GWIJI WA WIKI: Nancy Okware

GWIJI WA WIKI: Nancy Okware

NA CHRIS ADUNGO

NANCY Okware alianza kuvutiwa na taaluma ya uanahabari akiwa mwanafunzi wa Darasa la Pili.

Alikuwa na mazoea ya kuiga watangazaji maarufu redioni na runingani; na wanafunzi wenzake wakamhimiza mara kwa mara awasomee taarifa za habari gwarideni au nyakati za mapumziko.

“Mamangu pia alinichochea mno. Alikuwa mwepesi wa kunirekodi kwenye kanda na akahakikisha kuwa wageni waliotutembelea nyumbani wananisikiliza. Wengi walipendezwa na “sauti yangu ya utangazaji”, anatanguliza.

Nancy alizaliwa na kulelewa katika Kaunti ya Machakos. Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kwa Tombe iliyoko Tala, Machakos kabla ya kuhamia AIC Girls, Kaunti ya Kajiado. Alijiunga baadaye na Moi Girls Isinya, Kajiado (2007-2010) kisha Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea shahada ya ualimu (Kiingereza/Fasihi) kati ya 2011 na 2016.

Mbali na wazazi wake, Bi Margaret Mbithe na Bw George Okware, wengine waliomtandikia zulia zuri la Kiswahili ni Bi Salome Sululu na Bi Mwangi waliomfundisha katika shule ya msingi na upili mtawalia.

“Aliyekuwa mwalimu mkuu wa Moi Girls Isinya, Bi Phanice Manyala, naye alinipa fursa nyingi za kuhutubia wanafunzi na walimu gwarideni. Chama cha Mijadala nilichojiunga nacho katika shule ya sekondari nacho kilichangia kunoa makali yangu katika ulumbi na kuniamshia ujasiri wa kuzungumza mbele ya umma,” anasema.

Akiwa chuoni Kenyatta, Nancy alijiunga na idhaa ya KU FM kabla ya kuajiriwa na KU TV kuwa mtangazaji. Ilikuwa hadi 2018 alipohamia KBC Channel 1 kuwa ripota wa masuala ya afya, msomaji wa habari na mwendeshaji wa kipindi ‘Tamrini’ kinachoangazia mada mbalimbali kama vile siasa, elimu, jinsia, masuala ya vijana n.k.

“Japo nilisomea ualimu, najivunia kujishughulisha na taaluma niliyoiotea tangu utotoni. Ninawashukuru wote wanaozidi kunitia moyo, kunishabikia, kuniamshia ari ya kuchapukia Kiswahili na kunipigia mhuri wa kuwa mwanahabari bora,” anaeleza.

Tofauti na wanahabari wengine, Nancy anashikilia kuwa yeye huchukua kwanza nafasi ya mtazamaji kila anapoandaa taarifa au kuendesha mahojiano kwa kujiuliza, “Je, ni kipi ambacho mwananchi wa kawaida angependa kufahamu zaidi?”

Ni kutokana na fikira na falsafa hii ambapo taarifa na mahojiano yake hulenga kujibu kwa urahisi maswali ambayo mtazamaji anaweza kuwa nayo.

“Mtangazaji au mwanahabari anastahili kuwasilisha ujumbe wowote kwa mtazamaji, msomaji au msikilizaji wake kwa njia rahisi,” anasema Nancy kwa kukiri kuwa kielelezo chake kitaaluma ni mwanahabari mzoefu wa KTN News, Zubeidah Kananu Koome.

Kubwa zaidi katika malengo ya Nancy ni kugusa na kubadilisha maisha ya Wakenya wengi kupitia taaluma ya uanahabari na kuweka hai ndoto ya kuwa miongoni mwa wadau wakuu wenye uwezo wa kutoa maamuzi muhimu katika shirika kubwa la habari.

Mwanahabari Nancy Okware wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO

Anaazimia pia kukuza na kulea vipaji vya wanahabari chipukizi katika ngazi na viwango tofauti na kuwa kiini cha motisha itakayotawala wanataaluma wengi wa kike wanaoinukia na watakaoinukia katika tasnia ya uanahabari.

“Kupata habari za kweli ni muhimu sana katika kutoa uamuzi wowote maishani. Kupitia uanahabari, ningependa kuona watu zaidi wakipata habari sahihi zinazowahusu na zenye umuhimu katika jamii,” anaongezea.

Nancy pia ni mfawidhi wa sherehe na mshauri wa wanafunzi na wanamakundi wenye azma ya kuwa wanahabari katika siku za usoni.

“Inasikitisha kuona chipukizi wanaohitaji mwelekeo wakitapatapa baada ya wenye uwezo wa kuwaelekeza kuzembea. Unapokuwa katika nafasi ya ushawishi – hata iwe ndogo kiasi kipi – usisahau majukumu yako katika jamii. Kuna wengi wanaokutegemea,” anashauri.

  • Tags

You can share this post!

Stephen Mule ahifadhi kiti cha eneobunge la Matungulu

Ruto afagia upinzani katika ngome yake

T L