Makala

GWIJI WA WIKI: Musa Mirobi

July 10th, 2019 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

UKITAKA kuvua, vua na wavuvi; si wavivu.

Hakuna zuri litakalokufikia bila ya kudhurika.

Kujishaua si njia mwafaka ya kumshukuru Mungu anapoamua kukukweza katika ngazi ya mafanikio.

Unapokuwa kileleni, usisahau ulikotoka.

Vyovyote vile uwavyo, jinsi utakavyokuwa kesho ni matokeo ya jinsi unavyoamini leo kuhusu hiyo kesho yako.

Kuna idadi kubwa ya watu ambao kwa sasa wanajivunia mafao ya Kiswahili ulimwenguni. Siri ya mafanikio yao imekuwa ni kufuata misukumo ya ndani ya nafsi zao hadi ndoto zao zikatimia.

Kwa hivyo, lenga kuwa bora katika chochote unachoteua kukishughulikia. Kwa kuwa Mola ndiye mwelekezi wa hatua zote tunazozipiga maishani, inatujuzu kumweka mbele siku zote.

Kufaulu katika jambo lolote kunahitaji mtu kuwa na maono na kutenda mema bila ya kudhamiria malipo.

Nidhamu, bidii na imani ni kati ya mambo mengine yanayochangia mafanikio ya binadamu.

Anza kushindana na wakati badala ya binadamu wenzako.

Huu ndio ushauri wa Bw Musa Mirobi, mwandishi na mwalimu wa Kiswahili ambaye kwa sasa ni Meneja katika Shule ya Msingi ya HEZTA Preparatory, Kaunti ya Nyandarua.

Maisha ya Awali

Bw Mirobi alizaliwa katika kijiji cha Kahuho, eneo la Ol Moran, Kaunti ya Laikipia akiwa mwana wa tatu katika familia ya watoto 12 wa marehemu Bi Flora Wanjira na Bw Gabriel Mwangi ambaye kwa sasa ni mkulima maarufu katika eneo la Laikipia Magharibi.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Kahuho, Laikipia Magharibi alikosomea hadi darasa la sita kabla ya kuhamia Shule ya Msingi ya Murera-Njau, Nyandarua.

Aliufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) mwaka 1992.

Ingawa alama nzuri alizozipata zilimpa fursa ya kujiunga na Shule ya Upili ya Kagumo Boys, Nyeri uchechefu wa karo ulimweka katika ulazima wa kusomea katika Shule ya Upili ya Wanjohi, Nyandarua kati ya 1993 na 1996.

Nusura kitumbua chake cha elimu kiingie mchanga baada ya babu yake, aliyekuwa akimhimiza pakubwa masomoni, kuaga dunia mnamo 1994.

Kifo cha babuye Mirobi kilitokea miaka miwili tu baada ya mamaye mzazi kutangulia mbele za haki.

Mirobi alijipata akitumwa nyumbani karibu kila uchao kutafuta karo ambayo aghalabu haikuwa ndani ya uwezo wa baba yake mzazi kuimudu.

Badala ya kutamauka, changamoto na masaibu yote aliyoyapitia yalimpa moyo zaidi wa kujikaza kisabuni darasani na kutolegeza kamba kabisa katika safari ya elimu na maisha.

Ilimjuzu mara si haba kujihimu, kujihini na kujikusuru katika hali zote ili kudumisha uhai wa ndoto zake za kuwa ama mwalimu mashuhuri au mwanahabari shupavu katika siku za halafu.

Ualimu

Mnamo 1998, Mirobi alijiunga na Chuo cha Walimu cha Murang’a.

Alihitimu mwishoni mwa 1999. Kabla ya kujitosa rasmi katika ulingo wa ukufunzi, alikabiliana na misukosuko na mapito mengi ya kutamausha. Kwa wakati fulani, alilazimika kufanya vibarua vya kuwaosha nguruwe na kuchimba misingi ya majengo mbalimbali katika eneo la Makuyu, Kaunti ya Murang’a.

Baada ya kupata nauli iliyomwezesha kuondoka Makuyu, alianza kufundisha Kiingereza katika Shule ya Msingi ya Dayspring, Nyandarua mwishoni mwa 1999.

Ilikuwa hadi 2002 ambapo alianza kukichapukia Kiswahili kwa hali na mali baada ya kukutana na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah katika mojawapo ya makongamano ya Kiswahili yaliyoandaliwa hotelini Tewan, Ol Kalou, Nyandarua.

“Guru alitambua upekee wa kipaji changu na kuchochea pakubwa ilhamu ya kukichangamkia Kiswahili ndani yangu. Alikifanya Kiswahili kianze kunibishia milango kwa lazima. Kwa sasa kimepata makao salama na ya kudumu zaidi ndani ya moyo wangu baada ya mimi kukifungulia madirisha yote na kuinyoosha mikono yangu miwili kukipokea,” anasema Mirobi.

Baada ya kufundisha Kiswahili kwa muhula mmoja pekee, mwalimu Mirobi aliamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa lugha hiyo miongoni mwa mwanafunzi na walimu wenzake shuleni Dayspring.

Upekee katika mbinu za ufundishaji wake ulichangia matokeo ya Kiswahili kuimarikazaidi katika mitihani ya KCPE kiasi kwamba wanafunzi wake waliwahi kuibuka wa kwanza katika iliyokuwa Wilaya ya Nyandarua.

Ufanisi huo ulimfanya kuanza kualikwa kukipigia chapuo Kiswahili kupitia makongomano yaliyompa majukwaa ya kufundisha, kushauri, kuwahamasisha na kuwaelekeza walimu pamoja na wanafunzi katika shule mbalimbali za msingi ndani na nje ya Kaunti ya Nyandarua kuhusu njia mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa ya KCPE.

Baada ya kuhudumu shuleni Dayspring kwa miaka sita, Mirobi alihamia Shule ya Msingi ya HETZA Preparatory mnamo 2005.

Alifundisha huko Kiswahili kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kutua katika Shule ya Msingi ya Danjose iliyoko Ruiru, Kaunti ya Kiambu mwishoni mwa 2006. Alihudumu huko kwa mwongo mmoja kabla ya kurejea HETZA alikoaminiwa wadhifa wa Umeneja mnamo 2016.

Mbali na majukumu mengi ya uongozi, Mirobi bado anafundisha Kiswahili shuleni HEZTA. Mojawapo ya mashairi aliyoyatunga limewapa wanafunzi wake fursa ya kushiriki tamasha za kitaifa za muziki na drama zitakazoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Kabarak, Kaunti ya Nakuru kuanzia Agosti 6, 2019.

Kituo cha Wasta

Kipindi ‘Ukarabati wa Lugha’ kilichokuwa kikiendeshwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah katika KBC Idhaa ya Taifa ndicho kilichochochea na kuuwasha moto wa azma ya Mirobi katika ufundishaji na uandishi wa vitabu vya Kiswahili. Wallah Bin Wallah alimtuza mara kwa

mara kutokana na upekee wa mchango wake kila alipoyajibu maswali kwa ufasaha mkubwa kipindi hicho kilipokuwa kikiendeshwa.

Kwa mara si chache, Mirobi alialikwa na Wallah Bin Wallah katika studio za KBC Nairobi mnamo 2005.

Mwalimu huyu mfia-lugha alisomea Stashahada ya Kiswahili katika WASTA Kituo cha Kiswahili Mufti kati ya 2008 na 2009.

Kituo hiki kilichopo eneo la Matasia, Ngong kinamilikiwa na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah – mwalimu maarufu, mwandishi mashuhuri na Doyen wa Kiswahili hapa Afrika Mashariki.

Kituo hiki ambacho hutambua na kuwatuza wapenzi na watetezi wa Kiswahili kila mwaka, kiliasisiwa kwa madhumuni ya kufundisha, kulea, kukuza na kueneza Kiswahili mufti miongoni mwa watumiaji wa lugha hii.

Uandishi wa hisani

‘Utamu wa Insha’ ni kitabu ambacho Mirobi alikiandika alipokuwa mwalimu katika Shule ya Msingi ya Danjose, Ruiru.

Kazi hiyo ilichapishwa na kampuni ya Frajopa, Nairobi mnamo 2011.

Akiamini kuwa Mungu humbariki zaidi anayejitolea kusaidia kwa nia safi, Mirobi amepania kutumia mrabaha wote utokanao na mauzo ya kitabu hicho kuwasomesha wanafunzi wanaotokea katika familia zisizojiweza kifedha katika Kaunti ya Nyandarua.

Kwa sasa anayadhamini masomo ya Monica Wanjiku (mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Upili ya Huruma, Ol Kalou) na aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Starehe Boys Centre, George Kiruthe ambaye kwa sasa anasomea katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Mirobi pia alikuwa mdhamini wa wanafunzi Joseph Mwangi (Shule ya Upili ya Sipili, Kaunti ya Laikipia) na aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Ol Moran, Samuel Mwaniki ambaye kwa sasa anasomea katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Jivunio

Kwa pamoja na mkewe Bi Catherine Wangui, wamejaliwa watoto wawili wa kiume: Gabriel Mwangi anayejiandaa kujiunga na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro, Samuel Mwangi ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa darasa la tano shuleni HEZTA Preparatory na Flora Wanjira.

Bw Hosea Kimotho (Chuo Kikuu cha Nairobi), Bw Alex Njuguna (Mombasa) na Dkt Justus Muchemi (Tanzania) ni miongoni mwa wanafunzi ambao Mirobi anajivunia sana kuwakuza masomoni na kuwahimiza kitaaluma.