Makala

GWIJI WA WIKI: Kapia Wa Makapia

October 9th, 2019 5 min read

Na CHRIS ADUNGO

HATUA ya mwanzo kabisa katika safari yoyote ya ufanisi ni kufahamu kile unachokitaka; kujielewa wewe ni nani na kutambua mahali unakokwenda.

Katika dunia hii, kuna watu wasio na maono.

Lengo lao ni kuwazimia wengine ndoto zinazotawala mawazo yao. Jiepushe kabisa na kundi la watu wa aina hiyo.

Usilie wala kukata tamaa usipofaulu.

Pania sana kutenda mema na ukipende kwa dhati hicho unachokifanya. Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta.

Yaruhusu mawazo yako yatawaliwe na fikira za ushindi.

Vumilia ugumu wa leo kwa matumaini kwamba kile unachokihangaikia kitatimia kesho. Kubali kuchumia juani na kuchanika kwa mpini. Utakulia kivulini na hutakufa njaa. Usizoee kufuata njia za mkato unaposaka mafanikio. Njia za mkato hukata!

Kumbuka ufanisi unaopatikana kwa upesi huisha upesi. Angalia sana thamani ya mambo unayoyatenda. Fanya maamuzi sahihi na pangia vyema jinsi unavyotumia muda wako.

Huu ndio ushauri wa Bw Abdallah Makapia almaarufu Kapia Wa Makapia.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Jina langu kamili ni Abdallah Makapia. Wenzangu nyumbani huniita Kapia Wa Makapia kumaanisha mtu anayechukua kitu na kukiunda upya ili kiwe bora na kizuri zaidi. Kwa maana hiyo, ukiona vyaelea jua vimeundwa! Kapia ni muundaji! Kwa pamoja na familia na baadhi ya marafiki zangu, tumeunda Wakfu wa Kapia Wa Makapia kwa azimio la kutoa mchango wetu kwa jamii tulikozaliwa katika eneo la Mumias, Kaunti ya Kakamega.

Tufafanulie kuhusu maisha yako ya awali

Nilizaliwa mnamo Agosti 17, 1983, katika kijiji cha Bumanyi, kata ya Nabongo, eneobunge la Mumias Magharibi, Kakamega. Asilimia kubwa ya makuzi yangu ni ujombani katika kijiji cha Buchifi-Bukaya, Kakamega.

Nilisomea katika Shule ya Msingi ya Mtakatifu Stephano

Mwitoti na kuibuka mwanafunzi bora zaidi katika mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) mnamo 1997. Nilijiunga na Shule ya Upili ya Wavulana ya Kakamega na nikafanya mtihani wa kitaifa wa kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2001. Nashukuru Jalali kwamba nilifaulu kujiunga na Chuo Kikuu cha Maseno nilikohitimu kwa shahada ya Usimamizi wa Biashara mnamo 2007. Nilijiendeleza baadaye kitaaluma kwa kusomea shahada ya uzamili katika masuala ya Usimamizi wa Biashara.

Ni nini cha pekee ambacho kwa sasa unajishughulisha nacho?

Kwa muda wa zaidi ya miaka kumi sasa, nimekuwa nikijihusisha na masuala ya ujenzi wa jamii na taifa kwa jumla. Mbali na kuchangia malezi ya elimu, nimekuwa nikipania sana kuinua viwango vya michezo mashinani, kuboresha sekta ya kilimo, kuimarisha muziki na sanaa na kuzishughulikia changamoto za ajira kwa vijana kupitia Wakfu wa Kapia Wa Makapia.

Nimekuwa mstari wa mbele kupigania upatikanaji wa maji safi kwa wanajamii, ustawi wa misitu kupitia upandaji wa miti na kuhakikisha kwamba kuna usawa katika ugavi wa mbegu na pembejeo nyinginezo zinazotolewa kwa wakulima nyakati za misimu ya upanzi. Niliunda Wakfu wa Kapia Wa Makapia kwa madhumuni mengine ya kutambua, kukuza na kulea vipaji mbalimbali miongoni mwa vijana chipukizi ili wapate ujuzi wa kukabiliana vilivyo na janga la umaskini na changamoto za mara kwa mara katika maisha ya kawaida ya binadamu.

Ni upi mchango wako katika sekta ya elimu?

Nimefaulu kuzitembelea shule mbalimbali kwa nia ya kuwahamasisha wanafunzi kuhusu umuhimu wa masomo katika maisha yao ya sasa na ya siku za usoni. Nimekuwa pia nikishiriki nyingi za sherehe za kutuzwa kwa wanafunzi baada kutolewa kwa matokeo yao ya mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE. Hili ni jambo ambalo nimekuwa nikilifanya tangu mwaka wa 1998 hasa baada ya mimi pia kuzawidiwa kutokana na ubora wa matokeo yangu katika KCPE 1997.

Tangu wakati huo, nimekuwa nikihisi ulazima wa kuwa kielelezo chema kwa wanajamii wenzangu; na kuwatuza wanafunzi wachapakazi shuleni ni jukumu ambalo nimejitolea kutekeleza katika siku zote za maisha yangu. Nimekuwa majuzi katika Shule ya Msingi ya Ihonje katika eneo la Otiato-Etenje, Mumias Magharibi kwa sherehe za kutuzwa kwa wanafunzi waliotia fora katika mitihani yao ya awali.

Hafla za sampuli hii hunipa majukwaa maridhawa ya kuwazungumzia vijana kuhusu manufaa ya kujitahidi masomoni na umuhimu wa kujiepusha na mimba za mapema, matumizi ya mihadarati na dawa za kulevya.

Panapo afya, uzima na uhai, tutafanikisha sherehe za haiba kubwa za kutolewa kwa tuzo hizi mwakani; na tutaleta pamoja shule zote katika eneo pana la Mumias. Chini ya Wakfu wa Kapia Wa Makapia, nimekuwa nikiwatuza na kuwapa motisha walimu wanaowaongoza wanafunzi wao kusajili matokeo bora mitihanini kwa njia tofauti tofauti.

Ni vipi unavyolishughulikia tatizo la ajira kwa vijana?

Nimejitahidi kuwafungulia baadhi ya vinyozi chipukizi jumla ya vibanda 50 vya kunyolea na maduka 20 ya wao kuendeshea biashara ya ususi.

Mbali na kuwanunulia wengine vyombo vya kuzishughulikia kazi hizi, nimejitahidi pia kuwalipia karo ili wasome zaidi na kuongeza ujuzi wao kitaluuma.

Pia nimetoa ng’ombe wa maziwa kwa familia kadhaa ili kuwapa wanajamii uwezo wa kujiajiri katika sekta ya kilimo na ufugaji wa kisasa.

Kila msimu wa upanzi, Wakfu wa Kapia Wa Makapia pia hutoa mbegu na pembejeo nyinginezo na kuandaa semina za kuwahamasisha wakulima kuhusu njia bora na faafu zaidi za kuboresha mazao ya kilimo chao. Tunapanga kuongeza idadi ya wanaonufaika kutokana na miradi hii kutoka watu 1,000 kwa sasa hadi 5,000 mwaka ujao. Tuko radhi kushirikiana na wadau wengine kulipigia chapuo suala hili.

Ni upi mchango wako katika suala la ukuzaji wa talanta na sanaa mashinani?

Mnamo Aprili 2018, tuliandaa mashindano ya kuwania taji la Miss Mumias. Kwa sasa, Wakfu wa Kapia Wa Makapia unaandaa mashindano yatakayoshirikisha kwaya za makanisa na shule, vikundi vya kitamaduni na kaswida misikitini. Mashindano haya yataandaliwa mjini Mumias. Timu kutoka Zanzibar, Tanzania, Uganda na Afrika Kusini tayari zimethibitisha kushiriki.

Ni kipi cha pekee unachokifanya tofauti na wenzako kitaaluma?

Nimekuwa nikipania sana kuwainua wenzangu katika jamii na kuyaboresha maisha yao. Huwa tija na fahari tele kwangu kuwaona wale niliowalea na kuwakuza katika nyanja tofauti tofauti wakifanikiwa kujiajiri na kupiga hatua za kimaendeleo kama vile wasanii MC Malosa na MC Lejah.

Baadhi ya wale ambao nimewainua sana kibiashara ni Mustapha (Time X Kinyozi, Misheni), Kassim (Home Life Kinyozi, Mumias Posta), Kandia (Hot Sound, Kamkon), Kevin (Executive Kinyozi Shibale), Nyendwe (Wisdom Kinyozi, Buhuru), Patrick (Home Ground Kinyozi, Khungema), Kennedy (Maisha Kinyozi, Otiato), Ochieng (K’Ogalo Kinyozi, Emukhuwa), Joseph (Upendo Kinyozi, Lukongo), Philip (Soft Cut Kinyozi, Imanga) miongoni mwa wengine.

Je, ni nini na nani aliyekuchochea kujitwika jukumu hili la kuhudumia jamii?

Mimi ni mfuasi sugu wa mwendazake Mama Winnie Madikizela-Mandela (1936-2018) ambaye katika uhai wake, alijitolea sabili kuitumikia jamii wakati wa vita vya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

Licha ya kuwa mumewe marehemu Nelson Mandela (1918-2013) alikuwa korokoroni kwa kipindi cha miaka 27, mama huyu hakutamauka maishani. Badala yake, alisalia kuwa shujaa na akaendeleza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi huku akitetea na kuwahudumia watu wake walioumia chini ya serikali dhalimu ya Wazungu. Haya ni kati ya matendo ya Winnie Madikizela ambayo hunitia moyo wa kuwa kiongozi kwa nia ya kuihudumia jamii licha ya changamoto za kila sampuli.

Unapozungumzia uongozi, je, una azma ya kujitosa katika ulingo wa siasa?

Kufikia sasa nimekuwa nikihimizwa sana na watu mbalimbali kutoka maeneo ya Mumias niwatumikie katika ngazi nyingine tofauti kwa kuwa wameona kipaji cha uongozi na moyo wa kutoa ndani yangu. Kutoa ni moyo, si utajiri!

Mpaka mwisho wa mwezi uliopita, nimekuwa nikipokea ujumbe maalumu wa wazee kutoka Mumias, wakiongozwa na Mama Mhe Hannah Wanalo, Mhe Obwaka, Fahim Daffy, Mhe Rocky Omwendo, Mhe Athman, Mhe Mungoma Charles Shikanda, Mhe Bilal, Mzee Bakari Osanya, Bw Kennedy Murunga, Mwalimu Isaac Mukoya na wengineo, wakiniomba kugombea kiti cha ubunge katika eneo la Mumias Magharibi ufikapo mwaka wa 2022. Ingawa hivyo, lengo langu kubwa kwa sasa ni kutoa mwongozo wa kuigwa kwa wakazi wapendwa wa Mumias Magharibi na sehemu nyingine za taifa hili. Pia nisisitize kuwa kwa sasa mikono yangu imejaa majukumu mbalimbali ninayoyatekeleza chini ya Wakfu wa Kapia Wa Makapia.

Itakuwa vyema nikiwapa viongozi waliochaguliwa awali nafasi ya kutimiza ahadi walizotoa wakati walipokuwa wakiomba kupigiwa kura katika uchaguzi uliopita. Wakati wa siasa utakuja. Mungu akijalia, tukifika hapo. Na tutafanya maamuzi ya busara kwa heshima ya wananchi ambao wana mamlaka ya kuamua ni nani atakayekuwa kiongozi wao.

Mbali na kutumikia jamii, ni kipi kingine unachokifanya kwa sasa?

Mimi ni mfanyabiashara na meneja wa benki moja ya hapa nchini Kenya.

Unajivunia nini kikubwa katika maisha yako?

Najivunia kuwa mwasisi wa Wakfu wa Kapia Wa Makapia. Hakuna kinachonipa raha zaidi kuliko kushuhudia idadi kubwa ya watu wakifanikiwa chini ya wakfu huu. Zaidi ya kuwa mfano mwema na kielelezo bora kwa wanajamii wenzangu, najivunia familia yangu ambayo ninaistahi sana. Nimeoa na mimi ni mzazi.