Makala

GWIJI WA WIKI: Mwanakombo Abdulrahman kutoka shule ya msingi ya Kongowea

September 15th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

UALIMU ni wito. Tuwapende watoto ndipo tuuone ufalme wa Mungu. Dumisha urafiki na watoto, usidharau sauti zao na tuzidi kuwaombea kila mara ili nao watimize ndoto zao za maisha.

Huu ni ushauri wa Bi Mwanakombo Abdulrahman ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili, Kiingereza na somo la Dini ya Kiislamu (IRE) katika Shule ya Msingi ya Kongowea, Kaunti ya Mombasa.

“Nimekuwa mwalimu kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita. Hii ni kazi ninayojivunia kufanya na ambayo nachangamkia kwa kani na idili. Mwalimu ana mchango mkubwa katika kuchochea hamu ya wanafunzi wake kupenda masomo,” anatanguliza kwa kuhimiza walimu kuionea kazi yao fahari tele.

“Siri ya kuwa mwalimu bora ni kutawaliwa na upendo wa dhati kwa taaluma, kuchangamkia masuala yanayohusiana na mtaala na kuwa mwepesi wa kubuni mbinu mbalimbali za kufundishia,” anasema kwa kukiri kwamba anapenda kuwasaidia watoto kwa sababu naye alisaidiwa hadi kufikia mahali alipo kwa sasa.

Ingawa ndoto yake ya tangu utotoni ilikuwa kusomea uuguzi, kujitosa kwake katika taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa pakubwa na Bw Alexander Maina Mwangi – mhubiri aliyemtwaa baada ya wazazi wake kuaga dunia mnamo 1995.

Bw Maina ndiye alimpokeza Mwanakombo malezi katika makao ya watoto yatima ya Shabab Children’s Home, Kaunti ya Nakuru.

“Kufariki kwa wazazi wangu kulinitikisa pakubwa maishani. Uchechefu wa karo ulitishia kunizimia mshumaa wa matumaini uliosalia kuning’inia kwenye uzi mwembamba wa imani. ”

“Niliachwa bila maangalizi yoyote na nikatorokea katika mitaa ya Mombasa kufanyia watu kazi za nyumbani na kujishughulisha na ususi baada ya walioachiwa majukumu ya kunilea kuanika azma ya kunioza kwa lazima.”

Changamoto za kila sampuli wakati huo zilimsukuma Mwanakombo kuanza kushiriki matumizi ya dawa za kulevya hadi alipokutana na Bw Maina aliyempa hifadhi katika Kanisa la PCEA Nakuru ambalo baadaye lilifadhili masomo yake katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Migori.

“Ualimu ni kazi inayokupa jukwaa la kubadilisha maisha ya watu wengi katika jamii. Ukikubali wito wa kuwa mwalimu, fahamu kwamba taifa lote la kesho linakutegemea kupitia watoto unaowafundisha. Kwa sababu hiyo, matarajio kutoka kwa mwalimu huwa ni ya kiwango cha juu sana,” anasema.

Ratiba ya Mwanakombo kila siku huanza alfajiri ya saa kumi na moja na nusu. Yeye hufika shuleni saa kumi na mbili asubuhi na mara nyingi ndiye huwa wa mwisho kuagana na lango la shule.

“Mbali na majukumu ya kawaida ya kufundisha, yapo mambo mengi ambayo watoto hustahili kufanyiwa. Kwa kuwa mwalimu pia ni mlezi, inabidi kutambua kwamba wapo watoto waliolala njaa usiku uliotangulia, wasiojua kujiosha na wale wanaopitia panda-shuka za kila namna katika familia zao.”

“Msaada kwa wanafunzi wa sampuli hii ndio hunipa tija katika kazi yangu,” anaendelea kwa kufichua kuwa anatazamia kuwa mmiliki wa makao ya watoto yatima chini ya kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Mwanakombo alizaliwa katika mtaa wa Mwandoni, eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa. Wazazi wake ni marehemu Bw Abdulrahman Juma na marehemu Bi Tumu Ali.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Kathonzweni AIC Boarding, Kaunti ya Makueni kati ya 1985 na 1991 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya St John’s Girls Kaloleni, Kaunti ya Kilifi alikosomea kati ya 1992 na 1995.

Baada ya kuhitimu ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Migori (1997-1999), alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Msingi ya Azhar Shariff, eneo la Nyali, Mombasa mnamo 2000 kabla ya Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kumwajiri na kumtuma katika Shule ya Msingi ya Kisauni mnamo 2003.

Alihudumu huko kwa miaka mitano kabla ya kupata uhamisho hadi Shule ya Msingi ya Frere Town, Mombasa alikofundisha hadi 2014 kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Kongowea mwanzoni mwa 2015.

Akiwa Frere Town, Mwanakombo ambaye pia ni mwelekezi wa michezo ya netiboli, kandanda na riadha, aliwaongoza wanafunzi wake kushiriki tamasha za muziki na drama hadi kiwango cha kitaifa mara nne katika maeneo ya Mombasa, Nairobi, Meru na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, Kaunti ya Kakamega.

Ilikuwa hadi mwaka wa 2011 ambapo alipata ufadhili wa masomo kupitia Wakfu wa Aga Khan ambao umekuwa mstari wa mbele kupiga jeki juhudi zake za kuchangia maendeleo ya jamii na kuhakikisha kwamba anawapa wanafunzi malezi bora ya kiakademia katika eneo zima la Mwandoni.

“Kupitia mradi wa Plot49 Community Policing, ninashirikiana pia na wadau wengine kutetea haki za kizazi cha sasa, kulinda usalama wa watoto, kuwaelekeza kimaadili na kuwaopoa kwenye lindi la matumizi ya mihadarati,” anaeleza.

Mbali na Jackson Mohamed Odhiambo ambaye ni mwanawe wa kupanga, Mwanakombo amejaliwa watoto watano: Abdulrahman Mwangi, 21, Adam Daudi, 18, Tumu Juma, 13, Mohamed Juma, 9, na Pili Zanira, 4.