Makala

GWIJI WA WIKI: Mwalimu Namanda

February 12th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

MAAMUZI yoyote unayoyafanya maishani ni zao la agano kati ya nafsi na mawazo yako mwenyewe.

Watu wengine hujikana na kutamauka kwa kuamini kwamba wapo walio bora zaidi kuliko wao. Jiamini, jikubali na ukatae maisha ya kujihukumu. Anayeongozwa na imani, akakumbatia nidhamu na kutawaliwa na stahamala mwishowe hufaulu!

Unapoanza kujilinganisha na watu wengine; matokeo yake ni kwamba utaanza kujidharau, kujuta, kusononeka na kujiona asiyefaa au asiyeweza kabisa kufanya jambo lolote. Jitume kwa sababu uzembe ni adui ya ufanisi; na ujifunze kwa kuwa elimu ni bahari.

Usilipe tatizo heshima, staha wala hadhi yoyote. Muone Mungu kuwa mkubwa zaidi kuliko matatizo na changamoto zote zinazokukabili. Watu wengine wanapohesabu idadi ya matatizo yaliyowatokea maishani, wewe endelea kuhesabu baraka zako!

Huu ndio ushauri wa Mwalimu Namanda – mwandishi chipukizi na mlezi wa vipaji ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Moi Kabarak, Nakuru.

Maisha ya awali

Namanda alizaliwa mnamo 1987 katika eneo la Lukume, Kaunti ya Kakamega akiwa mwanambee katika familia ya watoto sita wa Bi Eunice na Bw Julius Namanda.

Alipata elimu ya awali katika Shule ya Msingi ya Lukume alikofanyia mtihani wa KCPE mnamo 2004 kisha akajiunga na Shule ya Upili ya St Paul’s Emulakha, Kakamega mwanzoni mwa 2005. Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) shuleni humo mwishoni mwa 2008.

Anaungama kuwa aliyemshajiisha kujitahidi masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni Bw Tom Nyerere ambaye pia alimtia hamasa ya kusomea taaluma ya ualimu.

Namanda anatambua pia ukubwa na upekee wa mchango wa Bw Atibu Bakari katika kumwelekeza na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali. Aliyemtandikia zulia zuri katika jitihada za kukichapukia Kiswahili kwa ghera na idili, ni aliyekuwa mwalimu wake katika Shule ya Msingi ya Lukume, marehemu Ibrahim Abdallah.

Ilikuwa hadi Mei 2010 ambapo Namanda alijiunga na Chuo cha Walimu cha Meshad, Kakamega na akafuzu Julai 2012. Anakiri kwamba ilhamu ya kuzamia utetezi wa Kiswahili akiwa chuoni ni zao la kutangamana kwa karibu sana na wahadhiri wake, hasa Bw Wafula na Bw Kombo waliomtanguliza vyema katika kozi za Isimu na Fasihi ya Kiswahili.

Mbali na kupanda na kuotesha mbegu za mapenzi ya dhati kwa Kiswahili ndani ya Namanda, wawili hawa walimpokeza mwanafunzi wao huyo malezi bora zaidi ya kiakademia.

Wengine waliomchochea Namanda kwa imani kwamba Kiswahili kina uwezo wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hii ni kiwanda kikubwa cha maarifa, ajira na uvumbuzi; ni Bw Ashindu na Bw Ann Mundia waliomnoa vilivyo katika Shule ya Upili ya St Paul’s Emulakha.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa na Namanda kwa sasa katika ulingo wa Kiswahili ulichangiwa pakubwa na tukio la yeye kufundishwa na watu ambao mbali na kubobea ajabu katika taaluma, pia waliipenda na kutawaliwa na kariha ya kuipigia chapuo lugha hii.

Ualimu

Namanda alijitosa katika ulingo huu pindi alipohitimisha masomo yake ya shule ya sekondari. Alifundisha katika Shule ya Upili ya Lukume kati ya 2008 na 2010 kabla ya kujiunga na Chuo cha Walimu cha Meshad.

Baada ya kuhitimu ualimu, alipata ajira katika Shule ya Msingi ya Nabongo, Kaunti ya Kakamega. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi cha muhula mmoja pekee kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Fesbeth Academy, Kakamega alikofundisha hadi Disemba 2012.

Akiwa huko, aliteuliwa kuwa Katibu wa Idara ya Kiswahili na akaamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na hata walimu wenzake.

Namanda alihamia katika Shule ya Msingi ya Kakamega Hill mnamo Januari 2013 na kuaminiwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili. Alifundisha huko kwa miaka mitatu kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Moi Kabarak mnamo Mei 2016. Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili shuleni humo mwanzoni mwa Januari 2017.

Namanda anashikilia kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote hutegemea mtazamo wake kwa somo husika na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni Moi Kabarak ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaoujivunia kila mwaka matokeo ya KCPE yanapotolewa.

Uandishi

Namanda anaamini kwamba uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani yake tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Nyingi za insha bora alizozitunga zilimvunia tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha mno. Kwa mara si haba, tungo zake zilimpandisha katika majukwaa ya kila sampuli ya makuzi ya Kiswahili.

Mnamo 2013 alichapishiwa hadithi ‘Sungura Mjanja’ kabla ya kufyatua hadithi ‘Mbweha Mweusi’ mwaka mmoja baadaye.

Alishirikiana na Mwalimu Masika, Bw Otieno Mjomba na Bw Zadock Amakoye kuandaa kitabu ‘Fumbuo la Msamiati’ kilichochapishwa na Fumbuo Publishers mnamo 2016.

Kwa sasa, anashirikiana na walimu wengine kutoka sehemu mbalimbali za humu nchini kutunga mitihani ya Kiswahili kwa wanafunzi wa darasa la sita hadi la nane.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa, mhadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu kisha Mbunge wa eneo la Malava mwaka 2032 majaliwa, Namanda anajivunia kuandaa na kuhudhuria makongamano mengi kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili, kuwaelekeza, kuwashauri na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCPE.

Amekuwa mtahini wa Baraza la Mitihani ya Kenya (KNEC) tangu mwaka wa 2016.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, Namanda hujishughulisha pia na kilimo cha miwa katika Kaunti ya Kakamega.

Anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Kwa pamoja na mkewe Bi Lydia Mukhulu, wamejaliwa watoto watatu: Gloria Namanda, Gift Namanda na Elvins Namanda.