Makala

GWIJI WA WIKI: Jack Otiya, mwandishi chipukizi na mwalimu wa Kiswahili

July 8th, 2020 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIZURI unachokifikiria ndicho utakachokipata. Fuata mkondo wa fikira zako!

Jipende, kipende unachokifanya na namna unavyokifanya. Usifanye jambo kwa sababu wengine walilifanya au wanalifanya. Upekee wa mtu ndio ubora wake!

Marafiki wanaweza kukujenga au kukubomoa. Teua marafiki wema wenye fikira na uwezo wa kukutoa hapa na kukufikisha pale katika safari ya ufanisi. Fanya hivyo ili ufike mbali!

Ukiona vyaelea jua vimeundwa. Mjenzi bora hujfunza ujenzi akaboreka hata zaidi. Mwandishi husoma kazi za watangulizi wake ndipo awe stadi na hodari kabisa. Huwezi kuwa mwalimu kabla ya kuwa mwanafunzi!

Huu ndio ushauri wa Bw Jack Omusugu Otiya –mwandishi chipukizi na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Bishop King’oo Okuleu, Kaunti ya Busia.

MAISHA YA WALI

Jack Otiya alizaliwa mnamo Julai 24, 1993 kijijini Kakinei, kata ndogo ya Okuleu, eneo la Teso Kaskazini, Busia. Yeye ni mzaliwa wa pili katika familia ya watoto saba wa Bw Nicodemus Otiya na Bi Goretty Otiya. Nduguze ni Faith, Daniel, Doreen, Edison, Lucas na Tobias.

Otiya alilelewa katika utamaduni uliosisitiza ulazima wa mtoto kuadhibiwa na kushauriwa na mzazi yeyote kwa kuwa jukumu la ulezi lilikuwa la jamii nzima.

Baada ya kupata elimu ya msingi shuleni Amagoro kati ya mwaka wa 2000 na 2007, alijiunga na Shule ya Upili ya Malava Boys, Kaunti ya Kakamega alikofanyia Mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE).

Alijiunga baadaye na Chuo Kikuu cha Moi (Bewa Kuu), Eldoret kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini) na akahitimu mnamo 2018.

Otiya anatambua ukubwa na upekee wa mchango wa wazazi wake waliomhangaikia katika kila hali na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali. Zaidi ya kuwa walimu wake wa awali maishani, wazazi hawa walimshajiisha sana masomoni.

“Nitakuwa mchache wa fadhila endapo sitazitambua juhudi za wazazi wangu katika kunilea na kuelekeza kila mojawapo ya hatua zangu katika safari ya maisha. Mama alikuwa msitari wa mbele kunihimiza kujitahidi darasani. Baba alinishauri mara kwa mara na alikuwa radhi kuninunulia kila kitabu nilichokihitaji.”

Otiya anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhamasishwa mno na waliokuwa walimu wake katika Shule ya Msingi ya Amagoro.

Mbali na Bi Doreen Wafula aliyependa kumpongeza na kumtuza mwanafunzi wake huyu kila alipofaulu vyema katika mtihani wa somo la Kiswahili, wengine waliomtia Otiya motisha na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichangamkia Kiswahili; ni Bi Rodah Wafula, Mwalimu Macleos Chala na Bw William Ikomol.

Mwingine aliyemchochea kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hii ni kiwanda kikuu cha maarifa, ujuzi, ajira na uvumbuzi; ni Bw Wepoh Wesah aliyemfundisha shuleni Malava Boys.

Kariha na ilhamu zaidi ilichangiwa na wahadhiri waliotangamana naye kwa karibu sana na kumpokeza malezi bora ya kiakademia katika Chuo Kikuu cha Moi. Hawa ni pamoja na Bw Keitany Kemboi na Dkt Robert Oduori.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa na Otiya kwa sasa katika Kiswahili ulichangiwa sana na tukio la yeye kufundishwa na watu ambao mbali na kubobea ajabu katika taaluma, pia waliipenda na kutawaliwa na ghera ya kuchangia makuzi ya lugha hii kwa kani na idili.

Otiya aligundua utajiri wa kipaji chake katika utangazaji akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Alikuwa na mazoea ya kuziiga sauti za wanahabari Leonard Mambo Mbotela na Khadija Ali kila walipokuwa wakitangaza taarifa au kuendesha vipindi redioni.

Isitoshe, alikuwa mpenzi kindakindaki wa kipindi ‘Ukarabati wa Lugha’ kilichokuwa kikiendeshwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah na Jack Oyoo Sylvester katika KBC Radio Taifa.

Kati ya matamanio makubwa zaidi ya Otiya hadi sasa, ni kujitosa kikamilifu katika ulingo wa uanahabari na kuwa mhariri shupavu wa Kiswahili katika mojawapo ya runinga maarufu nchini Kenya. Ualimu na uanahabari ni taaluma ambazo alivutiwa nazo tangu akiwa mtoto mdogo.

UALIMU

Akisubiri kujiunga na chuo kikuu baada ya kukamilisha mtihani wa KCSE, Otiya alipata kibarua cha kufundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Bishop King’oo Okuleu, Amagoro, Teso Kaskazini.

Nafasi hiyo ilimpa jukwaa mwafaka la kuzima kiu ya ualimu na kudhihirisha ukubwa wa uwezo alio nao na umilisi wake wa Kiswahili. Akiwa huko, aliamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

“Wanafunzi walianza kushiriki mashindano ya uigizaji, kughani mashairi katika tamasha za kitaifa za muziki na drama na kujihusisha sana na uandishi wa kazi bunilizi. Jambo hili lilibadilisha sura ya kusomwa na kufundishwa kwa masomo ya lugha, nao walimu wakapata msukumo na hamasa zaidi ya kukichapukia Kiswahili.”

UANAHABARI

Akiwa chuoni, Otiya aliwahi kuwa Afisa wa Uhusiano Mwema na Katibu Mkuu wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi (CHAKIMO) na mwanachama wa Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA).

Zaidi ya kuchangia makala na habari mbalimbali katika jarida la ‘Dafina Wiki Hii’ ambalo ni chapisho maalumu la CHAKIMO kila Jumatatu na Ijumaa, Otiya alichangia makuzi ya Kiswahili chuoni Moi kwa njia tofauti.

Alishiriki uendeshaji wa kipindi ‘Dafina ya Lugha’ katika idhaa ya MU FM (103.9) kila wiki na akashirikiana na wanafunzi wenzake kuandaa michezo mbalimbali ya kuigiza pamoja na kuandika ‘Miongozo’ ya vitabu teule vya fasihi vilivyokuwa vikitahiniwa katika mitihani ya KCSE Kiswahili.

Alikuwa pia mstari wa mbele kuwaongoza wanachama wenzake wa CHAKIMO kuzuru shule mbalimbali za Kaunti ya Uasin Gishu kwa nia ya kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa.

Otiya kwa sasa ni mchanganuzi wa masuala ya elimu katika kitengo cha ‘Uketo wa Lugha’ cha kipindi ‘Dira ya Watoto’ ambacho hupeperushwa hewani kila Jumamosi asubuhi na kituo cha redio Emuria FM (101.3) katika eneo la Teso Kusini, Busia.

UANDISHI

Otiya anaamini kwamba safari yake katika ulingo wa uandishi ilianza rasmi akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Nyingi za insha alizozitunga zilimvunia tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha. Alitunga pia idadi kubwa ya mashairi yaliyofana katika mashindano ya viwango mbalimbali. Kwa sasa anatazamia kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanafunzi wake katika ulingo wa uandishi.

Kampuni ya Bestar Publishers ilimchapishia Otiya kitabu ‘JUALEO’ mnamo Aprili 2019. Anaandaa sasa miswada ya riwaya na kitabu cha mazoezi na marudio ya Kiswahili kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa, mhadhiri wa chuo kikuu na mmiliki wa maktaba ya Kiswahili katika eneo la Teso Kaskazini, Otiya anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inawatawala walimu wenzake ndani na nje ya Kaunti ya Busia.

Anajivunia kuhudhuria na kuwasilisha makala ya kitaaluma katika makongamano mbalimbali kwa nia ya kupigia chapuo lugha ya Kiswahili.