Makala

GWIJI WA WIKI: Lilian Gathoni

October 7th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

JIFUNZE kutokata tamaa, kuwa mtu mwenye msimamo, jiamini na upende kushindana na wakati.

Ujasiri wa kukabiliana na changamoto mbalimbali na imani kuwa hakuna lisilowezekana ni siri kubwa ya kufanikiwa maishani na katika kitaaluma.

Kufaulu katika jambo lolote ni zao la jitihada, nidhamu, imani na stahamala.

Upo mahali ulipo kwa sababu kuna mtu aliyetambua ukubwa wa uwezo wako na akakuchochea kufikia kilele cha ndoto zako.

Uwajibikaji, ari ya kufanya kazi kwa kujituma pamoja na moyo wa kushirikiana na watu wengine katika mambo unayoyafanya, ni sifa muhimu na za lazima kwa mtu kuwa nazo ili afanikiwe. Mtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga na usonge mbele kwa mwendo na kasi yako.

Huu ndio ushauri wa Bi Lilian Gathoni Wambui –mwanafasihi chipukizi, mhariri na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili na somo la Dini katika Shule ya Upili ya Royal Star, eneo la Ongata Rongai, Kaunti ya Kajiado.

MAISHA YA AWALI

Gathoni alizaliwa katika kijiji cha Iruri, eneo la Kamacharia, Kaunti ya Murang’a akiwa mwanambee katika familia ya watoto wanne wa Bi Agnes Wambui. Nduguze Gathoni ni Glorious Chelang’at, Davis Kiplang’at na Alex Kipkoech.

Gathoni alilelewa katika utamaduni uliosisitiza ulazima wa mtoto kuadhibiwa na kushauriwa na mzazi yeyote kwa kuwa jukumu la ulezi lilikuwa la jamii nzima.

Baada ya kupata elimu ya msingi shuleni Iruri kati ya 2002 na 2010, alijiunga na Shule ya Upili ya Kiria-ini Girls, Murang’a mnamo 2011 na akahitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa 2014.

Gathoni alisomea ualimu (Kiswahili na Dini) katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kati ya Septemba 2015 na Disemba 2019.

Zaidi ya nyanya na mama mzazi kuwa walimu wake wa awali maishani, wawili hawa walimshajiisha sana Gathoni na kumhimiza ajitahidi masomoni.

Anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhamasishwa na aliyekuwa mwalimu wake wa Kiswahili katika shule ya msingi, Bi Mwangi. Kariha na ilhamu zaidi ilichangiwa na wahadhiri waliotangamana naye kwa karibu sana, kumpokeza malezi bora ya kiakademia na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichangamkia Kiswahili akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Zaidi ya Bw Stephen Wamalwa, wengine waliomchochea pakubwa kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote ni Dkt Hamisi Babusa, Dkt Miriam Osore, Dkt Timothy Arege, Dkt Joseph Gakuo, Mwalimu Mudhune na marehemu Mwalimu Kamunde.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa sasa na Gathoni katika Kiswahili umechangiwa pakubwa na tukio la yeye kufundishwa na watu ambao ni wabobevu na wapenzi kindakindaki wa lugha hii.

UALIMU

Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Gathoni alianza kufundisha katika Shule ya Upili ya Kenswed iliyoko katika eneo la Ngong, Kaunti ya Kajiado. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kati ya Mei na Agosti 2019 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Royal Star.

Gathoni anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote hutegemea mtazamo wake kwa somo husika na kwa mwalimu anayemfundisha darasani.

UANDISHI

Gathoni anaamini kwamba safari yake ya uandishi ilianza alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Ni katika kipindi hicho ambapo nyingi za insha alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kubwa kutoka kwa walimu wake wa Kiswahili.

Aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Kiria-ini Girls na wadhifa huo ukachangia kunoa kipaji chake cha ulumbi na kuinua kiwango chake cha umilisi wa lugha.

Chini ya uelekezi wa Mwalimu Daniels, Gathoni alishiriki mashindano mengi ya kutoa hotuba na kujizolea tuzo za haiba.

Kati ya waandishi waliomwamshia ari ya kutunga kazi za kibunifu kwa Kiswahili ni Bw Dominic Maina Oigo, Bw Wafula wa Wafula, Bw Djibril Adam, Bi Pauline Kea Kyovi, Bw Almasi Ndangili, Dkt Babusa na marehemu Profesa Ken Walibora.

Tangu 2017, Gathoni ameandika idadi kubwa ya miswada ambayo kwa sasa ipo katika hatua za mwishomwisho za uhariri katika mashirika mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu.

Kampuni ya Bustani Language Solutions (BLS) Nairobi ilimchapishia Gathoni hadithi ‘Kamari ya Maisha’ katika diwani ya ‘Mama Amerudi na Hadithi Nyingine’ mnamo Juni 2019.

Hadithi zake ‘Huba la Dhati’ na ‘Umdhaniaye Siye’ zilichapishwa na kampuni ya Bestar Publishers Nairobi katika mkusanyiko wa ‘Kitovu cha Shibiri na Hadithi Nyingine’ mnamo Disemba 2019.

Gathoni ndiye mwandishi wa hadithi ‘Vita vya Nafsi’ katika mkusanyiko wa ‘Hakimu wa Kifo na Hadithi Nyingine’ uliofyatuliwa na kampuni ya Bestar Publishers mnamo Februari 2020.

Gathoni ameshiriki pia mradi wa uandishi wa ‘Tusome Kenya’ kupitia kampuni ya Queenex Publishers Nairobi iliyomtolea kitabu ‘Mwati na Swale na Hadithi Nyingine’ mnamo Agosti 2020.

Gathoni kwa sasa anatafsiri riwaya ‘Son of Fate’ ya mwandishi John Kiriamiti hadi ‘Hatima Yangu’. Kazi hiyo itafyatuliwa na kampuni ya East African Educational Publishers (EAEP).

UHARIRI

Uhariri ulianza kujikuza ndani ya Gathoni tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya upili. Alikuwa mwepesi wa kuwakosoa wenzake waliovuruga lugha kila Jumatano ambayo ilikuwa ‘Siku ya Kiswahili’ shuleni mwao.

Kufikia sasa, amehariri makala mbalimbali ya kitaaluma, vitabu vya kiada na antholojia za hadithi fupi ambazo zimechapishwa na kampuni mbalimbali nchini Kenya.

Diwani yake ya kwanza kuihariri ni ‘Mama Amerudi na Hadithi Nyingine’ kabla ya kushirikiana baadaye na John Wanyonyi Wanyama kuipiga msasa diwani ‘Hakimu wa Kifo na Hadithi Nyingine’.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa, mwandishi maarufu na mhadhiri wa chuo kikuu, Gathoni anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala waandishi wengi chipukizi ambao wametangamana naye katika makongamano mbalimbali ya Kiswahili.