Makala

GWIJI WA WIKI: Mzee Abdalla Ali Shamte 'DP'

March 13th, 2019 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

HERI kuwa katika jeshi la kondoo linaloongozwa na simba kuliko jeshi la simba linaloongozwa na kondoo.

Kujisaka kwa kina na kujifahamu ulivyo ni sifa muhimu kwa binadamu yeyote anayeazimia kufaulu maishani.

Heri kuwa mwerevu mjinga kuliko kuwa mjinga mwerevu.

Mwerevu mjinga huwa radhi kuelekezwa ili hatimaye awe mjuzi wa jambo.

Mjinga mwerevu ni mpumbavu asiyependa mabadiliko.

Ni mbishi anayedai kuwa mjuvi wa kila kitu.

Huwa muhali sana kwa watu wa sampuli hii kupiga hatua za kuwasogeza mbele kwa kuwa hawana uwezo wa kuishi vyema na wanadamu wenzao.

Naanza kwa kuyasimanga mashairi ya kikoa cha kizazi kipya cha leo.

Nawahimiza chipukizi wajaribu sana kuiga mitindo ya watunzi wa kale ili wadumishe uasilia na ubora wa ushairi wa jadi.

Vijana wakumbatie ufasaha wa lugha na wajitahidi mno kusarifu tungo za kuongoa nyoyo, kuonya, kukashifu matendo mabaya na kuonyesha wema ukishinda uovu.

Mshairi bora ni yule anayepania kuielewa sana hadhira yake na kutunga kazi zenye kukidhi mahitaji ya hadhira hiyo.

 

Mzee Abdalla Ali Shamte. Picha/ Chris Adungo

Kujikuza katika ushairi kunamhitaji mtu kuwa na mazoea ya kusoma kwingi na kuwa radhi kukosolewa.

Mtu haamki siku moja akawa malenga, ustadh au shaha. Ufanisi ni zao la bidii, nidhamu, imani na stahamala. Milango ya heri hujifungua yenyewe kwa watu wenye sifa hizi.

Mara nyingine inamjuzu mtu kuchukua hatua ambazo zitaifanya ndoto yake kuwa ya kweli.

Achague maono yenye matarajio na aote ndoto zenye thamani ili maazimio yake yatimie.

Huu ni ushauri wa Mzee Abdalla Ali Shamte ‘DP’ kutoka Mwembekuku, Mombasa.

Yeye ni mshairi nguli anayefahamika kwa lakabu ‘Mtumwa wa Mungu’, mchoraji hodari, mwimbaji stadi wa Taarab na mwanasoka mkongwe aliyetamba katika enzi yake ya usogora.

Maisha ya awali

Shamte alizaliwa miaka ya ’40 katika eneo la Kisauni, Mombasa (Old Town) akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto saba.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Nuru Islam mnamo 1950 kabla ya kujiunga na Arab Boys Primary School hadi alipohitimu cheti cha darasa la saba.

Mnamo 1957 alijiunga na Shule ya Upili ya Khamis, Mombasa alikosomea hadi darasa la tisa.

Katika kipindi hiki, hamasa na mapenzi yake ya dhati kwa mashairi ya Kiswahili yalichangiwa zaidi na mama mzazi aliyemfunza kusarifu tungo mbalimbali.

Ushairi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Shamte tangu akiwa mtoto mdogo. Baada ya muda mfupi, kazi zake zilianza kuchapishwa katika Jarida la Sauti ya Pwani.

Jarida hili lilianzishwa kwa lengo mahsusi la kuyachapisha mashairi ili kuwatumbuiza wapenzi kindakindaki wa sanaa hiyo.

Pili, mjomba wake marehemu Abdulrahman Sudi Boti alikuwa pia mshairi shupavu na mweledi wa kutunga na kuimba nyimbo Taarab.

Boti alikipalilia zaidi kipaji cha mpwa wake huyu baada ya kumfunza kunga zote za utunzi na kuwa mstari wa mbele kumlainishia nudhuma zake zilizoandikwa kwa ufundi na ukomavu mkubwa wa kisanii.

Kariha na ilhamu zaidi ilichochewa na Aziz Bin Abdallah Kiwillo. Huyu alikuwa mshairi mzoefu wa kipindi kirefu kutoka Afrika Mashariki aliyepanda na kuotesha mbegu za utashi wa uandishi ndani ya Shamte.

Alimfundisha Shamte kughani mashairi kwa mahadhi yaliyomwezesha kupanda kwenye majukwaa ya kila sampuli ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa katika hafla na sherehe tofauti tofauti.

Kufikia mapema miaka ya sabini, sifa za Shamte zilikuwa zimeenea kote Afrika Mashariki kutokana na ubora wa tungo zake za kuusia watu.

Kwamba angekuja kuwa mmoja wa washairi wanaostahiwa pakubwa humu nchini, azisarifu kwa ufasaha mkubwa beti za tungo zake, ulimi wake uwe mwepesi wa kukariri kazi azitungazo, sauti yake iwe kiungo cha ladha tamu ya kunogesha maghani ya kila sampuli, kisha ayaite maneno ya Kiswahili hadi yakubali kuitika kila anapojipata katika majukwaa mbalimbali ya kutukuzwa kwa ushairi wa Kiswahili; ni jambo lililokuwa bayana kwa yeyote aliyewahi kutagusana naye ujanani.

Anakiri kwamba umahiri wake katika ulingo wa ushairi ni zao la ushirikiano mkubwa kati yake na marehemu Hassan Mwalimu Mbega, Ustadh Sitara, Adinani Mwinyi na Ahmad Nassir Juma Bhalo miongoni mwa watunzi wengine waliokuwa wanachama wa Chama cha Jungu Kuu.

Jungu Kuu ni chama cha washairi kilichoasisiwa kwa malengo mahsusi ya kuandaa tamasha za malumbano ya kishairi ambapo watunzi maarufu kama vile Khamis Abdalla Chombo ‘Jemedari Mlumbi’ na Sheikh Abdalla Said Kizere wangejitosa ugani pamoja na majeshi yao kupambana kishairi na kudhihirisha weledi wao katika sanaa.

Shamte anashikilia kwamba malumbano ya aina hiyo ndiyo yaliyoipa sanaa ya ushairi nguvu zaidi.

Ili apate heshima yake na kustahiwa zaidi katika ulingo wa ushairi, Shamte aliwahi kulitembelea kaburi la mtunzi Muyaka Bin Haji (Muyaka wa Muhaji) katika eneo la Aldina, Mombasa.

Akiwa mhudumu wa Shirika la Reli la Kenya, Shamte alikuwa akiandaliwa ziara za mara kwa mara za kikazi Afrika Mashariki. Mojawapo ya ziara hizo ni ile iliyomfikisha mjini Tanga mnamo 1976.

Kubwa ambalo lilikuwa mbali kabisa na ufahamisho wake, ni kwamba hapo ndipo angekutana na watoto wa marehemu Sheikh Shaaban Bin Robert: Iqbal Shaaban na marehemu Hussein ‘Mwana Nyoka’; wote hao wakiwa ni washairi kama baba yao.

Kulizuru kaburi la Shabaan Robert kulimpa Shamte fahari isiyo kifani na kumwongezea ari ya kutunga hata zaidi baada ya kustaajabishwa sana na hazina kubwa ya maandishi ambayo marehemu alikuwa amehifadhi kwa ajili ya kuchapishwa kabla ya kifo chake.

Kazi

Shamte alifanya kazi katika Shirika la Reli kuanzia 1970 hadi Jumuiya ya Afrika ilipovunjika.

Kati ya 1977 na 1982, alikuwa tarishi katika Shirika la Posta. Katika miaka ya 1960, alichangia sana makala, habari na mashairi katika gazeti la Taifa Leo.

Mbali na kuwa mwanasoka mahiri wa iliyokuwa klabu ya Liverpool jijini Mombasa, Shamte aliwahi pia kuvalia jezi za vikosi vya Coastal Union na African Sport nchini Tanzania.

Ushawishi wake kila alipopata mpira ugani ni kiini cha timu hizo kutawazwa mabingwa wa Nyama Cup wakati wa usogora wake.

Uchoraji ni sanaa nyingine ambayo Shamte alianza kujishughulisha nayo tangu akiwa tineja.

Machapisho

Mbali na mashairi yake kuchapishwa takriban kila wiki kupitia kumbi za Ushairi Wenu, Malumbano na Sokomoko katika gazeti la Taifa Leo, Shamte anajivunia diwani Umbuji wa Umalenga.

Kutolewa kwa kitabu hiki ni zao la msaada kutoka kwa mabaharia walioamua kumfyatulia baadhi ya mashairi yake kupitia kampuni moja ya uchapishaji jijini Dubai.

Mlumbi wa Wambi (Abdalla Ali Shamte) na Kisasi cha Waoga (Jeff Mandila na Richard Maosi) ni miswada iliyosheheni mashairi mengi ya Shamte. Diwani hizi zitachapishwa hivi karibuni.

Jivunio

Nyingi za tungo zake zimekuwa zikitumiwa kutahini somo la ushairi miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu, vyuo vya walimu na wale wanaohitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE).

Uwezo wake wa kutunga mashairi kwa kutumia lahaja mbalimbali, hasa za Kingozi na Kimvita ndicho kiini cha upekee wake katika ulingo mpana wa ushairi wa Kiswahili.

Kwa pamoja na mkewe, amejaliwa watoto wawili: Ali Abdalla na Zainab Abdalla.