GWIJI WA WIKI: Kennedy Wandera

GWIJI WA WIKI: Kennedy Wandera

NA CHRIS ADUNGO

KWAMBA angekuja kuwa miongoni mwa wanahabari wanaostahiwa kimataifa na sauti yake irindime na kupasua mawimbi nyuma ya mabomba; ni jambo lililokuwa muhali kufikirika katika maisha ya awali ya Kennedy Wandera.

Ingawa matamanio yake ya tangu utotoni yalikuwa kusomea uanasheria na kuwa wakili, ndoto ya kujitosa katika ulingo wa uanahabari ilianza pia kumtambalia katika umri mdogo.

“Niliingia shuleni nikifahamu thamani ya Kiswahili na umuhimu wa redio. Nilikuwa shabiki mkubwa wa vipindi vilivyokuwa vikipeperushwa na idhaa mbalimbali za kimataifa. Mazoea hayo yalinitandikia zulia zuri la lugha na kunipa utashi wa kuwa mwanahabari,” anasema.

Baada ya kutambua kipaji chake cha utangazaji, Wandera alitia azma ya kukipalilia. Walimu walimpa fursa za kughani mashairi darasani na kusoma habari za matukio mbalimbali gwarideni kila Ijumaa. Majukwaa hayo adhimu yalinoa kipawa chake cha ulumbi na akawa maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake.

Wandera alizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Bukeki, eneobunge la Budalangi, Kaunti ya Busia. Ndiye wa mwisho katika familia ya watoto watatu wa marehemu Bw Boniface Okumu na marehemu Bi Grace Anyango.

Alisomea katika shule ya msingi ya Musoma, Budalangi kabla ya kujiunga na shule ya upili ya St Mary’s Mundika, Busia (2004-2005) kisha shule ya upili ya Shilce, Nairobi (2006-2007). Baada ya kukamilisha KCSE, alijiunga na chuo kimoja jijini Nairobi kusomea masuala ya Teknolojia ya Habari.

Mnamo 2010, Wandera alielekea jijini Juba, Sudan Kusini kuwa sehemu ya watekelezaji wa programu za maendeleo zilizoendeshwa na shirika moja la Uingereza kwa pamoja na Kanisa la Angilikana la Episcopal Church of The Sudan, Dayosisi ya Ibba.

Akiwa huko, alifanya kazi na Shirika la Kimataifa la Utangazaji la Ujerumani, Deutsche Welle (DW), na akategemewa sana kuripoti matukio ya kujitenga kwa Sudan Kusini kutoka Sudan mnamo 2011.

Alirejea Kenya mnamo 2012 na akajiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea shahada ya Uanahabari. Alipokea mafunzo ya nyanjani katika runinga ya Citizen kabla ya kuajiriwa na Sauti ya Amerika (VOA) mnamo 2016 kuwa mtangazaji wa habari na mtayarishaji wa makala ya vipindi vya redio na runinga.

Mwanahabari wa VOA, Kennedy Wandera, wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO

Wandera kwa sasa anasomea shahada ya uzamili katika tasnia ya uanahabari. Amekuwa Mwenyekiti wa Muungano wa Waandishi wa Habari wanaoripotia Idhaa za Kimataifa barani Afrika (FPAA) tangu 2019. FPAA ina afisi jijini Nairobi (Kenya), Johannesburg (Afrika Kusini), Yaounde (Cameroon), Abuja (Nigeria), London (Uingereza) na New York (Amerika).

Kubwa zaidi katika maazimio ya Wandera ni kusomea uanasheria na kuwa miongoni mwa wadau wakuu wenye uwezo wa kutoa maamuzi muhimu katika tasnia ya uanahabari.

Anapania pia kuwa mmliki wa kituo cha mafunzo ya uanahabari chenye malengo mahsusi ya kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanahabari chipukizi watakaoangazia masuala ya maendeleo ya jamii.

“Kufaulu katika uanahabari kunahitaji mtu kuwa na msukumo, ari na mshawasha wa kushiriki kikamilifu mafunzo yatakayomkuza kitaaluma. Ukipata mwanya wa kufanya kazi, jitume ipasavyo na uzoee kukamilisha majukumu yako mapema. Usimuige yeyote. Thibitisha habari kabla ya kuzipeperusha au kuchapisha. Ipo hadhira inayokutegemea. Usiipotoshe,” anashauri.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iwaachie maseneta kazi ya kufuatilia...

VYAMA: Chama cha Uanahabari Ukanda wa Magharibi ya Kenya...

T L