Makala

GWIJI WA WIKI: Mohammed Ghassani

February 20th, 2019 3 min read

MOHAMMED GHASSANI

Na CHRIS ADUNGO

WAZEE wamestaafu na sasa vijana wamechukua hatamu. Nawakumbuka sana wengi wa wazee hao kwa maana wakianza kutangaza taarifa ya habari, ilikuwa ni lazima usikilize iishe yote. Walikuwa na mvuto wa haiba kubwa na weledi wa hali ya juu katika tasnia ya uanahabari.

Sijui kama tutawahi kuwapata watangazaji kama hao ambao mbali na kuipenda sana kazi yao, walijitolea sabili kukitetea Kiswahili kwa hali na mali. Ben Wazir, Othman Miraji, Ramadhan Ally, David Wakati, Abdul Ngalawa, Jacob Tesha, Manase Lukungu, Oumilkheir Hamidou na marehemu Abdul Wajih Sheikh ni baadhi tu.

Labda aliyebaki kwa sasa ni Mohammed Khelef Ghassani – mwalimu na mwandishi wa hadithi ‘Maeko’ katika diwani ya Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine. Ni kama walivyokuwa akina Hassan Gwai, Makame Abdallah, Khamis Shaban, Salim Mbonde na Charles Hillary Martin katika ulingo wa utangazaji wa soka katika ujana wao!

Mwandishi wa Fasihi ya Kiswahili na mwanahabari wa DW, Mohammed Khelef Ghassani (kulia) akiwa kazini. Picha/Chris Adungo

Nasaha
Mara nyingine tunatahiniwa na Mola wetu ili tuibuke kwenye kesho yetu tukiwa bora zaidi kuliko jana yetu, na hatimaye mbele yake tuwe na daraja la juu zaidi kuliko wengine. Tusikimwe na mitihani.

Tuombe bega tu la kuibebea na vifua vya kuimezea. Lengo la mwendo ni kusonga mbele, lakini busara ya kwenda ni kupima baina ya mguu ukanyagapo na mahala mwendaji aendapo.

Akiegemea kimoja kati yao, safari haiwi. Iwapo mwendaji ataangalia tu aendako bila ya kutazama akanyagapo, atajikwaa, ajichome miba, ajikate kwa magaye, aanguke na safari isiwe! Na iwapo atatazama tu akanyagapo bila ya kuangalia aendako, atakuwa hafiki mahala, atapotea njia, azunguke papo kwa papo!

Maisha ya awali
Ghassani alizaliwa mnamo 1977 katika kijiji cha Kinazini, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini, Kisiwani Pemba. Alilelewa na baba yake mzazi katika kijiji cha Mchangani, alikohudhuria Madrassa.

Alianza rasmi safari yake ya elimu katika Wilaya ya Wete kisha akahitimu masomo ya Darasa la 10 katika Shule ya Msingi ya Pandani-Pemba, kabla ya kujiunga na Shule ya Utaani, Wete kwa elimu ya Darasa la 11 na 12.

Mnamo 1993, alijiunga na Shule ya Upili ya Fidel Castro, eneo la Vitongoji katika Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini kwa minajili ya elimu ya Kidato cha Tano na Sita. Alihitimu mwishoni mwa 1994, mwaka mmoja kabla ya babaye aliyemhimiza pakubwa siku zote kuaga dunia.

Ingawa tukio hilo lilimyumbisha pakubwa maishani, Ghassani alijiunga na Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) ambayo ilianzishwa nchini Zanzibar mnamo 1979 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili.

TAKILUKI ambayo inafanya kazi chini ya udhamini wa Wizara ya Elimu ya Zanzibar imepania kuwafundisha wageni Kiswahili, kufanya utafiti kuhusu lahaja mbalimbali na Fasihi Simulizi ya Kiswahili pamoja na kutoa mafunzo ya lugha za kigeni kwa watu mbalimbali. Mbali na kukusanya na kuchambua Fasihi Simulizi ya Visiwa vya Unguja na Pemba, TAKILUKI pia hutoa mafunzo na masomo ya Kiswahili kwa watumishi wa Serikali ya Zanzibar, viongozi mbalimbali na wageni ili kukuza ujuzi na umilisi wao wa lugha.
Ghassani aliondoka TAKILUKI mnamo 1998 na kuelekea mjini Dodoma kufanya kazi ya upigaji picha katika kampuni ya Bossphoto Fast.
Alihudumu huko kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea Kisiwani Unguja kujiunga na TAKILUKI kwa ajili ya kusomea Diploma katika Lugha na taaluma ya Ualimu. Alihitimu mnamo 2001 na kupata ajira katika Shirika la Utalii la Fisherman Tours & Travel Ltd.
Haja ya kubadilisha mkondo wa maisha yake pamoja na msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ni kati ya mambo yaliyomchochea kuelekea Dar es Salaam mnamo Julai 2006 kusomea Shahada ya Kwanza katika Habari na Mawasiliano ya Umma. Alifuzu mwishoni mwa 2009. Wakati akiwa Fisherman Tours, alianza kuchangia makala katika gazeti la Dira nchini Zanzibar mnamo 2002 hadi chapisho hilo lilipopigwa marufuku mwishoni mwa 2004 kwa sababu za kisiasa.
Mnamo 2003, Ghassani aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Habari wa Civic United Front (CUF) ambacho ni chama cha upinzani katika ulingo wa siasa nchini Zanzibar. Alihudumu katika wadhifa huo kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea TAKILUKI alikoajiriwa kuwa Mhadhiri Msaidizi wa Kijerumani katika Chuo Kikuu cha Taifa, Zanzibar (SUZA). Mbali na kufundisha kozi za Kijerumani, aliaminiwa pia kuwaelekeza baadhi ya wanafunzi wa Diploma katika Ushairi na Nadharia za Fasihi ya Kiswahili.
Alihudumu chuoni SUZA hadi mwanzoni mwa 2009 ambapo alijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kusomea Shahada ya Uzamili katika taaluma ya Tafsiri. Mnamo Septemba 2010, alitua Ujerumani alikopokezwa mafunzo ya miezi sita kuhusu utangazaji wa habari katika Kituo cha Deutsche Welle (DW) ambacho hupeperusha vipindi na matangazo mbalimbali kwa zaidi ya lugha 30.
Kituo hicho kilichoasisiwa mnamo Mei 3, 1953 kwa sasa kina makao makuu jijini Bonn, Ujerumani. Ghassani aliaminiwa kuwa mhariri na mtangazaji wa habari za Kiswahili za DW Sauti ya Ujerumani mnamo Februari 2011, nafasi ambayo anaishikilia hadi kufikia sasa. Anakiri kwamba waliomchochea pakubwa kujitosa katika ulingo wa uanahabari ni Godwin Gondwe ambaye ni mtangazaji maarufu wa redio na runinga nchini Tanzania, Ali Saleh (BBC), Ali Salim (DW) na aliyekuwa mtangazaji mahiri wa DW, Othman Miraji.

Uandishi
Ghassani alitambua upekee wa kipaji chake katika uchoraji na uandishi tangu akiwa mwanafunzi wa darasa la tano. Katika umri huo mdogo, alianza kutunga hadithi fupi za kusisimua pamoja na mashairi yenye kusifia uzalendo na uhuru kutokana na athari za kazi za waandishi Elvis Msiba na marehemu Ben Mtobwa.
Sawa na watunzi wengi wa fasihi, anaungama kwamba uandishi una nguvu ya ajabu na uwezo mkubwa katika kuelimisha, kuadilisha na kumkutanisha mtunzi na watu wa aina mbalimbali kama zilivyo taaluma za uanahabari na ualimu.
Anajivunia kuchapishiwa vitabu Andamo: Msafiri Safarini, Siwachi Kusema: Uhuru U Kifungoni, Kalamu ya Mapinduzi: Mapambano Yanaendelea, Machozi Yamenishiya na N’na Kwetu: Sauti ya Mgeni Ugenini ambacho kilimpatia Tuzo ya Fasihi ya Afrika kwa Kiswahili iliyotolewa na Mabati-Cornell mnamo 2015.