ipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji chini ya mwavuli wa Chama cha Waandishi wa Kiswahili (CHAWAKI). Kazi zake zinazidi kupata umaarufu miongoni mwa washikadau katika sekta ya elimu, hasa walimu na wanafunzi katika shule mbalimbali nchini Kenya.

KICHOCHEO

Kilichomchochea Fatma kujitosa katika ulingo wa uandishi wa Kiswahili ni ukubwa wa kiwango cha kuathiriwa na kazi za Prof Said A. Mohamed, Mohammed S. Mohammed, Penina Muhando Mlama, Zainab Burhani, Pauline Kea Kyovi na marehemu Prof Ken Walibora.

Wengine ambao wamekuwa wakimchochea pakubwa na kumpa ari ya kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi wa vitabu ni Dkt Collins Kenga Mumbo, Dkt Harriet Ibala, Bw Vincent Magugu na Dkt Robert Oduori – mikota na walezi wa Kiswahili waliompigia mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi bunilizi.

Fatma amewahi kuwa mwalimu katika Shule ya Upili ya Kwale Boys, Shule ya Msingi ya Bridge(Mtopanga) na Shule ya Mumias Muslim Girls(Kakamega).

Bw Richard Amunga Ondoli ambaye pia ni mwandishi chipukizi wa Fasihi ya Kiswahili, amechangia pakubwa kustawisha uandishi wa Fatma anayemstahi sana mwanahabari Hassan Mwana wa Ali (Redio Maisha). Fatma kwa sasa anashirikiana na wanafunzi wenzake – Papaa kombo, Amunga na Said Hamisi kuchangia mijadala ya kitaaluma (Isimu ya Kiswahili) kupitia msururu wa video za ‘Youtube’.

UANAHABARI

Fatma ni mwanachama wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi (CHAKIMO) na huchangia makala, mashairi na habari mbalimbali katika jarida la ‘Dafina Wiki Hii’ ambalo ni chapisho maalumu la CHAKIMO kila Jumatatu na Ijumaa.

Aliwahi kushiriki uendeshaji wa kipindi ‘Dafina ya Lugha’ na kutangaza habari za saa tatu asubuhi kila Ijumaa katika idhaa ya MU-FM (103.9) kwa miaka miwili ya kiakademia (2018-19). Alitawazwa Mtangazaji Bora wa Mwaka katika maadhimisho ya ‘Siku ya Vipawa’ katika Chuo Kikuu cha Moi mnamo 2019.

Ameshirikiana pia na wanafunzi wenzake kuandaa michezo mbalimbali ya kuigiza pamoja na kuandika ‘Miongozo’ ya vitabu teule vya fasihi vinavyotahiniwa katika KCSE Kiswahili.

Aidha, amekuwa mstari wa mbele kuwaongoza wanachama wenzake wa CHAKIMO kuzuru shule mbalimbali kwa nia ya kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

MAAZIMIO

Kubwa zaidi katika maazimio ya Fatma ni kuzamia kabisa taaluma ya Kiswahili na kuweka hai ndoto ya kuwa profesa. Analenga pia kuwa mwanazuoni atakayekuwa kiini cha motisha itakayotawala wanataaluma wengi wa kike watakaoinukia katika bahari ya Kiswahili. Anaazimia kuwa mmliki wa kampuni ya uchapishaji itakayokuwa na malengo mahsusi ya kutambua, kukuza na kulea vipaji vya waandishi chipukizi.

You can share this post!

WASONGA: Covid: Kenya isitoe chanjo kwa wafanyakazi wa...

NASAHA: Hakikisho la kufanya vizuri ndicho kichocheo kwa...