Makala

GWIJI WA WIKI: Jennifer Wachira

March 18th, 2020 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

CHANGAMOTO tunazozipitia mara kwa mara zinastahili kuwa jukwaa mwafaka la kutukomaza na kubadilisha mitazamo yetu kuhusu maisha.

Utakapoanza kujiamini, kukumbatia nidhamu na kujitahidi katika chochote unachokifanya, Mungu atakufungulia milango ya heri.

Mtumainie sana Muumba wako katika kila jambo na mpe nafasi afanye kazi yake katika maisha yako kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka na rehema zote.

Amini kwamba hakuna lisilowezekana na vyovyote uwazavyo, ndoto zako zinapaswa kukuinua na kuweka kitu kipya zaidi katika maisha yako. Kitumie kipaji chako vyema ili hatimaye kikuinue.

Kila hatua unayoipiga, hata iwe ndogo kiasi gani, ni fursa njema ya kusonga mbele maishani. Fanya maamuzi sahihi na uanze kuupangia vyema muda wako. Kufaulu katika jambo lolote kunahitaji mtu kuwa na maono na kutenda yaliyo mema bila ya kudhamiria malipo.

Kuanzia leo, anza kushindana na wakati badala ya binadamu wenzako. Jikubali jinsi ulivyo na usijilinganishe na mtu mwingine. Pania siku zote kutembea na wanaojua ili wakuelezekeze ipasavyo.

Huu ndio ushauri wa Bi Jennifer Wachira – mlezi wa vipaji, mwandishi mahiri, mtunzi shupavu wa mitihani, mshairi stadi, mshauri nasaha na mwalimu mbobevu ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Alexis Ruchu Girls, Kaunti ya Murang’a.

MAISHA YA AWALI

Jennifer alizaliwa zaidi ya miaka 50 iliyopita katika kijiji cha Thuita, eneo la Gatanga, Kaunti ya Murang’a akiwa mwanambee katika familia ya watoto sita wa Bw Humphrey Wachira na marehemu Bi Beatrice Wachira.

Alijiunga na Shule ya Msingi ya Nyaga, Thuita mnamo 1968 na kuufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la saba (CPE) mwishoni mwa 1975. Alama nzuri alizozipata katika mtihani huo zilimpa nafasi katika Shule ya Upili ya Kamahuha Girls, eneo la Sabasaba, Murang’a mnamo 1976.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Kidato cha Nne (EACE) mwishoni mwa 1979 kisha akajiunga na Shule ya Upili ya Senior Chief Koinange, Kiambu alikosomea kiwango cha ‘A-Levels’ kati ya 1980 na 1981.

Mnamo 1983, Jennifer alijiunga na Chuo cha Walimu cha Kagumo, Nyeri. Alifuzu mwishoni mwa 1985. Anakiri kwamba kariha na ilhamu ya kuzamia utetezi wa Kiswahili ni zao la kutangamana na kutagusana kwa karibu sana na walimu pamoja na wahadhiri wake.

Mbali na Bw Gitimu aliyempokeza malezi bora zaidi ya kiakademia shuleni Kamahuha Girls, mwingine aliyepanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichapukia Kiswahili ni Bw Kinuthia aliyemnoa vilivyo katika Shule ya Upili ya Senior Chief Koinange.

Bw Kinuthia alimchochea sana mwanafunzi wake huyu baada ya kutambua kipaji chake cha uanahabari na ukubwa wa kiwango chake cha umilisi wa Kiswahili. Alimhimiza mara kwa mara azidi kukichangamkia Kiswahili ili aje kuwa mtangazaji wa habari runingani au mhariri wa gazeti la Taifa Leo katika siku za halafu.

UALIMU

Baada ya kuhitimu mnamo 1985, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma Jennifer kufundisha katika Shule ya Upili ya Gatanga Girls, Murang’a alikoamsha ari ya kuthaminiwa kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na hata walimu wenzake.

Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka mitano kabla ya kuelekea Kihumbuini Girls, Gatanga mnamo Mei 1991.

“Wanafunzi walianza kuchangamkia sana mashindano ya uigizaji na kughani mashairi katika tamasha za kitaifa za muziki na drama. Jambo hili lilibadilisha pakubwa sura ya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili shuleni Kihumbuini Girls,” anasema.

Akiwa Mlezi wa Chama cha Kiswahili shuleni humo, alitambua na kukuza vipaji vya wanafunzi anuwai; hasa katika utunzi wa kazi za kubuni.

Kupitia tamasha za kitaifa za muziki na drama, Jennifer alikuwa mstari wa mbele kuwaelekeza wanafunzi wake kutunga mashairi ya kila sampuli na kushiriki michezo ya kuigiza iliyofichua utajiri wa talanta zao katika ulingo wa sanaa. Kwa miaka si haba, wanafunzi wake walitamba sana michezoni huku wakifikia kiwango cha kitaifa kila waliposhiriki tamasha za muziki na drama.

Mnamo Januari 2014 Jennifer alihamia katika Shule ya Upili ya Ruchu Girls na akateuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili.

Anakiri kwamba kufaulu kwa mwanafunzi yeyote huwa ni zao la bidii, nidhamu, imani na mtazamo wake kuhusu masomo na walimu wanaompokeza elimu ya darasani na ujuzi wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni Ruchu Girls ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaojivunia kila mwaka matokeo ya KCSE yanapotolewa. Baadhi ya walimu hao ni Bi Abigael Njenga, Bi Bena Kamau, Bw Joseph Kamotho, Bw Kinoti, Bi Alfa Nyabicha, Bw Jacob na Bi Alice Waithaka.

UANDISHI

Jennifer anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza rasmi miaka 10 iliyopita. Utunzi wa mashairi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani yake akiwa na umri mdogo.

Insha alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kubwa na kumpandisha katika majukwaa mbalimbali ya kutukuzwa kwa Kiswahili. Nyingi za tungo zake zilifana sana katika tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Mnamo 2010, Jennifer alipata kazi ya kutathmini na kuhariri baadhi ya vitabu vya Longhorn Publishers, Nairobi.

Mwaka uo huo, Longhorn Publishers ilimchapishia kitabu ‘Marudio Hima Hima ya Kiswahili Kidato cha Nne’. Jennifer kwa sasa ni mtunzi maarufu wa mitihani ya Karatasi ya Pili ya Kiswahili (Ufahamu, Ufupisho, Lugha, Isimujamii) katika kaunti ndogo ya Kandara, Murang’a.

JIVUNIO

Jennifer amekuwa mtunzi wa mitihani ya Kiswahili inayochapishwa katika misururu ya vitabu vya High Flyer Series KCSE tangu 2014. Tajriba hiyo pana imemchochea kuandaa na kuhudhuria makongamano mengi katika sehemu mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kila sampuli.

Katika kipindi cha zaidi ya miongo mitatu ya ualimu, Jennifer amefundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili. Miongoni mwao ni Jane Magu (Nairobi) na Ann Kihiu (TSC) aliowatandikia zulia zuri la Kiswahili katika Shule ya Upili ya Gatanga Girls.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, Jennifer hujishughulisha na kilimo cha parachichi na ufugaji wa kuku, nguruwe na ng’ombe wa maziwa katika eneo a Gatanga. Yeye pia ni mshauri nasaha wa masuala ya jamii katika Chuo cha Maranatha, Thika, Kaunti ya Kiambu.

Kwa pamoja na mumewe Bw Joseph Njenga, wamejaliwa watoto wawili: Joan Wairimu na Ram Riitho. Wajukuu wao ni Grace Wambui na Ian Thiga.