GWIJI WA WIKI: Gladys Mungai

GWIJI WA WIKI: Gladys Mungai

NA CHRIS ADUNGO

UANAHABARI ni taaluma ambayo Gladys Mungai alianza kuvutiwa nayo katika umri mdogo.

Alianza masomo akifahamu thamani ya Kiswahili na umuhimu wa vyombo vya habari.

Alipokamilisha KCSE, alihiari kutupilia mbali fursa ya kusomea ualimu katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), ili kusomea uanahabari katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU), Bewa la Nairobi (2012-2015).

“Nilikuwa shabiki mkubwa wa vipindi vya lugha redioni na runingani. Mazoea ya kuvisikiliza na kuvitazama yalinitandikia zulia zuri la lugha na kunipa utashi wa kuwa mwanahabari. Nilikuwa pia mwepesi wa kujirekodi nikiwaiga baadhi ya watangazaji maarufu,” anasema.

Baada ya kutambua kipaji chake cha utangazaji, Gladys alitia azma ya kukipalilia.

Alianza kutunga na kukariri mashairi na akawakilisha shule yake ya msingi katika mashindano ya tarafa.

Alipoingia sekondari, tayari alikuwa mwandishi stadi wa insha ambazo aliziwasilisha kwa ufundi wa kustaajabisha.

Alijiunga pia na makundi ya uimbaji na uigizaji yaliyokuwa yakitumbuiza wageni kwa nyimbo na maigizo nyakati za hafla mbalimbali shuleni.

Walimu nao walimpa fursa za kughani mashairi darasani na kusoma habari za matukio tofautitofauti gwarideni. Majukwaa hayo aliyopata yalichangia vilivyo kunoa kipawa chake cha ulumbi na akawa maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Mbali na Bw Victor Gatimu Njenga (Mwalimu Mkuu), wengine waliompokeza Gladys malezi bora ya kiakademia katika shule ya upili na kumchochea pakubwa kujitosa katika tasnia ya uanahabari baada ya kutambua uwezo wake katika Kiswahili ni Bw Samuel Ng’ang’a, Bw Warutumo na Bw Mukuria.

Gladys alilelewa katika eneo la Lanet, Kaunti ya Nakuru.

Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watano wa Bw David Mungai na Bi Margaret Wambui. Safari yake ya elimu ilianzia katika shule ya msingi ya Kianda, Nakuru kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Bavuni, Nakuru (2007-2010).

Yeye kwa sasa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) anakosomea Udiplomasia na Mahusiano ya Kimataifa.

Baada ya kupokea mafunzo ya nyanjani katika kampuni ya mawasiliano ya Standard Group (SG) mnamo 2016, Gladys aliajiriwa na kituo cha Ebru TV kuwa mtangazaji wa habari za Kiswahili na mtayarishaji wa makala ya vipindi mbalimbali runingani.

Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kujiunga na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) mnamo Novemba 2018.

Mbali na kuwa ripota wa matukio ya bungeni na masuala ya kisiasa katika KBC Channel 1, yeye pia ni msomaji wa habari za ‘Darubini’ na mwendeshaji wa kipindi ‘Tamrini’.

Gladys Mungai wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO

Anashiriakana vilevile na mwanahabari Harith Salim kutayarisha na kuendesha kipindi ‘Kenya Yaamua’ kila Jumapili.

Zaidi ya kuwa mfanyabiashara jijini Nairobi, Gladys amewekeza pakubwa katika sekta ya kilimo.

Anamiliki Wakfu wa Gladys Mungai unaoshughulikia afya ya kiakili na kuchangia elimu kwa watoto wanaotokea katika familia maskini.

Anapolenga kujitosa katika medani ya siasa na kuwania ubunge mnamo 2027, analenga pia kukuza na kulea vipaji vya wanahabari chipukizi katika ngazi na viwango tofauti.

Maazimio yake mengine ni kuwa miongoni mwa wadau wakuu wenye uwezo wa kutoa maamuzi muhimu katika tasnia ya uanahabari nchini Kenya.

“Kufaulu katika uanahabari kunahitaji mtu kuwa na msukumo, ari na mshawasha wa kujikuza kitaaluma. Kipende unachokifanya, weka Mungu mbele na ujitume ipasavyo,” anashauri.

You can share this post!

NGUVU ZA HOJA: Baadhi ya changamoto zinazokumba makuzi ya...

Ukoo wa Jaramogi wavuna tiketi za ODM kuwania vyeo Agosti

T L