GWIJI WA WIKI: Geoffrey Mwamburi

GWIJI WA WIKI: Geoffrey Mwamburi

Na CHRIS ADUNGO

SAUTI ya kurindima inayopasua mawimbi kwa wepesi ndio upekee wa Geoffrey Mwamburi Mwaviswa (Beki wa kupanda na kushuka) kila anapojipata nyuma ya bomba katika majukwaa ya utangazaji wa mpira.

Alizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Kilulu, eneo la Shimba Hills, Msambweni, Kaunti ya Kwale. Ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto watano wa Bw Jacob Mwaviswa na Bi Jaldrine Wambuga Mwangura.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Msingi ya Kilulu kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Shimba Hills (2005-2008). Alisomea Habari na Mawasiliano katika Chuo cha Mombasa Aviation mnamo 2009 kabla ya kujiendeleza kitaaluma baadaye.

Utangazaji ni kipaji kilichoanza kujikuza ndani ya Mwamburi akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Alitia azma ya kukipalilia zaidi chini ya uelekezi wa marehemu Gilbert Simiyu Wawire aliyekuwa mwalimu wake shuleni Shimba Hills.

“Mbali na mazoea ya kusikiliza redio nikiwaiga watangazaji wazoefu wa mpira kutoka Kenya na Tanzania, ukubwa wa uwezo wangu katika Kiswahili ulinielekeza katika ulazima wa kujitosa katika taaluma ya uanahabari,” anasema.

Zaidi ya Ezekiel Juma Malongo, Jesse John, Juma Nkamia na marehemu Halima Mchuka, wanahabari wengine waliomchochea Mwamburi katika utangazaji wa soka ni Jack Oyoo Sylvester, Ali Salim M’Manga, Torome Tirike na marehemu Mohammed Juma Njuguna.

“Nilikuwa mwepesi wa kusoma habari za michezo gwarideni nikiwa shuleni. Ujasiri huo ulichangia kunoa kipaji changu cha ulumbi, nikawa maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzangu.”

Mwamburi alianza kuandalia idhaa ya KBC ripoti za michezo akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu kwa usaidizi wa Cheye David. Aliaminiwa kuwa mfawidhi wa shughuli zote za michezo katika eneo la Pwani na akapata fursa ya kutangamana na wanahabari maarufu waliompigia mhuri wa kuwa mtangazaji bora wa redioni.

Baada ya kupata mafunzo ya nyanjani katika idhaa ya Pwani FM mnamo 2009, alianza kutangaza mpira wakati wa vipute mbalimbali vilivyoandaliwa na wanasiasa katika eneo la Pwani.

Aliajiriwa na kituo cha kimataifa cha Sifa FM, Voi mnamo 2010 kuwa msomaji wa taarifa za alasiri na mwendeshaji wa vipindi vya dini na michezo.

Ilikuwa hadi 2011 ambapo alijiunga na Royal Media Services (RMS) kuwa mtangazaji wa Bahari FM. Alihudumu huko kwa miaka mitatu akiwa mtayarishaji wa vipindi ‘Kwasinda’, ‘Mwangaza’ na ‘Uhondo Michezoni’. Alijiunga na Radio Citizen inayomilikiwa pia na RMS mnamo 2013 kuwa mtangazaji wa mpira na mwendeshaji wa vipindi.

Mwamburi alitangaza fainali za SportPesa Super Cup kati ya Gor Mahia na Everton nchini Tanzania mnamo 2017, Kombe la Mataifa Bingwa Afrika kwa Wanawake (AWCON) nchini Ghana mnamo 2018 na makala ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwaWanawake mnamo 2021 nchini Misri.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kukuza na kulea vipaji vya wanahabari chipukizi katika ngazi na viwango tofauti.

“Usijitose katika taaluma ya uanahabari iwapo lengo lako ni kutafuta umaarufu. Mtangulize Mungu katika kila hatua. Tia bidii na udumishe nidhamu. Usiwe na majivuno baada ya kufaulu. Majivuno huzaa dharau,” anashauri.

You can share this post!

Kenya ilivyozoa medali 6 taekwondo Afrika 2021 Ogalo...

KAULI YA MATUNDURA: Baadhi ya tamathali za usemi ambazo...

T L