Makala

GWIJI WA WIKI: Jessicah Rebeccah Mkwalafu

June 26th, 2019 5 min read

Na CHRIS ADUNGO

UALIMU ni zaidi ya kazi!

Kipimo halisi cha upevu wa mwalimu bora ni upana wa uelewa wake kuhusu jambo hili.

Thamani ya mwalimu huboreshwa na wanafunzi wake. Ukubwa wa thamani hiyo, ambayo hutarajiwa kuwa kiini cha sifa zake, hushinda ubora wa pesa na vitu vyote vingine vya msimu!

Pania sana kutenda wema siku zote kwa sababu hifadhi ya jina zuri katika fikra za wanafunzi wako ndiyo malipo bora zaidi kwa mwalimu.

Upeo wa mafanikio ya mtu hutegemea pakubwa juhudi zake, nidhamu, uvumilivu na imani aliyonayo kuhusu jambo.

Hakuna kitu kinachoridhisha zaidi nafsi ya mwenye kutenda jambo kuliko kuwafanyia watu kazi nzuri itakayodumu katika kumbukumbu zao kutokana na jinsi itakavyoboresha maisha yao na kubadilisha mikondo ya fikra zao.

Mwamini sana Mungu wako ili akufungulie milango ya heri. Mtumainie katika kila jambo na mpe nafasi afanye kazi yake katika maisha yako kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka na rehema zote.

Huu ndio ushauri wa Bi Jessicah Rebeccah Mkwalafu – mshauri nasaha, mlezi wa vipaji, mshairi shupavu na mwandishi chipukizi wa Fasihi ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Teresa Mukunga, Kakamega.

Maisha ya awali

Jessicah alizaliwa mnamo 1993 mjini Eldoret, Uasin Gishu akiwa mtoto wa nne kati ya watano katika familia ya Bi Jennifer na Bw John Mkwalafu.

Akiwa na umri wa miaka mitano, alijiunga na chekechea ya Bondeni mjini Eldoret alikoanzia safari yake ya elimu.

Miaka miwili baadaye, familia yake iligura na kuelekea katika sehemu ya mashinani ya Nangili, Kaunti ya Kakamega alipojiunga na Shule ya Msingi ya Nangili. Alisomea pale hadi alipoufanya mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane, KCPE.

Anasema hatamsahau kamwe aliyekuwa mwalimu wake, Bi Susan Mbuti ambaye aliionea lugha ya Kiingereza tija na fahari tele. Jessicah anamtambua pia Bi Kedogo aliyekuwa mwalimu wake wa somo la Kiswahili kuanzia darasa la sita hadi la nane shuleni Nangili.

Anasema mwalimu huyo alizungumza kwa lafudhi ya Pwani, jambo lililowafanya wanafunzi wake kutaka sana kuzungumza kama yeye katika jitihada za kumuiga.

Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, Jessicah aliandika insha zilizotuzwa alama nyingi na kusifiwa zaidi kila baada ya kutolewa kwa matokeo ya mijarabu.

Mengi ya mashairi aliyoyatunga yalimzolea sifa na kumvunia umaarufu miongoni mwa mwenzake. Aidha, ufundi mkubwa katika tungo alizozisuka ni upekee uliompandisha kwenye majukwaa ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha sana katika ulingo wa Kiswahili.

Kipendacho roho ni dawa! Matokeo ya mtihani wa KCSE yalipotolewa, Jessicah alikuwa amefaulu vyema zaidi katika somo la Kiswahili. Alama nzuri alizozipata katika mtihani mzima zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya Wasichana ya Moi Girls’ Nangili.

Akiwa kule, alikutana na Bi Milah Njoroge aliyemwelekeza vilivyo katika uandishi wa Insha bora za Kiswahili na hata kuchochea zaidi kipaji chake cha utunzi wa mashairi kwa ushirikiano na mwalimu Alfred Alfuma. Kila wakati, Jessicah alituzwa pakubwa kutokana na ubora wa matokeo yake katika somo la Kiswahili.

Baada ya kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE), alijiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya Bewa la Eldoret kusomea ualimu (Kiswahili na Dini).

Alifuzu mnamo 2016. Anatoa shukrani zake kwa mhadhiri Angola ambaye alimpokeza malezi bora zaidi ya kiakademia chuoni.

Mbali na kupanda ndani yake mbegu za mapenzi ya dhati kwa taaluma ya ualimu, Bw Angola pia alimshajiisha zaidi masomoni. Alimwaminisha kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hiyo ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi.Hivyo, alimtaka azamie zaidi taaluma mbalimbali za Kiswahili ili aje kuwa msomi na mtaalamu wa Kiswahili katika siku za halafu.

Ualimu

Jessicah aliwahi kufundisha Kiswahili na somo la Sayansi Kimu katika Shule ya St Elizabeth Langas, Eldoret akiwa bado mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mt Kenya mnamo 2014.

Aliwahi pia kufundisha katika Shule ya Upili ya Kahoya Mixed, Eldoret wakati alipokuwa akisubiri kufuzu mnamo 2016 baada ya kuhitimisha masomo yake kwa minajili ya Shahada ya Kwanza katika taaluma ya ualimu.

Akiwa Kahoya, alikuwa Mkuu wa Idara ya Lugha.

Zaidi ya kuamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake, aliwaelekeza wanafunzi vyema na kuwachochea wengi wao kutaka kukisomea Kiswahili hata baada ya kukamilisha elimu ya sekondari. Mwanahabari Fuzia Hassan alikuwa miongoni mwa wanafunzi wake waliokithamini na kukichapukia zaidi Kiswahili alaa kulihali.

Mnamo 2018, Jessicah alijiunga na Shule ya Upili ya St Teresa Mukunga, Kakamega kufundisha Kiswahili na Somo la Dini.

Mbali na kuwaelekeza wanafunzi wake katika utunzi wa mashairi kwa minajili ya tamasha za kitaifa za muziki na drama, pia anawashirikisha katika mashindano ya Uandishi wa Insha katika gazeti la Taifa Leo.

Wengi wa wanafunzi wake kwa sasa wameanza kutambua utajiri mkubwa wa vipaji vyao katika utunzi wa kazi bunilizi na huchangamkia sana fursa za kukariri na kughani mashairi ya mwalimu wao Bi Jessicah kwa lengo la kuwatumbuiza wageni nyakati za hafla mbalimbali shuleni St Teresa Mukunga.

Jessicah anaazimia kuwa malenga shupavu na mwandishi arifu wa riwaya pendwa za Kiswahili.

Mapenzi ya kutunga mashairi na kuyaghani mbele ya hadhira ni fani iliyojikuza ndani yake tangu akiwa tineja. Amekuwa akitunga mashairi mengi kwa matumaini ya kuchapishiwa diwani ambayo anaamini itabadilisha pakubwa sura ya kufundishwa kwa somo la Ushairi katika shule za upili za ndani na nje ya Kenya.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto zake za kujiendeleza kitaaluma, Jessicah anajivunia mafao mengi kutokana na Kiswahili ambacho kimempa fursa ya kufundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Kikubwa zaidi kinachomridhisha nafsi ni tija ya kuwaona wengi wa wanafunzi wake wakitaka sana kuiga mfano wake na kujitosa katika ulingo wa Kiswahili kwa lengo la kuwa ama walimu maarufu au wanahabari mashuhuri.Anaungama kwamba kufaulu kwa mwanafunzi yeyote hutegemea pakubwa mtazamo wake kwa masomo anayofundishwa na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Lugha shuleni St Teresa Mukunga, ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaojivunia kwa sasa katika somo la Kiswahili.

Uzoefu alionao katika ufundishaji wa Kiswahili umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwashauri, kuwaelekeza na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Anaeleza kuwa katika kazi yake ya ualimu, yeye huwapa wanafunzi kipaumbele, huwaweka sana moyoni na kuwaombea heri siku zote.

Jessicah hutumia muda wake mwingi kuwa pamoja na wanafunzi kwa imani kwamba matokeo bora hupatikana iwapo mwalimu atasalia kuwa karibu na wanafunzi wake ili hatimaye awaondolee wasiwasi kwa kujibu maswali yao yote kadri wanavyojifanyia mazoezi na marudio.

Yeye hutumia mbinu mbalimbali za kufundishia ili kunasa usikivu wa wanafunzi kila wakati na kuwaamshia msukumo wa kulipenda somo.

Kila afundishapo, yeye hupenda sana kutumia mifano ambayo wanafunzi wanaifahamu ili waelewe na kukumbuka kwa haraka mengi ya masuala wanayoyajadili.

Anasisitiza kwamba ni muhimu kwa mwalimu kuyaelewa mahitaji na matamanio ya kila mmojawapo wa wanafunzi wake na kuyashughulikia kwa njia mwafaka zaidi.

Anawahimiza walimu kutowahadithia wanafunzi kuhusu changamoto mbalimbali za maisha, bali wawe mfano bora siku zote ili wanafunzi wao wahamasike zaidi kuwaiga kutokana na mengi ya mafanikio yao.

Jessicah anatambua upekee wa mchango wa mumewe Bw Washington Asusa Rurache katika kumhimiza pakubwa kuchangia makuzi ya Kiswahili.

Kwa pamoja, wamejaliwa mtoto wa kiume: Duren Johnson Masitsa.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, wanajishughulisha pia na ukulima wa mboga ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya familia yao.