Makala

GWIJI WA WIKI: Job Mokaya

March 20th, 2019 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

WEKA Mungu mbele. Heshimu viongozi wote; wakubwa kwa wadogo wako kazini.

Tia bidii kazini, kuwa na nidhamu na ujiamini.

Kuwa wa mwisho kutoka darasani. Kuwa wa mwisho kutoka shuleni.

Kuwa wa mwisho kutoka ofisini. Kuwa pia wa kwanza kuingia katika sehemu hizi siku zote.

Tumia muda mwingi kufanya kazi kwa kujituma.

Fanya mambo tofauti na wengine. Usifanye kama wengine.

Ukiwezeshwa, tumia rasilimali yako binafsi kufanikisha mambo fulani iwapo ile uliyopewa haitoshi.

Siku moja utalipwa; na utalipwa vizuri sana! Ukifanya mazuri, utalipwa mema. Ukitenda mabaya utalipwa maovu.

Kwa ufupi, chochote unachokifanya, kiwe kizuri au kibaya; hatimaye utalipwa! Mwisho, jiweke vyema. Kula vizuri. Tunza mwili na ulinde afya yako.

Huu ndio ushauri wa Bw Job Nyangena Mokaya.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Mimi ni mpenzi kindakindaki wa Kiswahili, mhariri, mwandishi, mwalimu na mhakiki. Kwa sasa ni Meneja wa Uhariri katika Shirika la Uchapishaji la East African Educational Publishers (EAEP).

Aidha, nimewahi kuwa Mhariri Mwandamizi wa Kiswahili katika Shirika la Oxford University Press (OUP) pamoja na kuwa mhariri wa jumla katika Shirika la Uchapishaji la Storymoja Africa.

Kabla ya kujiunga na tasnia ya uchapishaji, niliwahi kufundisha somo la Kiswahili katika Shule za Upili za St Michaels Nyarongi, Tarang’anya Boys High, Pesoda Complex (zote za Migori), Nyabomo High na Mwencha Academy Kitale (zote za Trans-Nzoia).

Ulizaliwa, ukalelewa na kusomea wapi?

Nilizaliwa katika Kaunti ya Trans-Nzoia yapata miaka 34 iliyopita.

Nilianzia safari yangu ya elimu katika Shule ya Msingi ya Nyabomo hadi darasa la saba kisha nikajiunga na Shule ya Msingi ya Lungai, Saboti nilikofanyia mtihani wa KCPE.

Nilifaulu vyema na kupata nafasi katika Shule ya Upili ya Nyagesenda Adventist, Kisii. Nilijiunga baadaye na Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kwa ufadhili wa serikali mnamo 2005.

Nilisomea Shahada ya Kwanza katika BA Kiswahili na kufuzu mnamo 2008.

Pia nina Stashahada ya Uanahabari kutoka East African School of Media Studies.

Sasa hivi ninapania kufanya Shahada ya Uzamili katika masuala ya Upangaji na Usimamizi wa Miradi (Project Planning and Management).

Nani aliyekuchochea zaidi kukipenda Kiswahili?

Babangu mzazi. Akiwa mwalimu wa shule ya msingi mjini Kitale, alipenda sana kurejea nyumbani akiwa na vitabu vya hadithi za kila sampuli.

Jambo hili liliniweka katika ulazima wa kusoma kazi nyingi za Kiswahili katika umri huo wangu mdogo. Nilisoma Hekaya za Abunuwasi na kitabu Mabepari wa Venisi kilichowahi kutahiniwa katika mitihani ya KCSE Kiswahili nikiwa mwanafunzi wa darasa la tatu!

Ilhamu na kariha zaidi ilichangiwa na marafiki wangu James Oriango na Vincent Ayienda niliokuwa nikishindana nao darasani kusoma Ufahamu katika vitabu vya kiada tukiwa wanafunzi wa shule ya msingi.

Natambua pia ukubwa wa mchango wa Evans Njaga Ochogo, Miriam Ombui na Dennis Manwa waliokuwa wanafunzi wenzangu katika shule ya upili. Nilikuwa nikishindana nao kuandika Insha bora zilizosomwa na mwalimu mara kwa mara darasani.

Umahiri wangu katika ulumbi uliwahi kunipa fursa adhimu ya kukishiriki kilichokuwa kipindi maarufu cha Idhaa ya KBC, Maswali kwa Wanafunzi kikiongozwa na marehemu Billy Omala.

Mbali na wanahabari Elvis Ondiek, Patrick Injendi, Ferdinand Mwongela na Nicholas Anyuor, wengine walionitia hamasa ya kukichangamkia Kiswahili kwa dhati ni Stephen Musamali na Chris Adungo niliosoma nao chuoni huku tukiwa pia vinara wa Chama cha Kiswahili cha Moi (CHAKIMO).

Job Mokaya. Picha/ Maktaba

Ni upi mchango wako katika makuzi ya Kiswahili hadi kufikia sasa?

Kubwa zaidi ninalojivunia ni kuamsha ari ya kuthaminiwa sana kwa somo la Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wangu nilipokuwa mwalimu katika Shule ya Upili ya St Michaels Nyarongi, eneo la Suna, Kaunti ya Migori.

Wanafunzi niliowafundisha shuleni humo waliongoza katika iliyokuwa Wilaya ya Migori kwenye mtihani wa KCSE Kiswahili mnamo 2009.

Kazi ya uhariri imenipa fursa maridhawa ya kushirikiana na wenzangu kuchapisha baadhi ya vitabu ambavyo kwa sasa vinapendwa zaidi na idadi kubwa ya wasomaji ndani na nje ya taifa la Kenya.

Ulianza lini safari yako ya uandishi?

Nikiwa mwanafunzi wa shule ya sekondari, hasa kutokana na mazoea yangu ya kuandika insha na shajara. Nilipohitimisha masomo ya chuo kikuu, nilikusanya shajara hizo zote na kuongezea ubunifu kiasi; kisha kuunda muswada niliouwasilishia wahariri wa EAEP.

Badala ya kuchapishiwa muswada huo, nilipokezwa kazi ya uhariri katika kampuni hiyo!

Safari ya Mjini ni kitabu changu cha kwanza kilichofyatuliwa na EAEP mnamo 2013. Hiki ni kitabu cha wanafunzi wa darasa la sita ambacho kinasomwa sana katika shule za umma nchini Uganda.

Kitabu changu cha pili ni Score More KCSE Kiswahili kilichochapishwa na kampuni ya Storymoja Africa mnamo 2014. Nilishirikiana na wenzangu watatu kukiandika.

Nimechangia pia kuchapishwa kwa Kamusi Teule Toleo la Kwanza na Pili (EAEP 2013, 2019).

Zaidi ya uhariri, unajishughulisha na nini kingine?

Huwa ninaandaa, kuhudhuria na kuwasilisha makala mbalimbali katika makongamano ya Kiswahili (kitaifa na kimataifa) kuanzia yale ya walimu na wanafunzi wa shule za msingi, shule za upili, vyuo vya walimu na vyuo vikuu. Mimi pia ni mwandishi na mchanganuzi mpevu wa masuala ya soka katika vyombo vya habari. Japo ya halafu ninamwachia Mungu, ninapania sana kuwa mkulima hodari katika siku za usoni.

Ni kipi cha pekee unachokifanya tofauti na wenzako kitaaluma?

Mungu kamuumba kila mtu kwa namna tofauti. Kila mja ana uwezo na upekee wake. Hatuwezi kabisa kulingana kwa ubora. Kikubwa kinachonikuza maishani na kitaaluma ni mazoea ya kujisaka upya mara kwa mara na kukimakinikia vilivyo kila kitu ninachokishughulikia.

Umewahi kutambuliwa na kutuzwa kutokana na mapenzi yako kwa Kiswahili?

Nimepokea tuzo nyingi kiasi cha haja tangu nikiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, upili na chuo kikuu. Nimetambuliwa si haba katika majukwaa tele ya kutolewa kwa tuzo za Kiswahili tangu nilipoanza kufundisha na hata nilipojitosa kabisa katika ulingo wa uhariri.

Unajivunia nini kikubwa katika taaluma yako?

Taaluma imenikuza na kunifanya nilivyo leo. Inaniwezesha kuyakidhi mengi ya mahitaji yangu binafsi na ya familia yangu. Inanipa kidogo nikipatacho. Nacho hicho huwa ninawamegea wengine wachache wasiojiweza katika jamii.