GWIJI WA WIKI: Hussein Kassim

GWIJI WA WIKI: Hussein Kassim

Na CHRIS ADUNGO

USHAURI si ushauri iwapo hautaleta athari chanya katika maisha ya mtu. Iwapo nasaha haimtafaa yeyote, basi nathubutu kusema kuwa huwa ni maneno shinikizi tu. Ashakum si matusi, labda niseme, hiyo huwa porojo!

Kwa yeyote anayetaka kujipa ridhaa ya moyo, basi asichoke kukikumbatia na kukipenda kwa dhati kitu hicho kimoja kinachomridhisha nafsi. Akifuate na kukihangaikia kwa jinsi yoyote iwayo ile, yaje masika au kiangazi!

Aonekane kama ambaye kapagawa kwa namna fulani. Kwanza, aanze kuzoeleka na jamaa zake wa karibu na hata rafikize kwamba kitu hicho ndiyo hewa apumuwayo kila uchao. Kisha, anasibishwe na kitu hicho kokote aendako. Kitajwapo kitu hicho popote, mabongo ya waja yawe yanapata taswira ya fulani huyo – tena na tena na tena, bila kuchoka!

Mwisho wa kwisha, atakuwa amepata mwao na mbinu ya kujipenyeza hadi waliko watu waliofaulu. Siri za kufaulu ni mbili tu – kifanye hicho ukipendacho bila ya kuchoka wala kutamauka na upanie kupata ridhaa na faraja ya moyo kila unapokifanya kitu hicho!

Huu ndio ushauri wa Bw Hussein Kassim almaarufu Bongo Pevu – mtaalamu wa masuala ya afya, mhariri, mtafsiri na mshairi anayeinukia vyema katika uandishi wa Fasihi ya Kiswahili.

MAISHA YA AWALI

Hussein alizaliwa mnamo 1994. Ndiye mwanambee katika familia ya Bw Kassim Mukanda ya wana watano – Suleiman, Mustafa, Leila na Suheila katika usanjari huo. Alilelewa na kupata masomo yake ya awali katika kijiji cha Eshiakhulo kilichoko katika eneo la Mumias Mashariki, Kaunti ya Kakamega.

Hussein alisomea katika shule mbili tofauti za upili – Mumias Boys Muslim (Kakamega) na Laiser Hill Academy (Kaunti ya Kajiado). Alijiunga baadaye na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa kwa masomo ya Shahada ya Kwanza katika taaluma ya Afya ya Jamii na akahitimu mwaka wa 2019.

Mtu wa awali kabisa kuiotesha mbegu ya mapenzi ya Kiswahili ndani yake alikuwa mwalimu Violet Vinaywa aliyemfundisha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Eshiakhulo. Wengine waliopalilia mche ule na kuwa mti maridadi ni Bi Linah Achieng na Bw Paul Byattah Nambwaya waliomchochea kwa kiwango kikubwa walipokuwa wakimpokeza malezi ya kiakademia katika shule ya msingi.

Marehemu Profesa Ken Walibora! (Roho yake ilazwe pema penye wema.) Alikuwa chanzo kikuu cha mapenzi ya Hussein kwa lugha hii ashirafu ya Kiswahili.

Itakuwa si haki kutotaja na kutambua juhudi za Bw Kassim (babaye) ambaye amemshika mkono siku zote kuhakikisha kuwa anazidi kuvipanda vidato vya mafanikio katika safari ya maisha.

Hakuwahi kuchoka wala haelekei kufanya hivyo, akiwa na matumaini kuwa mwanawe atakuja kuwa mtu wa maana sana katika jamii. Humwamini mwanawe siku zote na anazidi kumlea kwa misingi ya kumcha Mungu na kuwaheshimu watu wote – wakubwa kwa wadogo.

Bw Kassim ni miongoni mwa watu waliomshajiisha Hussein maishani, kumhimiza ajitahidi masomoni na kumwelekeza ipasavyo katika kila hatua.

MCHANGO KITAALUMA

Baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu, Hussein tayari ameshaanza kujihusisha na taaluma yake, ingawa bado hajaajiriwa. Kwa kutumia kipaji chake cha uandishi, amepiga hatua kubwa sana ya kuoanisha talanta na taaluma aliyosomea kwa kuchapisha kitabu cha mashairi ‘Diwani ya Maradhi’.

Ingawa hiki ni miongoni mwa vitabu vingi alivyoandika mnamo 2020, anajivunia sana kazi hii kwa kuwa wazo la kuiandaa lilitoka mvunguni mwa moyo wake. Anaamini kuwa kitabu hicho kitapiga hatua na kuifaa jamii pakubwa mno.

Vitabu vingine alivyoshiriki kuandika katika mwaka wa 2020 ni mikusanyiko ya hadithi fupi ‘Mapenzi ya Pesa’, ‘Shaka ya Maisha’, ‘Makovu ya Moyoni’, ‘Harusi ya Kiharusi’ na ‘Kuku Ameshinda Kura’. Bila shaka, hakuupoteza mwaka huo kama walivyolalama watu wengi duniani kutokana na janga la korona. Ilikuwa fursa yake ya kutamba, naye akaitumia vizuri sana!

Hussein amefanya na anazidi kufanya mambo makuu ili kuikuza lugha hii adhimu ya Kiswahili pamoja na fasihi yake. Mbali na uandishi wa vitabu, pia anafanya tafsiri na ufasiri (Kiingereza-Kiswahili). Umilisi wake wa lugha hizi mbili ni wa kipekee.

Mbali na kuhariri vitabu na makala kwa malipo ama kwa kujitolea tu, yeye ni huendesha masimulizi ya visa kwenye YouTube (Bongo Pevu TV).

Kwa kuwa hakufaulu kuutalii taaluma ya uanahabari, anajifunga kibwebwe kuhakikisha kuwa anafanya mazoezi katika ulingo huo kwa lengo la kuiridhisha nafsi yake.

Anaishi kwa imani kwamba mvuto na mguso wa kipekee uliomo ndani ya mrindimo wa sauti yake utakuja kuwa kitambulisho chake atakapokuwa mwanahabari – taaluma ambayo amekuwa akiiotea tangu utotoni.

Zaidi ya kuandika makala ya kuburudisha na kuelimisha kwenye kaunti ya mtandao wake wa kijamii wa Facebook (Hussayn Qassym), Hussein ni mwanablogu anayeshiriki na kuchangia mijadala mingi ya kitaaluma kupitia vipindi vya redio, runinga na kumbi za Kiswahili mitandaoni.

Anapojitahidi katika ulingo wa uandishi na kuihangaikia taaluma aliyosomea, Hussein amezamia kwa sasa masuala ya biashara ambayo humpa tonge la kila siku.

Anayajaribia maisha biasharani akingoja mlango wa heri ufunguke katika kozi aliyoisomea. Hupata pia fungu la riziki yake kwa kutafsiri katiba, nyaraka na stakabadhi za vyama na mashirika mbalimbali ya humu nchini. Uwezo wake huu umemwezesha kukidhi mengo ya mahitaji yake ya kila siku.

MAAZIMIO

Hussein anaazimia kuvikwea vidato vya uandishi na kuwa miongoni mwa watunzi stadi wa kazi za kitaaluma na bunilizi.

Anapania kuwa kielelezo na mfano wa kuigwa na vijana wenzake ili hatimaye aache jina zuri duniani – atajwe kwa uzuri kama wanavyotajwa mabingwa na mikota wa Kiswahili waliotenda wema kabla ya kufunga safari isiyo na marejeo.

JIVUNIO

Hussein anamstahi sana babaye mzazi, Bw Kassim. Humwombea dua siku zote azidi kuwapo ili aendelee kumfaa. Pia anajivunia watu wengine wa familia yake wanaomwamini siku zote kama vile Imran Hussein, Mustafa Kassim, Rashid Mohammed, Ramadhan Wesonga na Abdul Fibanda.

Pia anajivunia kuwa na marafiki adhimu wanaozidi kumfaa. Hawa ni pamoja na Sylvia Amunga, Suleiman Ofutumbo, Eunniah Mbabazi, Mturi Katana, Nyagemi Nyamwaro Mabuka, Timothy Sumba, Richard Amunga na wengineo wengi.

Hussein amekuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wengi wa wanafunzi, wanahabari na walimu ambao wametangamana naye katika warsha na makongamano mbalimbali ya kupigia chapuo Kiswahili.

Isitoshe, anajivunia kuwashika mikono baadhi ya rafikize, nao wakatia bidii na kupiga hatua kubwa maishani. Kama alivyoshikwa mkono naye akafika alipofika, amefanya juhudi kuwainua wenzake. Miongoni mwao ni Juma Patrick Kurwa, Dorcas Asianut, Emily Gatwiri na Diana Muhandachi.

You can share this post!

Nairobi: Mutura afanya mabadiliko kiasi katika serikali yake

Spika aliye mwiba kwa Trump kuongoza Congress muhula wa 4