Makala

GWIJI WA WIKI: Hannah Mbuthia

August 7th, 2019 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

CHANGAMOTO za mara kwa mara ambazo tunazipitia maishani zinakusudiwa kutukomaza, kutunoa vilivyo na kutufanya kuwa watu bora.

Utakapoanza kutia bidii katika kazi yako, Mungu atafanikisha chochote utakachokiweka mikononi mwako.

Mwamini sana Mungu wako kwa kuwa ndiye wa pekee mwenye uwezo wa kukufungulia milango ya heri.

Mtumainie katika kila jambo na mpe nafasi afanye kazi yake katika maisha yako kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka na rehema zote. Amini kwamba hakuna lisilowezekana na vyovyote uwazavyo, ndoto zako zitakuinua iwapo utaziwekea dira.

Huu ndio ushauri wa Bi Hannah Mbuthia – mshairi shupavu, mwandishi chipukizi na mwalimu mbobevu ambaye kwa sasa ni Mlezi wa Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Josephs Githunguri Boys, Kiambu.

Maisha ya awali

Hannah alizaliwa mnamo 1970 katika kijiji cha Kianjogu, eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu akiwa mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanane wa Bw Joseph Mbuthia na marehemu Bi Mary Wangui.

Alilelewa katika utamaduni uliosisitiza ulazima wa mtoto kuadhibiwa na kushauriwa na mzazi yeyote kwa kuwa jukumu la ulezi lilikuwa la jamii nzima.

Ingawa hivyo, mapitio hayo magumu katika maisha ya utotoni hayakumtamausha wala kumvunja moyo.

Alijiunga na Shule ya Msingi ya Giathieko, Kiambu mnamo 1976 na kuufanya mtihani wa CPE mwishoni mwa 1982 katika mfumo wa elimu wa 7-4-2-3 (kabla ya majilio ya mtaala wa 8-4-4).

Alama nzuri alizojizolea zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya All Saints Sagana alikosomea kati ya 1983 na 1986.

Alifaulu vyema katika mtihani wa Kidato cha Nne (KCE) kwa kupata Division II na hivyo kujipa fursa ya kusomea A-Levels katika Shule ya Upili ya Loreto Kiambu Girls kati ya 1987 na 1988.

Katika mtihani wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Kidato cha Sita (KACE), alipata 3 Principals na Subsidiary (pointi 8), kasoro alama mbili pekee ajiunge na chuo kikuu kwa njia ya moja kwa moja wakati huo.

Alijiunga na Chuo cha Walimu cha Kaimosi, Kaunti ya Vihiga mwanzoni mwa 1994 na kufuzu miaka miwili baadaye.

Anatambua ukubwa wa mchango wa wazazi wake katika kumwelekeza, kumshauri na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Mbali na mwalimu Damaris Wainaina aliyemshajiisha zaidi masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, mwingine aliyemhimiza kujitahidi ni Bw Kiuyuru ambaye alipanda na kuotesha mbegu za mapenzi ya dhati kwa Kiswahili ndani ya mwanafunzi wake huyu.

Hannah anamstahi sana mwalimu Waithera Karanja kwa kumpokeza malezi bora ya kiakademia katika Shule ya Upili ya All Saints Sagana kabla ya Bw Njenga kumtanguliza vyema zaidi katika somo la Fasihi ya Kiswahili shuleni Loreto Kiambu Girls.

Akiwa huko, alijijengea desturi ya kusoma kazi nyingi za Kiswahili, utashi wake katika lugha hii ukakua na kupevuka mno kiasi cha wengi aliosoma nao kuanza kumuiga.

Hannah anakiri kwamba mtagusano wa karibu aliokuwa nao na wahadhiri wake katika Chuo Kikuu cha Nairobi; hasa Dkt Ayub Mukhwana, Prof Rayya Timamy na Prof Iribemwangi ulimpa ilhamu ya kuzitalii taaluma za Kiswahili.

Kariha na motisha zaidi ilitoka kwa wanafunzi wenzake waliokuwa wakimpongeza kwa upekee wa kiwango chake cha ubunifu katika utunzi wa nyimbo na mashairi.

Mwingine aliyemchochea pakubwa kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hii ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi ni Prof John Habwe aliyemvutia sana kila alipokuwa akikiendesha kipindi ‘Lugha Yetu’ katika KBC Idhaa ya Taifa.

Zaidi ya kuvutiwa na taaluma ya utangazaji, hamu ya kuwa mwalimu ilianza pia kumwandama Hannah tangu akiwa kitoto kidogo.

Ualimu

Miaka miwili baada ya kukamilisha masomo ya kidato cha sita, Hannah alipata kibarua cha kufundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Gachika, Kaunti ya Nyeri. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka minne hadi mnamo Aprili 1994.

Baada ya kuhitimu mwishoni mwa 1996, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma katika Shule ya Msingi ya Gichocho, Kiambu alikofundisha kwa miaka 14.

Akiwa huko, msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ulimchochea kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea Shahada ya Kwanza katika taaluma ya ualimu (Kiswahili na Dini) kati ya 2003 na 2008.

Baada ya kufuzu, alihudumu shuleni Gichocho kwa miaka miwili zaidi kabla ya TSC kumhamisha hadi Shule ya Upili ya St Joseph’s Githunguri Boys. Anatambua mapokezi mazuri kutoka kwa aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo wakati huo, Bw Kamau na Naibu wake Bw Gitau.

Zaidi ya kufufua ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi shuleni Githunguri Boys, Hannah alianza pia kuwashirikisha katika utunzi wa mashairi kwa minajili ya tamasha za kitaifa za muziki na drama ambapo yeye ni mwamuzi wa kupigiwa mfano.

Pia alipokezwa majukumu ya kuwa mlezi wa Chama cha Kiswahili na hivyo kupata jukwaa mwafaka zaidi la kutambua na kukuza vipaji vya uigizaji, ulumbi na uandishi wa kazi za kibunifu miongoni mwa wanafunzi wake.

Hannah amewahi kuwa mtahini wa KCPE katika Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC) kati ya 2003 na 2011. Tangu 2013, amekuwa mtahini wa Karatasi ya Tatu ya KCSE Kiswahili (Fasihi).

Uzoefu huu umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni Githunguri Boys (Bi Scholar Ihugo, Bi Stella Kinyanjui, Bw Allan Waititu, Bw Makori, Bw Thuo na Bi Muohi), ni nguzo kubwa katika mafanikio yao chini ya usimamizi wa Bw Francis Miano Wachira ambaye ni Mwalimu Mkuu.

Uandishi

Hannah anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Nyingi za insha na mashairi aliyoyatunga yalimzolea sifa na kumvunia umaarufu miongoni mwa wenzake.

Isitoshe, ufundi mkubwa katika tungo alilzozisuka ni upekee uliompandisha kwenye majukwaa ya kila sampuli ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa. Kwa sasa anatayarisha kitabu ‘Marudio ya KCSE Ushairi’ ambacho anaamini kitawanufaisha wanafunzi na walimu wengi wa shule za upili.

Jivunio

Katika kipindi cha takriban miongo mitatu ya ualimu, Hannah amefundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao wengi wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Hannah amejaliwa watoto wawili: Mary Wangui na Joseph Mbuthia ambao wamemzalia wajukuu watatu – Wayne Githinji, Wayne Kiarie na Caleb Kimani.