Makala

GWIJI WA WIKI: Jacinta Nyambura

September 25th, 2019 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

CHANGAMOTO tunazozipitia mara kwa mara zinastahili kuwa jukwaa mwafaka la kutukomaza na kubadilisha mitazamo yetu kuhusu maisha.

Utakapoanza kujiamini, kukumbatia nidhamu na kujitahidi katika chochote unachokifanya, Mungu atakufungulia milango ya heri.

Mtumainie sana Mola katika kila jambo na mpe nafasi afanye kazi yake katika maisha yako kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka na rehema zote.

Amini kwamba hakuna lisilowezekana na vyovyote uwazavyo, ndoto zako zinapaswa kukuinua na kuweka kitu kipya zaidi katika maisha yako.

Kitumie kipaji chako vyema ili hatimaye kikuinue. Kipawa ni ujuzi ambao Mungu aliweka ndani yako bila ya wewe mwenyewe kugharimia chochote. Inawezekana hujui talanta yako au bado hujajishughulisha kabisa kuitambua. Fanya jambo. Anza sasa hivi!

Huu ndio ushauri wa Bi Jacinta Nyambura Thuku – mshairi shupavu na mwalimu mbobevu ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Lugha katika Shule ya Upili ya Loreto Girls Kiambu na mchungaji katika kanisa la Deliverance Church Kizito, Nairobi.

Maisha ya awali

Jacinta alizaliwa kijijini Gatunguru, katika Kaunti ya Murang’a akiwa mtoto wa tatu baina ya tisa katika familia ya Bw na Bi Gituthu Muthaa.

Alijiunga na Shule ya Msingi ya Heshima Road, Nairobi mnamo 1969 na kuufanya mtihani wa CPE mwishoni mwa 1975.

Alama nzuri alizozipata katika mtihani huo wa kitaifa zilimpa nafasi katika Shule ya Upili ya Pangani Girls, Nairobi mnamo 1976. Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (EACE) mwishoni mwa 1979 kisha akajiunga na Shule ya Upili ya Moi Forces Academy, Nairobi kwa minajili ya kusomea kiwango cha ‘A-Level’ kati ya 1980 na 1981.

Usomi na utaalamu

Mnamo 1983, Jacinta alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea taaluma ya ualimu (Kiswahili na Dini). Alifuzu mwishoni mwa 1986.

Anakiri kwamba kariha na ilhamu ya kuzamia utetezi wa Kiswahili ni zao la kutangamana na kutagusana kwa karibu sana na wahadhiri wake chuoni, hasa Bw Mugambi na Profesa Kitula King’ei.

Mwingine aliyemchochea pakubwa kuanza kukichapukia Kiswahili ni marehemu Yusuf Mutuku King’ala ambaye hadi kufariki kwake mnamo 2005, alikuwa mwandishi stadi wa Fasihi Pendwa ya Kiswahili na Naibu Mkurugenzi Mkuu aliyesimamia masuala ya akademia katika Shule ya Upili ya Starehe Boys’ Centre, Nairobi.

Baada ya kufuzu na kuhitimu, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma Jacinta kufundisha katika Shule ya Upili ya Igandene, Meru alikoamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na hata walimu wenzake. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuelekea Starehe Boys Centre & School mnamo Mei 1988.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili shuleni humo mnamo 2000 na akaushikilia wadhifa huo hadi 2008.

Msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ulimchochea Jacinta kurejea katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea shahada ya Uzamili katika Elimu na Ushauri Nasaha mnamo Septemba 2008.

Alifuzu mnamo Septemba 2010 na TSC ikamtuma katika Shule ya Upili ya Loreto Girls Kiambu. Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Lugha shuleni humo mnamo 2015. Anakiri kwamba kufaulu kwa mwanafunzi shuleni pakubwa huwa ni zao la bidii, nidhamu, imani na mtazamo wake kwa masomo na walimu wanaompokeza elimu ya darasani na maarifa au ujuzi wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili Shuleni Loreto Girls Kiambu ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaoujivunia kila mwaka matokeo ya KCSE yanapotangazwa. Baadhi ya walimu hao ni Bi Muigai, Bi Muturi, Bw Kibet na Bi Joanta ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Somo la Kiswahili.

Ilikuwa hadi 2013 ambapo Jacinta alijiunga na Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Nairobi kusomea shahada ya Uzamifu (phD) katika Elimu na Saikolojia.

Uandishi

Jacinta anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza rasmi tangu akiwa mwanafunzi wa A-Level Shuleni Moi Forces Academy, Nairobi.

Utunzi wa mashairi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani yake akiwa kitoto cha umri wa miaka saba.

Mbali na mashairi yake kumvunia tuzo za haiba kubwa, pia yalimpandisha katika majukwaa mbalimbali ya kutuzwa kwa Kiswahili. Nyingi za tungo zake zilifana sana katika tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Kwa sasa anapania kuchapisha diwani ambazo kulingana naye, zitabadilisha sura na viwango vya ufundishaji na usomaji wa mashairi katika ngazi za shule za upili na vyuo vikuu ndani na nje ya Kenya.

Jivunio

Jacinta amekuwa Mtahini wa Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC) tangu 1989.

Tajriba hiyo pana imemchochea kuandaa na kuhudhuria makongamano mengi katika sehemu mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa ya KCSE Kiswahili. Isitoshe, anajivunia kuwa mwamuzi katika kipindi ‘Sanaa ya Lugha’ kilichokuwa kikitayarishwa na kuendeshwa na Bw James Kanuri katika runinga ya KBC.

Zaidi ya kupigania makuzi ya Kiswahili kupitia vyombo vya habari, Kanuri ambaye kwa sasa ni kinara wa shirika la Huduma za Kielimu kwa Taifa (NES) anajivunia taathira kubwa katika sera na maendeleo ya Lugha, Isimu na Fasihi.

Katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu ya ualimu, Jacinta amefundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Bw Daniel Kitonga Maanzo (Mbunge wa Makueni), Bw Ngotho ambaye kwa sasa ni Naibu Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya Kenyatta-Mahiga, eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri na Marehemu Ken Odhiambo Okoth aliyekuwa Mbunge wa Kibra, Nairobi ni miongoni mwa wanafunzi wake.

Jacinta kwa sasa ni mshauri mwenye tajriba pevu katika masuala ya jamii kupitia shirika la Silver Lining lililoko katika eneo la Kahawa Sukari, Nairobi.

Aidha, yeye ni miongoni mwa Wakurugenzi Wakuu wa Power Governors Ltd (PGL), kampuni inayouza vipuri na vidhibiti-kasi vya magari jijini Nairobi. Kwa pamoja na mumewe Bw Crispus Thuku, wamejaliwa watoto watatu: Mercy, James na Monica.